Wafariki dunia kwa kuangukiwa na nyumba

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 12:20 PM Apr 27 2024
Watu wakiwa kwenye nyumba ambayo imeanguka na kusababisha vifo vya watoto watatu wa familia moja.
Picha: Marco Maduhu
Watu wakiwa kwenye nyumba ambayo imeanguka na kusababisha vifo vya watoto watatu wa familia moja.

WATOTO watatu wa familia moja katika kijiji cha Mishepo wilayani Shinyanga, wamefariki dunia kwa kuangukiwa na nyumba kutokana na mvua inayoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini.

Taarifa zinabainisha kuwa tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana majira ya saa 9:00 alfajiri.

Watoto waliofariki dunia ni Nkamba Ngassa (13), Salamu Ngassa (8) na Gigwa Ngassa (6) na kwamba mtoto mmoja na mama yao walinusurika kifo. 

Akisimulia tukio hilo, jirani wa familia hiyo, Flora Abdallah, alisema nyumba yao tangu awali ilikuwa imeanguka ukuta mmoja lakini walikuwa wakiishi hivyo hivyo.

Alisema usiku wa kuamkia jana, mvua kubwa ilinyesha kijijini hapo na katika nyumba hiyo, walikuwa wamelala watoto wanne pamoja na mama yao, ndipo nyumba ikaanguka na kuwafukia kasoro mtoto mmoja huku mama yao ikabakizwa miguu tu.

Alisimulia kwamba yule mtoto ambaye alisalia, aliamka na kuona miguu ya Mama yake ndipo akamfukua, na kuanza kutafuta msaada kwa majirani, ili kuwafukua watoto wake watatu.

Mama wa watoto hao, Kashinje Nchembi, alisema mvua ilianza kunyesha majira ya saa 4:00  usiku na ilipofika saa 9:00 alfajiri, nyumba ilianguka na kuwafunika hatimaye kusababisha watoto  watatu kufariki dunia.

"Mimi nilikuwa nimefunikwa na kubakiza miguu tu, bahati nzuri mtoto wangu mmoja yeye alibahatika na kuja kunifukua, ndipo nikaomba msaada kwa majirani kuja kuwafukua watoto wangu wengine watatu," alisema Kashinje.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mishepo, Pastory Jackobo, alisema walipofika eneo hilo la tukio majira ya saa 10:00 alfajiri na kuanza kuwafukua watoto hao watatu, waliwakuta tayari wameshapoteza maisha.

Diwani wa Mwantini, Mpemba Jilungu, alisema tayari taratibu za mazishi juu ya watoto hao zinafanyika huku akitoa wito kwa wananchi ambao wanaishi kwenye maeneo hatarishi, ni vyema wakahama, hasa katika kipindi hiki cha mvua nyingi ili kunusuru maisha yao.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kennedy Mgani, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kubainisha kwamba tayari wameshaikabidhi miili ya marehemu kwenye familia kwa ajili ya mazishi.