Upungufu wa damu, lishe duni tatizo kwa wajawazito Z’bar

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 11:50 AM May 09 2024
Upungufu wa damu, lishe duni tatizo kwa wajawazito.
Picha: Maktaba
Upungufu wa damu, lishe duni tatizo kwa wajawazito.

UPUNGUFU wa damu na lishe duni bado ni changamoto kwa wajawazito visiwani Zanzibar, kunakosababishwa na kutokula mlo kamili wenye virutubisho ikiwamo mboga na matunda.

Ofisa Uzazi Salama kutoka Kitengo Shirikishi wa Afya ya Mama na Mtoto, Safia Haidhuru Ramadhan, ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 60 ya wajawazito wanaokwenda kujifungua wanatatizo la upungufu wa damu.

Safia amesema kukosekana kwa damu ya kutosha kwa baadhi ya wajawazito kunachangiwa kwa kiasi kikubwa kukosa mlo kamili wa lishe hasa wanawake wa vijijini.

Amesema hivi sasa kinamama wengi hawazingatii chakula cha lishe kwa kula vyakula vilivyokuwa havina faida katika afya zao ikiwemo ulaji wa chipsi kuku, urojo, udongo na vyakula vyenye mafuta mengi ambavyo havina faida kwa mama na mtoto.

Aidha, amesema mjamzito anapokwenda hospitali akiwa na damu pungufu na akicheleweshwa kufikishwa katika kituo cha afya husababisha kifo.

Pia, amesema hali ya vifo kwa wajawazito vitokanavyo na uzazi vimepungua na kwa mwaka 2022 waliripotiwa ni 70 na kwa mwaka 2023 ni 52.

Amesema kupungua kwa vifo hivyo kunatokana na elimu inayotolewa kwa kinamama wakati wanapokwenda kliniki.

Amesema licha ya kupungua kwa vifo vya mama wajawazito wakati wa kujifungua lakini bado idadi ya vifo vya watoto wachanga imeongezeka na mwaka 2021 hadi 2022  ilikuwa vifo 1,727.

Safia amesema katika kuhakikisha kuwa mtoto mchanga anakuwa salama wakati wote, kitengo hicho cha afya kinatoa elimu kwa wananchi na wajawazito juu ya kumtunza mtoto kabla ya kuzaliwa na baada ya kujifungua.

Amesema hivi sasa kinamama wanashauriwa kuwahi kwenda kliniki ili kutambuliwa mtoto hali ya makuzi yake ikoje ili kuzaliwa salama na asikumbwe na magonjwa.

Amesema msongo wa mawazo nao umeripotiwa kuwa tatizo kwa wajawazito kunakosababisha kuwatupa watoto wao baaada ya kujifungua kunakosababishwa na baba watoto kumtelekeza.