Mbunge atetea mazao yanayooza shambani

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 04:44 PM Feb 06 2025
Sofia Mwakagenda
Picha: Mtandao
Sofia Mwakagenda

MBUNGE wa Viti Maalum, Sofia Mwakagenda, ameitaka serikali kuweka mikakati kuhakikisha mazao yanayoharibika haraka kama vile parachichi, yananunuliwa kwa wakati shambani, ili kuepushia wakulima hasara.

Sophia alitoa hoja hiyo jana, bungeni, Dodoma, kupitia swali alilomuuliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,  akihoji mikakati ya serikali katika kuhakikisha mazao yananunuliwa kwa wakati shambani, ili yasioze.

Alisema baadhi ya mazao yamekuwa yakipata bei nzuri na kuwapatia wakulima faida wanayoitaka ila kumekuwa na wanunuzi ambao wamekuwa wakichelewa kununua mazao hayo na kusababisha kuoza na kuwatia hasara.

Kufuatia hali hiyo Sofia, aliishauri serikali kutoa kauli, ili kuwabana wanunuzi ambao wanachelewa kuyanunua kwa makusudi, yashuke bei na matokeo yake yaozee shambani.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu alisema mkakati wa serikali kupitia Mamlaka ya Mazao ya Bustani (TAHA), inahamasisha uwekezaji wa viwandani, ili kuhakikisha yananunuliwa kwa wakati mashambani na kuchakatwa.

“Kwa hiyo utaratibu ambao tunauweka sasa ni kuhamasisha uwekezaji kwa mazao ya kilimo kama vile maparachichi,” alisema.

Alisema mpaka sasa kuna viwanda vya uchakataji wa mazao Njombe na Mufindi, wanatarajia kujenga kingine Kilolo na  uwapo wake umechangia mazao hayo kutoharibikia shambani.