Ulawiti wa watoto Shinyanga wadhibitiwa

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 02:20 PM May 09 2024
Ulawiti wa watoto kudhibitiwa.
Picha: Maktaba
Ulawiti wa watoto kudhibitiwa.

VITENDO vya baadhi ya watoto wa kiume kulawiti katika Kata ya Iselamagazi wilayani Shinyanga vimedhibitiwa baada ya watuhumiwa kukamatwa na kuchukuliwa hatua kali.

Hayo yamebainishwa na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Iselamagazi, Amos Daudi, wakati akizungumza na Nipashe Digital kuhusu wanavyoshughulika na matukio ya ukatili dhidi ya watoto na wanawake.

Kwa mujibu wa Daudi, kwenye kata hiyo awali kulikuwa na matukio mengi ya ulawiti dhidi ya watoto wa kiume, yakifanywa na watu wazima.

Amesema serikali baada ya kupata taarifa kuhusiana na vitendo hivyo vya kinyama,  ilianza kuzifanyia kazi, kuwakamata watuhumiwa na kufikishwa mahakamani.

Ofisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Aisha Omary, ametoa wito kwa wazazi kujenga tabia ya kuwachunguza watoto mara kwa mara ili kubaini kama wanafanyiwa vitendo hivyo.

"Kuna mtoto mmoja alianza kulawitiwa akiwa darasa la kwanza na kubainika akiwa darasa la tatu ameharibiwa vibaya sehemu za haja kubwa," amesema Aisha na kuwataka watoto kutoa taarifa za ukatili katika mabaraza ya shuleni ili kutokomeza vitendo hivyo katika jamii.

Mmoja wa watoto wa Iselamagazi, amesema walikuwa wakifanyiwa vitendo hivyo baada ya kurubuniwa kwa kupewa hela za kutumia wanapokuwa shuleni.

Amesema kwa sasa hawafanyiwi ukatili huo baada ya vitendo hivyo kudhibitiwa, watuhumiwa kukamatwa na kufikishwa mahakamani.