WANANCHI wa Kata ya Lukobe, Manispaa ya Morogoro, wameiomba serikali kuona umuhimu wa kujenga barabara ya Kilombero-Mazimbu Farm kwa viwango bora, ili kukabiliana na changamoto ya kujaa maji.
Wamesema barabara hiyo wakati wa mvua za masika hukatisha mawasiliano, kwa saa kadhaa, na kuwasababishia maafa na kuwarudisha nyuma uchumi wao.
Wananchi hao walisema hayo jana, wakati wakiongea na vyombo vya habari, kutokana na mvua za masika inayotarajia kuanza.
Mmoja wa wananchi hao, dereva wa bajaji, Frank Alpakshard, aliiomba serikali iweke miundombinu rafiki kwenye barabara hiyo, ili kuifanya kuwa salama wakati wote na kuwaepusha na adha ya kuharibu vifaa vyao vya moto na kuingia gharama za matengenezo.
Getruda Cosmas, ni mkazi wa mtaa wa Tushikamane, aliiomba serikali kuona umuhimu wa kuwajengea barabara kwa haraka, ili kuwaepusha kushindwa kwenda kazini kwa siku kadhaa, kutokana na mvua na barabara kutopitika na kulazimika kuvuka kwa miguu kwenye maji mengi na hivyo kuhatarisha afya zao.
Anasema ujenzi wa barabara hiyo, utasaidia kudhibiti maji mengi yanayotoka kwenye maeneo na wilaya za jirani na milima inayozunguka eneo hilo na kuwaondolea wananchi changamoto zinazowakabili mara kwa mara.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED