Yanga, Azam fainali ya kisasi Kombe la FA

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:25 AM May 20 2024
news
Picha: Mtandaoni
Stephane Aziz Ki.

HATIMAYE fainali ya Kombe la Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), iliyopangwa kufanyika Uwanja wa Tanzanite, Babati mkoani Manyara, utazikutanisha Azam FC na Mabingwa Watetezi, Yanga kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Hii ni baada ya Yanga jana kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya nusu fainali iliyochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Ilibidi Yanga isubiri hadi dakika ya 100 ili kupata bao baada ya mechi hiyo kuingia kwenye dakika 120 kufuatia dakika 90 kumalizika bila kufungana.

Bao hilo lilifungwa na kiungo, Stephane Aziz Ki kwa shuti kali la mguu wa kushoto baada ya kupokea pasi ya Pacome Zouzoua aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Maxi Nzengeli.

Mpira ulianzia kwa Khalid Aucho aliyemnyang'anya mchezaji mmoja wa Ihefu na kuipeleka wingi ya kulia ambako Pacome alikuwapo, akaingia ndani kidogo na kumtengea mfungaji wa bao.

Bao hilo limeipeleka Yanga fainali kwenda kuumana na Azam FC, ambayo ilitinga hatua hiyo juzi, ilipoifunga Coastal Union mabao 3-0, Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Fainali hiyo itakuwa inajirudia tena kwani msimu uliopita timu hizo zilikutana Juni 12, mwaka jana, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Yanga ilifanikiwa kutwaa ubingwa baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0, lililowekwa wavuni na Kennedy Musonda.

Jana timu zote mbili zilianza kwa kucheza pasi ndefu kwenda kwenye wingi zao za kulia na kushoto, lakini mabeki wa pande zote walikaa imara.

Dakika ya 12, Yanga ilianza kulisalimia lango la Ihefu, pale mshambuliaji Clement Mzize alipoupata mpira akiwa ndani ya eneo la hatari, akiwa amebaki golikipa wa Ihefu, Khomein Aboubakar, shuti lake dhaifu liliishia mikononi mwa kipa huyo.

Dakika tano baadaye Ihefu ilijibu kwa shambulizi kupitia kwa mshambuliaji raia wa Togo, Marouf Tchakei, ambaye aliambaa na mpira kutoka katikati ya uwanja na kabla hajaingia ndani ya boksi, aliachia shuti kali lililompita kipa wa kimataifa wa Mali, Djugui Diarra, lakini badala ya kutinga wavuni ukatoka nje.

Yanga nayo ilikosa bao la wazi dakika ya 27, pale Aziz Ki alipounganisha vibaya krosi ya Mzize kutoka pembeni kidogo upande wa kulia.

Dakika kumi kabla ya mechi kwenda mapumziko, beki wa kulia wa Yanga, Nickson Kibabage alianguka peke yake uwanjani, baada ya kufanyiwa matibabu akatolewa nje nafasi yake ikachukuliwa na Joyce Lomalisa.

Joseph Mahundi itabidi ajilaumu mwenyewe, alipokosa bao la wazi dakika za nyongeza kabla ya kwenda mapumziko, alipompora mpira, Mohamed Ibrahim 'Bacca', akakimbia nao mpaka ndani ya boksi huku kipa Diara akiwa ametokea, alipiga shuti la ovyo mpira ukatoka nje wakati goli likiwa tupu.

Mshambuliaji Rupia alikaribia kuifungia Ihefu goli lakini mpira wake wa kichwa ulipanguliwa kiufundi na Diarra.

Kipindi cha pili hakikuwa kizuri kama cha kwanza, kwani timu zote zilionekana kufunga njia na mpira kuchezwa kati zaidi, huku kukiwa na mashambulizi machache.

Pia dakika za mwisho, Ihefu ilionekana kupaki basi zaidi na kushambulia mara chache.