BIRTHDAY YA SAMIA; Shinyanga yapanda miti 500

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 12:51 PM Jan 27 2025
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, akiongoza upandaji miti katika kusherehekea kumbukumbu ya kuzaliwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, akiongoza upandaji miti katika kusherehekea kumbukumbu ya kuzaliwa Rais Samia Suluhu Hassan.

MKOA wa Shinyanga, umesherehekea kumbukumbu ya kuzaliwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kupanda miti 500 katika shule ya msingi Mapinduzi, iliyoko Manispaa ya Shinyanga, mkoani hapa.

Upandaji huo umefanyika leo, Januari 27, 2025, siku ambayo Rais Samia, anatimiza umri wa miaka 65 tangu kuzaliwa kwake, mwaka 1960.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, amesema ni siku njema kwa Watanzania katika kusherehekea siku ya kuzaliwa Rais Samia, na kwamba katika mkoa huo, wameamua kupanda miti ili kuendelea kutekeleza kampeni ya kutunza mazingira na kukabiliana na madiliko ya tabianchi.

Shinyanga yapanda miti 500
“Miti hii 500 ambayo tumeipanda leo, tunasherehekea siku ya kuzaliwa Rais Samia.Tunajivunia kupanda mti wa kitaifa hapa mkoani Shinyanga na ni sehemu ya kutekeleza kampeni yake ya upandaji miti.

“Naagiza miti hii itunzwe na ikue vizuri, ili tukirudi hapa tukute imeweka mandhari nzuri ya kijani,” amesema Macha.

Amewasihi wananchi, taasisi na halmashauri zote  sita za mkoa huo, kuendelea kupanda miti zaidi katika maeneo yao, pamoja na ya machimbo ya madini huku akiagiza wafugaji wa mifugo wanachunga kwenye maeneo yaliyopandwa miti, wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Shinyanga yapanda miti 500
Amewaonya wananchi katika vitendo vya kukata miti hovyo bila ya kupata kibali kutoka kwa mamlaka husika na kwamba mti mmoja ukikatwa, inapaswa kupandwa zaidi ya miwili.

Macha amempongeza Rais Samia, kwa utendaji wake mzuri, akitaja mchango wake katika uongozi wa kimataifa na hata kuongoza Mkutano Mkuu wa Nishati wa Wakuu za Nchi za Afrika, unaofanyikia hapa nchini.

Amesema masuala ya nishati pia yanasaidia katika kuondokana na utegemezi wa matumizi ya mkaa, ambao husababisha uharibifu wa mazingira kwa kukata miti hovyo.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amesema wataendelea kutekeleza maagizo ya kampeni hiyo ya kupanda miti.

Shinyanga yapanda miti 500
Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Elias Masumbuko, amesema watazingatia, ikiwamo kufuatilia miti iliyopandwa na kuhamasisha wananchi pamoja na,ili kuifanya Shinyanga iwe ya kijani, kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mwanafunzi Godfrey Mgeta, kutoka shule hiyo, alieleza furaha yake kwa kushiriki upandaji miti, akisema ina umuhimu na watakuwa mabalozi wa kuhamasisha kupanda majumbani.