Kaya 2,500 zatarajia kupata maji kutoka Ziwa Victoria

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 05:02 PM May 09 2024
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita akishuhuduiwa utiaji Saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji wa ziwa vitoria wa kupeleka maji mtaa wa mtakuja kata ya Nyahanga.
PICHA: SHABAN NJIA
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita akishuhuduiwa utiaji Saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji wa ziwa vitoria wa kupeleka maji mtaa wa mtakuja kata ya Nyahanga.

ZAIDI ya wakazi 2,500 wa mtaa wa Mtakuja kata ya Nyahanga Halmashauri ya Manspaa ya Kahama mkoani Shinyanga, wanatarajia kuondokana na adha ya ukosefu wa maji safi na salama baada ya serikali kutoa zaidi ya Sh. milioni 452.5 za kusambaza maji ya ziwa Victoria katika mtaa huo ambao uko juu ya mlima.

Haya yamebainisha leo na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mjini Kahama (KUWASA), Mhandisi Allen Marwa, wakati wa hafla fupi ya utiaji Saini mkataba wa ujenzi mradi wa usambazaji maji na Kampuni ya Africa One Construction kwa gharama zaidi ya Sh. milioni 452.5, huku ukishuhudiwa na wananchi wa mtaa huo.

Amesema, mradi utakamilika kwa wakati na wananchi kupata maji na kuondokana na adha ya kutembea umbali wa umbali mrefu kutafuta maji ya kwenye maghati yaliyopo na sasa wanasogezewa huduma ndani ya kaya zao na kumtaka mkandarasi kuzingatia masharti ya mkataba ili amalize mapema na kupewa hati zake kwa wakati.

Diwani wa kata ya Nyahanga Pankarasi Ikongoli amesema, kero ya maji katika mtaa huo ni kubwa kulinganisha na mitaa mingine na hii ni kwasababu ya kuwa juu ya mlima, na kupata maji ilikuwa inawalazimu kushuka chini na kwenda kuchota kwenye maghati na kupanisha nayo juu kwenye makazi yao.

Amesema, sasa wanaondokana na adha hiyo na kupelekewa maji safi na salama kwenye kaya zao moja kwa moja na kuwataka kushirikana pamoja kulinda vifaa vya ujenzi visiibiwe na ukapokamilika kulinda miundombinu yake ili iendelee kuwanufaisha muda wote.

Mkazi wa mtaa huo Sauda Juma amesema, kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuondoa adha waliyokuwa wakikabiliana nayo ikiwemo ya kusafiri umbali wa kilometa nne kutafuta huduma ya maji kwenye maghati yaliyopo chini ya mlima huku wajawazito wakishindwa kuchota na kubaki majumbani.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita amewataka wananchi hao kuwa waaminifu na kulinda miundombinu ya maji ili kutoisababishia serikali hasara huku akimsihi mkandarasi kuwapatia ajira za muda zisizohitaji ujuzi wowote vijana wanaotoka mtaa huo ili kuongeza kasi ya ujenzi wake.

Amesema, serikali imekuwa ikitafuta fedha usiku na mchana kuhakikisha wananchi wake wanafikia na huduma muhimu ikiwemo maji na sasa imetoa kiasi cha Sh.milioni 184 na kumtaka Mwenyekiti wa mtaa na wananchi kukaa pamoja na kuunda timu ya kulinda vifaa vya ujenzi wakati ujenzi wake ukiendelee.