Kesi za udhalilishaji 471 zaripotiwa ndani ya siku 90

By Hawa Abdallah , Nipashe
Published at 11:27 AM May 09 2024
Kesi za udhalilishaji 471 zaripotiwa mahakamani.
Picha: Maktaba
Kesi za udhalilishaji 471 zaripotiwa mahakamani.

KESI 471 za udhalilishaji wa kijinsia visiwani Zanzibar zimeripotiwa katika maeneo mbalimbali katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu.

Hayo yamesemwa na ofisa kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar, Ramla Hassan Pandu, wakati akiwasilisha mada katika warsha ya usambazaji wa matokeo ya uhamasishaji wa matumizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa asasi za kiraia.

Amesema katika vitendo hivyo 240 ni vya ubakaji, 31 kulawiti, 19 kuingiliwa kinyume na maumbile, shambulio la aibu 50 na kutorosha ni saba.

Ramla amesema bado kuna changamoto ya upatikanaji wa takwimu halisi hasa kwa matokeo hayo kutokana na baadhi ya familia za waathiriwa kumalizana nyumbani.

Amesema licha ya asasi za kirai pamoja na taasisi za serikali kuendelea kutoa elimu katika jamii juu ya kuripoti matukio haya katika vyombo vinavyohusika, lakini bado baadhi ya jamii hawafanyi hivyo.

Ramla amesema kulingana na hali hiyo inaonesha kuwa licha ya jamii kupewa elimu juu ya athari za kutoripoti vitendo vya udhalilishaji, lakini bado hawana hamasa ya kuripoti matukio hayo.

“Tunaona jitihada kubwa zinachukuliwa na taasisi za kiserikali, mashirika na hata hizi taasisi zisizo za serikali lakini bado baadhi ya jamii hawajahamasika kuripoti haya matukio hasa kwa yale yanayafanywa ndani ya familia,” amesema.

Ofisa kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Asha Mahmoud, akiwasilisha takwimu za ajali za barabarani kwa miezi mitatu alisema ajali 550 zimeripotiwa.

Amesema chanzo cha ajali hizo mara nyingi zinatokana na uzembe wa madereva kutofauta sheria za barabarani ikiwamo mwendo kasi.

Asha amesema katika takwimu hizo ajali nyingi zimesababishwa na madereva wanaume, huku ajali ambazo zimesababishwa na madereva wanawake zikiwa chache.

Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Balozi  Mohmmed Haji Hamza, amesema takwimu hizo za sensa zitawasaidia taasisi hizo za kiraia katika miradi yao ya kuisaidia jamii.

Amesema kupitia takwimu hizo za idadi ya watu na makazi wataweza kupanga mipango yao kwa mujibu wa mahitaji yanayohitajika katika sehemu husika kulingana na idadi iliyopo.

“Takwimu hizi zitaisaidia serikali katika maendeleo lakini zitawasaidia katika kupanga mipango yenu ya miradi ambayo mnaifanya kupitia mambo mbalimbali,” amesema.

Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Salum Kassim Ali, amesema watajitahidi kutoa takwimu za matukio mbalimbali kila mwezi kupitia vyombo vya habari pamoja na mitandao ya ofisi hiyo ili jamii ijue kinachoendelea katika maeneo yao.

Hivyo, amewataka viongozi wa asasi za kirai kutosita kufika katika ofisini kwake kuchukua takwimu wanazozihitaji kwa ajili ya kufanyia kazi katika mambo yao wanayopanga.