ACT yatoa neno bajeti finyu ya elimu

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 09:49 AM May 09 2024
Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa ACT-Wazalendo, Hamidu Bobali.
Picha: Maktaba
Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa ACT-Wazalendo, Hamidu Bobali.

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimesema kuna haja serikali kutenga bajeti ya Sh.bilioni 50.2 ili kuongeza idadi ya ajira za walimu kwa shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu, kuongeza wakufunzi na wahadhiri angalau 5,000 ili kupunguza uhaba wa walimu vyuoni na vyuo vikuu.

Aidha, kimesema serikali itenge bajeti ya kutosha na kuongeza kiwango cha ruzuku kwa shule za msingi na sekondari kwa kiwango cha Sh. 25,000 kwa mwanafunzi wa shule ya msingi na Sh. 58,000 kwa mwanafunzi wa sekondari pamoja na kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa sera ya elimu kwa ajili ya ukaguzi na uthibiti ubora wa shule.

Kadhalika, chama hicho kimeiomba serikali kubeba gharama za ada, malipo ya mafunzo kwa vitendo, fedha za vitabu na viandikwa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na kwamba kufanya hivyo kutaondoa minyukano na kutatoa fursa sawa ya kupata elimu kwa wanafunzi bila kujali vipato vyao.

Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa ACT-Wazalendo, Hamidu Bobali, amesema hayo jana Dar es Salaam alipotoa taarifa ya tathmini ya uchambuzi wa bajeti ya Wizara hiyo ya mwaka wa fedha 2024/25 iliyowasilishwa Bungeni Dodoma na Waziri mwenye dhamana.

Bobali amesema kufanya hivyo kutasaidia kuondoa matabaka ya watoto wa wenye nacho na wasio nacho kwenye kuwania elimu. 

“Kwenye ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020 ACT-Wazalendo tulibainisha kuwa itafuta mikopo yote ya miaka ya nyuma iliyotolewa kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Italipa ada ya masomo, fedha za vitabu na gharama za mafunzo kwa vitendo kwa kila mwanafunzi anayedahiliwa kwenye chuo kikuu,” amesema Bobali.

“Hotuba ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/23 haijajibu changamoto za muda wote kuhusu mfumo wa ugharamiaji wa elimu ya juu.”

Kimependekeza kwamba ni vema usimamizi wa sekta ya elimu ukasimamiwa na wizara moja badala ya tatu kama ilivyo sasa.

“Kugawanywa katika wizara takribani zaidi ya tatu yaani, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto (kwa baadhi ya masuala) kuna fanya mpango wa bajeti kwenye sekta ya elimu kuyumbishwa kwa vipaumbele vyake,” amesema Bobali.

Bobali amesema pamoja na Sera ya Elimu ya mwaka 2014 na mitaala yake kufanyiwa marekebisho na kuanza utekelezaji wake, bado kuna mambo yanahitaji marekebisho ambayo yatasaidia kuimarisha na kuboresha sekta ya elimu ikiwamo kuweka wazi lugha ya Kiswahili kuwa rasmi kufundishia na kujifunzia.

Amesema lugha hiyo inatakiwa kuwa ya kufundishia na kujifunzia kwa ngazi zote na kupendekeza lugha nyingine zifundishwe kama somo.

Bobali amesema katika shule na vyuo, sera ya elimu haijaweka bayana juu ya lugha ya kufundishia kati ya Kiswahili na Kiingereza na hivyo, kuendeleza utata wa kutumia lugha ya Kiswahili kwa ngazi ya awali na elimu msingi, huku katika ngazi ya sekondari na chuo ikitumika ya Kiingereza. 

Jambo lingine ambalo amesema linahitaji marekebisho ni pamoja na suala la ugharimiaji wa elimu na mafunzo, kwamba sera hiyo haijaonyesha nani atagharamia upatikanji wa elimu katika kila ngazi, ijapokuwa imeonyesha wazi kuhusu uhaba wa bajeti na ongezeko na mahitaji.