Gamondi: Dube bado, afadhali kidogo Baleke

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:15 AM Jul 24 2024
KOCHA wa Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga, Miguel Gamondi.
Picha: Mtandao
KOCHA wa Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga, Miguel Gamondi.

KOCHA wa Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga, Miguel Gamondi, amesema mchezaji wake Prince Dube hayupo kwenye kiwango bora, ikiwamo kutokuwa na utimamu kwa mwili kutokana na kutocheza soka kwa muda mrefu, huku akibainika angalau Jean Beleke alionyesha ana afadhali.

Akizungumza jana kuelekea katika mchezo wa leo wa Kombe la Mpumalanga dhidi ya TS Galaxy, utakaochezwa jioni kwenye Uwanja wa Mbombela nchini Afrika Kusini, Gamondi, alisema Dube hayupo kwenye kiwango chake ndiyo maana ubora wake haukuonekana katika mechi dhidi ya Augsburg ya Ujerumani, ambao walichapwa mabao 2-1.

"Nafikiri wachezaji walicheza vizuri mechi iliyopita, lakini baadhi hawakufanya vizuri kwa sababu hawajacheza muda mrefu, mfano Dube, hakuwa uwanjani kwa zaidi ya miezi sita, Baleke alikuwa na afadhali kidogo, lakini wengine wanaonekana wako fiti, ila bado baadhi wanatakiwa wazoeane na wenzao, kujua wenzake wanapasiwa vipi mpira, na yeye mwenyewe mchezaji anatakiwa awe wapi ili apokee pasi kutoka kwa wenzake.

"Kiujumla kuna baadhi ya  wachezaji wanatakiwa wazoeane na wenzao ili kujua wachezeje, ila kwa ujumla kila kitu kinakwenda sawa," alisema Gamondi.

Mara ya mwisho Dube kuonekana uwanjani akicheza mechi ya ushindani ilikuwa ni Februari 9, mwaka huu, wakati timu yake ya Azam ikicheza dhidi ya Simba katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, timu hizo zikitoka sare ya bao 1-1, Mzimbabwe huyo akipachika bao dakika 14, kabla ya kusawazishwa na Mzambia, Clatous Chama dakika ya 90, na wote hao wamesajiliwa na Yanga kuelekea msimu ujao wa mashindano.

Baada ya hapo hakuonekana tena kutokana na kile kilichodaiwa kuwapo na mgogoro wa kimkataba baina yake na Klabu ya Azam ambao ulimalizika hivi karibuni akitakiwa kuilipa timu yake ya zamani kiasi cha Sh. milioni 500 ili awe huru na hilo lilifanyika kabla ya kutimkia Jangwani.

Kwa upande wa Baleke, baada ya kuachwa na Simba kipindi cha dirisha dogo Januari mwaka huu alitimkia Al Ittihad ya Libya na sasa ameonekana akiwa na kikosi cha Yanga na kufunga bao la kufutia machozi kwenye mechi ya Jumamosi dhidi ya Augsburg, ingawa hajatambulishwa rasmi.

Akizungumza mechi ya leo alisema atahakikisha kila mchezaji anapata fursa ya kuonyesha uwezo wake kwa sababu hakuna idadi maalum ya kuingiza wachezaji wa akiba.

"Nitampa nafasi kila mchezaji kucheza angalau kwa dakika 15 ili kuonyesha uwezo walionao na kuwafanya wawe na utimamu wa mwili, tunakwenda hivyo hivyo taratibu, kidogo kidogo lakini kwa uhakika," alisema kocha huyo raia wa Argentina.

Baada ya mechi hiyo, Yanga itakamilisha mechi zake Jumapili, ambapo inatarajiwa kucheza mchezo wa Kombe la Toyota, dhidi ya Kaizer Chief ya nchini humo itakayopigwa Uwanja wa Bloemfontein.