CBE yapigia debe uchumi wa kidijitali, yaja na mtaala wa infomatiki za biashara

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:08 PM Feb 06 2025
Mkuu wa chuo CBE Profesa Edda Lwoga,
PICHA: MWANDISHI WETU
Mkuu wa chuo CBE Profesa Edda Lwoga,

CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kinatarajia kuanzisha program ya Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Infomatiki ya Biashara ili kuleta mabadiliko ya uchumi wa kidijitali na teknolojia katika kufanya biashara za kidijitali kuendana na mabadiliko ya dunia.

Hayo yalisemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa chuo hicho, Profesa Edda Lwoga, wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo ya kujadili mtaala  wa masomo hayo yaliyowashirkisha wataalamu wabobezi kutoka taasisi mbalimbali za elimu ya juu.


Wataalamu hao walikuwa wakipitia mtaala ambao umeandaliwa na chuo hicho na kutoa maoni yao ili baada ya hapo upelekwe kwa mdhibiti ambaye ni Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi  (NACTIVET) kwaajili ya kupewa ithibati na kuanza kutumika.


Amesema kuanzishwa kwa shahada hiyo ni hatua muhimu yenye kuleta mabadiliko katika kuendeleza elimu ya juu, kukuza uvumbuzi wa kiteknolojia na kuchangia ajenda ya maendeleo ya taifa.


Amesema CBE ambayo inakampasi nne nchini kwa muda mrefu imekuwa kinara katika kutoa program mbalimbali za kitaaluma na kwa kushirikana na Chuo Kikuu cha Ufini ya Mashariki kimeandaa mtaala wa informatiki za biashara.


Amesema Shahada ya PhD kwenye infomatiki za baishara ni muhimu kwani inachanganya utaalamu wa biashara na uvumbuzi wa kiteknolojia ikilenga uchanganuzi wa data, mifumo ya habari, mabadiliko ya dijiti na utafiti unaotegemea suluhisho.


“Wahitimu wa program hii wanatafutwa sana kwenye sekta ya umma na binafsi na watakuwa wahusika wakuu katika kuleta mabadiliko ya teknolojia katika tasnia mbalimbali nchini,” amesema

Wataalamu wa vyuo vikuu wakipitia mtaala wa infomatiki za biashara unaotarajiwa kuanzishwa na Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es Salaam CBE

Amesema mtaala huo utawapa wanafunzi wa Tanzania ujuzi unaohitajika ili kuendesha na kuongoza katika uchumi wa kidijitali na kuchangia katika uboreshaji wa maendeleo ya viwanda.


Amesema mtaala huo utasaidia kuongeza tija katika biashara za kidijitali na kuimarisha ushindani wa kimataifa pamoja na kuongeza ujuzi katika kufanya tafiti na uvumbuzi wa kiteknolojia katika sekta ya biashara za kidijitali.


“Mkutano huu ni muhimu katika kuunda mustakabali wa program hii  na maoni yenu wadau yatasaidia kuunda mtaala unaoakisi mahitaji ya soko la ajira na kuendana na malengo ya maendeleo Tanzania,” amesema


Amesema wanatarajia baada ya kupata ithibati mtaala huo utaanza kutumika hapa nchini na utakuwa mtaala wa kwanza kwenye biashara ya infomatiki ambao utaenda kuzalisha wataalamu watakaokuwa watafiti wabobezi katika uvumbuzi wa kiteknolojia na kuangalia mifumo itakayosaidia kwenye biashara.


“Hivi sasa teknolojia inabadilika kwa haraka sana na kuna akili mnemba (AI) yote tumeyazingatia kwenye huo mtaala na juhudi kama hizi tulianza mwaka 2014 ambapo tuliingia makubaliano na chuo cha Finland Mashariki ambao wanatoa program hiimuda mrefu,” amesema na kuongeza


“Walitusaidia sana kuwapa mafunzo wataalamu wetu ambao tumekuwa tukiwapeleka kwenye chuo hicho na mpaka sasa tuna walimu wengi ambao wameshahitimu kwenye shahada ya infomatiki ya biashara Finland na sita bado wanaendelea na masomo yao huko huko,” amesema


Angela Runyoro ambaye Mhadhiri Mwandalizi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), amesema mitaalahiyo itawezesha kuwafundisha watu kutoka ndani nan je ya nchi kupata ujuzi wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA katika biashara.


“Kwa sasa TEHAMA inahitajika katika sekta zote, hakuna namna unaweza kufanya jambo ukaikwepa na CBE wenyewe wamejikita kuanza kutengeneza wataalamu wa infomatiki za biashara kwa kujua mifumo ya kuendesha biashara kisasa,”amesema


“Hawa wataalamu watafundisha wengine watafanya tafiti watachambua mifumo inayofaa katika teknolojia ya kustawisha biashara ili watu wasifanye baishara kizamani . Hii itakuwa na manufaa sana kwa wafanyabaishara na nchi  na ulimwengu kwa ujumla,” amesema   Dk Angela