JAMHURI ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imekumbwa na mgogoro, vita na mapigano hasa Mashariki mwa nchi, kwa miongoni takribani mitatu.
DRC, idadi ya watu ni takribani 111,347,333 kwa mujibu wa tovuti inayofuatilia data mbalimbali duniani Worldometer.
Ukubwa wa eneo la ardhi DRC, linakadiriwa kuwa ni mara mbili ya nchi ya Tanzania. Upande wa Mashariki mwa DRC linajumuisha majimbo ya Ituri, Kivu kusini na Kivu Kaskazini yana jumla ya makundi ya wapiganaji zaidi ya 129.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa kitaifa na kimataifa, Dk. Richard Mbunda, akizungumza kwenye mahojiano na redio Clouds, wiki hii, ameielezea nchi hiyo, akiitaja kuwa na historia ya migogoro kwa miongo kadhaa.
Anasema utajiri wa DRC, kuanzia uwapo wa ardhi yenye rutuba, madini ambayo mengi ni tegemeo la viwanda vikubwa duniani katika vifaa vya kiteknolojia, kumeisababishia migogoro.
“Mali zilizoko DRC zikitafsiriwa inaongoa kwenye orodha ya nchi tajiri duniani, ikishika namba mbili. Tafsiri ya nchi katika uchumi wake huangaliwa Pato la Taifa (GDP).
“Kwa sasa GDP ya Marekani ni dola trilioni 25, ikifuatiwa na China wana dola trilioni 17. Ila uatajiri Congo kama ukivunwa ni dola trilioni 24, ingekuwa ya pili duniani,” anasema.
Anasema mgororo wa nchini humo unachangiwa na vyanzo kadhaa; nchi majirani; makampuni ya uwekezaji ya kigeni; ubaguzi, sababu za kisiasa na wenyewe kwa wenyewe.
Kuhusu nchi majirani, anasema kuwa miongoni mwa sababu za mgogoro DRC, kunatokana na majirani zake kuwa na maslahi ya kiusalama, kwa kuwa nchi hiyo haina utulivu,
“Nchi majirani zilikuwa na maslahi ya kiusalama, wakati huo Zaire ya Mobutu (Sese Seko), ambayo ilikuwa inakumbatia vikundi vya waasi, likiwamo la FDLR.
Baadhi ya vikundi inasadikiwa Mobutu alivifadhili. Ila vingine vilitokana na ukosefu wa utengamao wa kisiasa nchi hiyo vikazaliwa vikundi vingine vingi,” anasema.
Kwa upande wa jirani yake Uganda, kiongozi Joseph Kony, aliongoza kiundi cha waasi Lords Resistance Army (LRA), walikuwa wanajipanga kwenda kumpindua Kagame.
Kwa hiyo Kagame naye akaona Congo inatunza kikundi cha waasi ambao wanaweza kuja kunipindua. Akawa na kikundi chake. Wote walijipanga wakiwa ndani ya DRC. Rwanda nayo ikawa inajilinda ikiwa ardhi ya DRC.
Angola, pia nao walikuwa wako Congo, walikuwa wanapata msaada na ushirikiano kutoka kwa Mobutu. Kwa hiyo aliwasaidia kuwaunganisha vikundi vya Rwanda, Uganda na Angola, kumsaidia.
Kilikuwapo kikundi kilichokuwa kinaungwa mkono na Rwanda, ‘Rarry for the Congolese Democracy’-RCD kiliongozwa na Ernest Wamba dia Wamba. Likaendelea kubadilika kulingana na wakati hadi kufikia kuwa M23.”
Anasema kipindi hicho miaka ya 1997 kilikuwapo vikundi vingi DRC kwa maslahi tofauti na vlikuwa vinaungwa mkono kutoka baadhi ya nchi zao.
FDLR, wanaodai wanajipanga kwenda kuikomboa Rwanda, bado wapo DRC. Baadae kundi ambalo lilikuwa linaungwa mkono na Rwanda, baadae likabadilika kuwa CNDP kama kundi la waasi na mwaka 2009 kulikuwa na makubaliano chini ya Joseph Kabila, Rais wa wakati huo DRC. CNDP wakabadilika kuwa chama cha siasa.
CNDP lilikuwa ni kundi la waasi lililoanzishwa na Laurent Nkunda katika eneo la Kivu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Desemba 2006. CNDP ilihusika katika mzozo wa Kivu, mzozo wa silaha dhidi ya jeshi la Congo. Januari 2009, CNDP iligawanyika na Nkunda alikamatwa na serikali ya Rwanda na kikundi chake kilichogawanyika, kinachoongozwa na Bosco Ntaganda, kilipangwa kuunganishwa katika jeshi la taifa.
“Malengo makubwa ya wao (CNDP) kuwa sehemu ya serikali hayakutimia, likaamua kujiondoa, wakaunda M23, kwa maslahi yao wenyewe kwa sababu wanajiangalia kama Wacongo, ingawa Wacongo wao wanaangalia kama watu wakuja. M23 hamu yao ni kuwa sehemu ya utawala wa Congo,” anafafanua.
Anasema maslahi mengine kwa nchi ya DRC yanatoka nje ya nchi, kutokana na uwapo wa makampuni yaliyowekeza hasa katika uchimbaji wa madini
UTAJIRI
Utajiri wa DRC, unaweza kuutaja uliobakia kwenye nadharia, licha ya kuwa ni nchi tajiri zaidi duniani kwa maliasili.
Ina madini mengi ghafi ambayo hayajatumika na yanadaiwa kuwa`na thamani ya hadi takriban dola trilioni 24.
Amana hizo ni pamoja na akiba kubwa zaidi ya madini ya coltan na kiasi kikubwa cha madini ya kobalti.
Hata hivyo kutokana na urahisi wa uchimbaji wa rasilimali hizo, taifa hilo utajiri wake wa madini hayo, umegeuka shubiri.
DRC ina maji yasiyo na kikomo, kutoka mto wa pili kwa ukubwa duniani, Congo, hali nzuri ya hewa na udongo wenye rutuba mbali na madini kama vile shaba, dhahabu, almasi, urani, koltani na mafuta ni baadhi tu ya madini ambayo yanapaswa kuifanya kuwa moja ya nchi tajiri zaidi duniani.
NYONGEZA: MTANDAO
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED