MKUU wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amekabidhi pikipiki 15, kwa wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo, ili zitumike kufanikisha kazi ya utoaji wa chanjo mbalimbali.
Kanali Mtambi, alikabidhi pikipiki hizo mwishoni mwa wiki, kwa wakurugenzi wa halmshauri na kuwaagiza wazitumie kwa kile kilichokusudiwa na zudumu kwa muda mrefu.
“Pikipiki hizi ni mpya, hivyo watumishi watakaotumia wahakikishe kile kilichokusudiwa, ili kuleta matokeo chanya katika huduma za chanjo pale zitakapohitajika kutolewa," amesema Kanali Mtambi.
Mkuu huyo wa mkoa, amewataka wazazi na walezi kuwapeleka watoto kwenye chanjo na kuachana na imani potofu, kuwa zina madhara na kusababisha wengine wasichanjwe.
"Nimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo amekuwa akitujali Watanzania, kwa kutoa vifaa hivyo, kwa ajili ya kurahisisha chanjo mkoani Mara," amesema.
Awali akitoa taarifa kuhusu pikipiki hizo, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Gerald Kusaya, amesema Wizara ya Afya pia imetoa gari moja, kwa ajili ya kufanikisha utoaji wa chanjo mkoani humo.“Gari litatumiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, kusambazia chanjo, lakini pikipiki 15 zitatumiwa na wasimamizi wa chanjo. Halmashauri sita kati ya tisa, zimepewa pikipiki mbili kila moja," amesema Kusaya.
Hafla ya kukabidhi pikipiki hizo, ilihudhuriwa wakuu wa wilaya, makatibu tawala wa wilaya, menejimenti ya sekretarieti ya mkoa, wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa, timu ya usimamizi wa sekta ya afya mkoa.
Wengine ni waganga wakuu, maofisa lishe, wahazini, maofisa utumishi na elimu msingi pamoja na sekondari, maafisa mipango wa halmashauri zote mkoani humo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED