TIMU ya Taifa ya vijana ya kuogelea itaondoka nchini Novemba 21, mwaka huu kuelekea Burundi ili kushiriki mashindano ya mchezo huo ya Kanda ya Tatu Afrika.
Mashindano hayo yanatarajia kufanyika Novemba 23 na 24, mwaka huu nchini humo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Michael Livingstone, alisema mashindano hayo yatashirikisha vijana wenye umri kuanzia miaka 12 na kuendelea na Tanzania itawakilishwa na waogeleaji 41.
"Maandalizi kuelekea katika mashindano hayo yanaendelea vizuri, kila klabu inajinoa na kwa upande wa wachezaji waliopo Dar es Salaam huwa wanafanya mazoezi asubuhi kwenye bwawa la kuogelea IST chini ya HPT, na jioni wanafanya kwenye mabwawa mengine, " alisema Livingstone.
Kocha huyo alisema mashindano hayo yatashirikisha waogeleaji kutoka klabu za Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar huku lengo lake ni kuwapa uzoefu wachezaji wa hapa nchini kuelekea michuano ya dunia.
"Tunaiomba serikali itusaidie kuziandaa timu za vijana ili ziwe zinapata mazoezi ya muda mrefu, mara nyingi wazazi huwa wanatumia gharama zao ili watoto wafanye mazoezi, endapo wakishindwa gharama hizo tunapoteza vipaji, " kocha huyo alisema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED