Wanafunzi wanaotumia dawa za kulevya shuleni kuchunguzwa

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 09:17 AM May 09 2024
Bunge kuchunguza wanafunzi wanaotumia dawa za kulevya shuleni.
Picha: Maktaba
Bunge kuchunguza wanafunzi wanaotumia dawa za kulevya shuleni.

BUNGE limeagiza serikali kufuatilia madai ya nusu ya wanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Ukombozi iliyoko Kata ya Saranga, Ubungo mkoani Dar es Salaam kulala darasani asubuhi kwa kile kilichoelezwa kuwa ni matumizi ya dawa za kulevya.

Mwenyekiti wa Bunge, Deodatus Mwanyika, ametoa maelekezo hayo kwa serikali bungeni baada ya Mbunge wa Kibamba (CCM), Issa Mtemvu, kutoa taarifa hiyo kuwa kuna tatizo la maadili ya watoto ndani ya jimbo hilo.

“Katika Jimbo la Kibamba ambako Rais amejenga shule nzuri kwa gharama ya zaidi ya Sh. milioni 400, Shule ya Ukombozi yenye watoto 1,400 ikifika saa 5:00 asubuhi, zaidi ya asilimia 70, yaani watoto 600, wameshalewa dawa za kulevya wanalala darasani. Hali hii ni mbaya kwa jamii,” amesema Mtemvu alipokuwa akimpa taarifa mchangiaji ambaye ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini (CCM), Hassan Kungu.

Kungu amesema anakubaliana na taarifa hiyo kwa kuwa ndio uhalisia na kwamba shule za sekondari bila kuwa na bweni wanafunzi wengi watapotea kimaadili.

Akizungumza wakati wa kuahirisha kikao cha bunge, Mwanyika amesema: “Kuna taarifa imetolewa na Mbunge wa Kibamba inaweza kuleta taharuki katika mazingira ambayo tunaongelea maadili. Tunaambiwa watoto saa tano mamia kwa mamia wamelewa, nadhani serikali mlifuatilie na kuleta taarifa ndani ya Bunge.”

Baada ya maelekezo hayo, Mwanyika  alimpa nafasi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, ambaye amesema amepokea maelekezo hayo na kwamba suala hilo limeishtua serikali kama shule ina zaidi ya watoto 1,000 na inapofika muda huo watoto 600 wanalala darasani kwa kulewa.

“Taarifa kidogo imetushtua kama serikali, tunapokea maelekezo yako kwa sababu tunafahamu serikali imejizatiti kupambana na matumizi ya dawa za kulevya na nguvu ya pekee imewekwa kwa watoto wa shule za msingi na sekondari,” amesema.

Amesema kwa mifumo ya elimu iliyopo kama kuna upungufu huo wa kushindwa kubaini suala hilo mapema itakuwa ni bahati mbaya.

“Kwa niaba ya serikali napokea maelekezo ya kiti na tutafuatilia ili kuwaokoa watoto na janga hilo na tufuatilie mifumo yetu inayoshindwa kujisimamia ili watoto kuenenda kwenye maadili mema,” amesema.