Putin aapishwa rasmi kuiongoza tena Urusi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:24 PM May 07 2024
Putin aapishwa kuwa rais wa Urusi kwa muhula wake wa tano baada ya kushinda uchaguzi uliosusiwa na upinzani.
PICHA: MAKTABA
Putin aapishwa kuwa rais wa Urusi kwa muhula wake wa tano baada ya kushinda uchaguzi uliosusiwa na upinzani.

RAIS wa Urusi, Vladimir Putin ameapishwa na kuanza rasmi muhula mwingine wa miaka mitano madarakani baada ya kupata ushindi wa kishindo wa asilimia 87 ya kura.

Putin mwenye umri wa miaka 71 na ambaye ametawala siasa za urusi kwa miaka 24, ameapishwa katika hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Kremlin mjini Moscow, na kuhudhuriwa na wanasiasa waandamizi wa Urusi, pamoja na wageni waalikwa ambao ni viongozi wenye vyeo vya juu.

Katika hotuba yake baada ya kuapishwa, Putin amesema mifumo ya nchi yake ni lazima iwe tayari kukabiliana na kitisho cha aina yoyote lakini akasisitiza kuwa, Urusi haitositisha mazungumzo na mataifa ya Magharibi lakini akazitaka nchi hizo kuwa na maamuzi.

Ili kusalia madarakani, Putin aliifanyia marekebisho katiba ya Urusi miaka michache iliyopita. Mabadiliko ambayo yatamuwezesha Putin baada ya muhula wake wa sasa kumalizika mwaka 2030, kuruhusiwa kugombea tena na kusalia madarakani hadi mwaka 2036, atakapokuwa na umri wa miaka 83.