Kweli mgeni njoo mwenyeji apone tumeiona

By Joseph kulangwa , Nipashe
Published at 06:34 PM Feb 06 2025
Katuni
Mchoro: Muhidin Msamba
Katuni

WAKATI tukiwa wadogo vijijini, tulikuwa tukila ugali kwenye visosi na kitoweo kwenye vibakuli au wakati mwingine vyungu au vigae. Yalikuwa maisha ya kawaida kabisa.

Tulizoea hivyo, tukiishi bila wasiwasi na tukisoma kama kawaida ingawa tukilazimika kutembea mwendo fulani mrefu kwenda na kurudi shuleni na tukifanikiwa.

Mathalan katika familia yetu, tulikuwa na kaka yetu aliyekuwa akisoma nje ya kijiji chetu, tukiambiwa anasoma chuo cha ualimu jijini Dar es Salaam, ambako tulisimuliwa kuwa Jiji kubwa lenye kila kitu na kila maisha.

Tukiwa kijijini tulitamba sana kuwa na kaka anayesoma Dar es Salaam, tukiambiwa ndio mji mkuu wa nchi na anakoishi Rais wa nchi, wakati huo akiwa Mwalimu Julius Nyerere.

Tuliona fahari sana kusikia hata kaka yetu anaishi Jiji moja na Rais Nyerere, kwa kweli tulijisikia vizuri sana, tukiamini kuna siku atakuja atuchukue nasi tukalione Jiji hilo lenye sifa lukuki.

Majirani zetu kijijini walijua fika kuwa tulikuwa na mtu tukijimwambafai naye kwa maisha hayo ya kufikirika, utadhani nasi tulikuwa tukiishi Dar es Salaam, kutokana na hisia tulizojivika.

Siku moja nilishangazwa kumsikia mama akitwambia tusilete marafiki zetu kucheza pale nyumbani, kwani alikuwa anatarajia kufanya usafi wa mazingira ndani na nje ya nyumba, hivyo hakutaka bughudha ya michezo ya kitoto.

Tulipomhoji ilikuwaje ghafla hivyo, wakati tulizoea kucheza na watoto wenzetu hapo nyumbani tena tukila pamoja, kama ambavyo tulifanya kwao, kwani enzi hizo mtoto wa mwenzio alikuwa wako kwelikweli.

Baadaye mama alitwambia alikuwa akitarajia ugeni kutoka Dar es Salaam, kumbe kaka alikuwa akija likizo. Tulimwona mama akisafisha hata vikombe na sahani kabatini, ambavyo hatukuwahi kuvitumia tangu vinunuliwe.

Ilikuwa mara ya kwanza, kumwona mama akitoa bilauri za glasi kabatini na kuzisafisha, tayari kutumiwa na mgeni, hatukuwahi kumwona mama akitoa bakuli za udongo na kuzisafisha tayari kwa matumizi ya mgeni.

Hatukutakiwa kabisa kuvisogelea, kwani tungeweza kusababisha ajali na kuvivunja kabla mgeni rasmi hajafika kuvitumia. Na hiyo ilikuwa miongoni mwa sababu za kutukataza kucheza pale nyumbani.

Hakika mama alifanya kazi kubwa ya kuhakikisha mazingira ni safi vyombo ni safi, na hata chumba atakamofikia kaka ni mashalaah. 

Tulikatazwa hata kuingiza kitu chumbani mle, bali mama ndiye alijipa ruhusa ya kuingia kusafisha na kufunga mlango.

Tulishangaa kimoyomoyo, huku tukijiuliza sababu ya usafi ule na kwa nini mgeni wetu naye asitumie visonzo kula ugali na vibakuli vya bati au vyungu tu mbona sisi miaka yote hatujadhurika! Kwa wenye chongo nawe vunja lako jicho.

Hakuna aliyeulizwa ili atujibu, kwani kufanya hivyo ilikuwa kuhatarisha vichwa au makalio yetu kwa makwenzi na viboko mtawalia. Tulisubiri kushuhudia siku mgeni anawasili, pengine ingekuwa ile ya mgeni njoo mwenyeji apone.

Kweli siku ilipowadia, kaka yetu akawasili na mabegi yake na tukampokea kwa bashasha sana, ingawa hatukuruhusiwa pia kugusa mabegi, bali mama tu na ndiye alimkaribisha ndani nasi kubaki nje kusubiri pengine vijizawadi.

Lakini ngoma ilikuwa kwenye kuoga, kwa sababu hatukuwa na huduma ya mabomba, hivyo ilibidi sote tukaoge ziwani hapakuwa na jinsi lazima aizoee hali, bila shaka naye Dar es Salaam alikuwa akienda baharini kuogelea.

Bahati nzuri wala hakuwa na majigambo, alifurahia maisha kama kawaida, nasi tukafaidi kutumia vyombo vya kisasa kwa chakula, ingawa Mungu si Athumani, tukafaidi pia kula wali na pilau lililoandaliwa mahsusi kwa ajili ya mgeni.

Haya maisha yako sehemu nyingi, kwamba mwenyeji unajinyima raha na starehe mpaka anapokuja mgeni ndipo nawe unaishi kama binadamu, kwani siku zote unakaa umejinyima hata kwa vitu ulivyonavyo ndani. Bila shaka tumezoea hata watoto kuwanunulia chakula na mavazi mazuri siku kuu.

Bila shaka mliona tulipokuwa na Mkutano wa Nishati Dar es Salaam, jinsi Jiji lilivyokuwa safi na wazi kana kwamba halikuwa na wenyeji. 

Yawezekana wageni waliokuja kwa siku hizo mbili, waliamini wakazi wa Dar ni wafanyakazi watiifu wasiozurura wakati wa kazi.

Wapo walioamini kuwa kumbe Jiji la Dar haina vurugu za mapikipiki na mabajaji, ni shwari na tulivu wakati wote na ndiyo sababu linaamini katika nishati safi isiyochafua mazingira. Kwa kifupi waliamini Dar ni Jiji lenye mazingira safi na salama kwa binadamu kuishi!