Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Godfrey Mnzava ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kutekeleza agizo la Rais Dk. Samia Suluhu Hassan la kutangaza zabuni za fedha za umma kwa kutumia mfumo wa kielektroniki wa (NeST).
Amesema kuwa Rais aliagiza zabuni zote za fedha za umma kutangazwa kwa kutumia mifumo ya kielektroniki kwa lengo la kuongeza uwazi na kupunguza malalamiko na upendeleo kwenye michakato ya zabuni.
Ameyasema hayo wakati wa ziara ya kutembelea na kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa usambazaji maji wa Dar es Salaam ya Kusini unaotekelezwa na DAWASA.
Ameongeza kuwa katika mradi huu Mamlaka imezingatia agizo la Rais la kutumia mfumo wa kielektroniki wa kutangaza zabuni na hivyo kupunguza upendeleo na malalamiko yaliyokuwa kwa muda mrefu.
Amebainisha kuwa Mwenge wa Uhuru Kitaifa umeridhika na utekelezaji wa mradi huu ambao unalenga kunufaisha wakazi wa maeneo haya ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais la kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa urahisi na kwa ukaribu, wasiende umbali mrefu kupata maji.
"Niwatake Mamlaka kuendelea na utekelezaji wa mradi huu kwa ufanisi ili ukamilike kwa wakati na wananchi wapate huduma ya maji," ameeleza.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ameipongeza Serikali ya Rais Dk. Samia kwa kudhihirisha nia yake ya kumtua Mama ndoo kichwani kwa kuidhinisha fedha za utekelezaji wa mradi huu mkubwa wa maji utakaotatua changamoto ya maji kwenye wilaya hiyo.
Ameongeza kuwa kupitia mradi huu unaotekelezwa huduma ya maji kwa wananchi wa Jimbo la Ilala itakuwa imara zaidi.
"Niwapongeze DAWASA kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kutekeleza mradi huu kwa ufanisi, hizi ni jitihada za kuigwa," ameeleza Mpogolo.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Ndugu Kiula Kingu amemshukuru Rais Dk. Samia kwa kuridhia kutoa fedha Shilingi bilioni 36.9 za kutekeleza mradi huu mkubwa unaolenga kunufaisha wananachi wa majimbo matano uchaguzi ikiwemo Ukonga, Segerea, Ubungo, Kibamba na Ilala.
Ameongeza kuwa eneo hili lilikuwa na changamoto ya muda mrefu ya maji na hata maji yaliyokuwa yanapatikana kwenye visima hayakuwa sio masafi.
"Hivyo kupitia mradi huu ambao unahusisha ujenzi wa tenki kubwa la lita milioni 9, ujenzi wa mtandao wa mabomba ya kusambaza maji kwa umbali wa kilomita 113, pamoja na ujenzi wa kituo cha kusukuma maji kinachonjengwa Kibamba, tunaimani tatizo la maji litaisha kabisa.
Mradi wa Kusambaza maji Dar es Salaam ya Kusini unatekelezwa na Mkandarasi wa M/S SINOHYDRO kutoka China na Mhandisi Mshauri ni kampuni ya M/S SCET TUNISIE ya nchini Tunisia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED