IMEELEZWA uongozi wa klabu ya Simba umetenga fedha za kutosha kwa ajili ya kufanikisha usajili wa kiungo wa klabu ya Azam FC, Feisal Salum 'Fei toto' ili ajiunge na timu hiyo.
Mbali na Fei Toto, Simba pia inaangalia uwezekano wa kumsajili kiungo wa Yanga, Stephane Aziz Ki katika harakati zao za kujiimarisha na kurudisha heshima ya klabu hiyo.
Aziz Ki ni kinara wa mabao kwenye ligi ambapo mpaka sasa ana magoli 15 akilingana na Fei Toto, hata hivyo mkataba wa mchezaji huyo ndani ya Yanga unamalizika mwishoni mwa msimu huu.
Mbali na Simba, pia inaelezwa kuna timu kutoka Afrika Kusini ambazo zinafanya mchakato wa kumsajili kiungo huyo wa kimataifa wa Burkina Faso.
Akizungumza na Nipashe jana, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema klabu hiyo ipo makini katika usajili na mchezaji wanayemtaka hawatashindwa kumsajili.
Alisema wanafahamu kiungo huyo mkataba wake unaenda ukingoni ingawa kwa Feitoto mambo sio mepesi kutokana na nyota huyo kuwa na mkataba hai na Azam.
“Ni kweli hao wachezaji wawili wapo kwenye mipango yetu mmoja mkataba wake umefikia ukingoni na bado hajasaini mkataba mpya, kwa Fei Toto ni suala la kuweka fedha mezani ili kumchukua," alisema Ahmed na kuongeza,
"Pia kuna wachezaji wengine wapya tunawafuatilia sokoni kulingana na mapendekezo ya benchi la ufundi kwa ajili ya kuwasajili na kuimarisha kikosi chetu kwa ajili ya msimu ujao,” alisema Ahmed.
Alisema uongozi wa klabu hiyo utawasilisha ofa yao kwa Azam kuangalia uwezekano wa kumchukua kiungo huyo wa timu ya taifa 'Taifa Stars' na Zanzibar.
Kuhusu taarifa za beki wao Henock Inonga kuondoka kwenda kwenye mapumziko, Ahmed alisema beki huyo ameondoka kwa ruhusa maalum bado na ni mali ya Simba hadi msimu ujao mkataba wake unapomalizika.
“Hakuna ukweli kuwa kuna ofa imekuja kwetu, Inonga ni mchezaji wetu, watu wasimgombanishe mchezaji na mashabiki wa Simba, hivyo Inonga atarejea nchini kuitumikia timu yake endapo hakutakuwa na ofa kutoka kwenye timu nyingine," alisema Ahmed.
Katika hatua nyingine, Ahmed alisema kikosi cha timu hiyo kinaendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo dhidi ya Geita Gold FC utakaochezwa kesho.
“Bado tunahitaji alama tisa katika michezo mitatu iliyosalia, hii ni muhimu sana kwetu kuzipata ili kujihakikishia nafasi ya pili na kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Ahmed.
Simba ipo nafasi ya tatu ikiwa na alama 60 wakilingana na Azam wanaoshika nafasi ya pili lakini wakiwa na uwiano mzuri wa magoli.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED