Gamondi apata dawa wanaopaki ‘bus' Bara

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:50 AM Nov 08 2024
KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi
Picha:Mtandao
KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema timu nyingi za Ligi Kuu Tanzania Bara zimekuwa na utamaduni wa 'kupaki basi' kila wanapocheza nazo na kuiweka timu yake katika nafasi ngumu ya kufunga idadi kubwa ya mabao.

Akizungumza na gazeti hili kabla ya kushuka dimbani kuivaa Tabora United jana jioni, Gamondi alisema mafanikio waliyopata katika misimu miwili iliyopita yamewafanya wapinzani wacheze kwa tahadhari na yeye tayari amejifunza 'kitu' na amepata dawa ya tatizo hilo.

Gamondi alisema bila kuficha Yanga ndiyo timu bora kwa sasa hapa Tanzania, hivyo timu nyingine zimekuwa zikicheza kwa tahadhari wanapokutana ili kujiepusha na kufungwa mabao mengi.

Alisema timu nyingi zimekuwa zikicheza mfumo wa kuweka idadi kubwa ya wachezaji nyuma kwa sababu zinajua kama zitafunguka, zinaweza kujikuta zinapokea dozi kubwa kama walivyofanya katika mechi nyingi msimu uliomalizika.

"Yanga ndiyo timu bora kwa sasa nchini, ndiyo maana kila timu ikija kucheza na sisi inakuja kwa tahadhari. Zinajua zikicheza na sisi kwa kupishana zitafungwa idadi kubwa ya mabao. Ni kazi sana kuzifungua timu kama hizi, kupiga krosi na kutafuta nafasi kwa ajili ya kufunga," Gamondi alisema.

Aliongeza hii ndiyo sababu inayofanya msimu huu wasiwe na idadi kubwa ya mabao, lakini ameahidi kuendelea kulifanyia kazi ili kurejea walipopazoea.

"Vitu vinavyotokea kwa sasa, tunapata mambo ya kujifunza, siku zote changamoto inakufanya ujue ufanye nini ili utatue tatizo, tunatakiwa turekebishe hili. Kinachobaki kila kitu ni upande wetu, tufanye nini kuwafungua wapinzani kwa kila staili tunayoweza hadi kushinda michezo yetu," alisema kocha huyo.

Aliongeza sababu nyingine inayowafanya  wachezaji wake waonekane wamepungua viwango ni idadi kubwa ya mechi wanazocheza ndani ya muda mfupi.

"Kucheza michezo mingi kwa muda mfupi pia kunasababisha wachezaji wangu kushindwa kuonyesha viwango vyao vilivyozoeleka kwa mashabiki. Tunacheza mechi kila baada ya siku tatu, na hii sisemi kwa wachezaji wangu tu, hata kwa timu nyingine wakati mwingine tunakwenda kucheza mchezo bila maandalizi baada ya kucheza uliopita," alifafanua.

Ingawa Yanga haijapata ushindi wa idadi kubwa ya mabao kama ilivyokuwa msimu uliopita, ukiacha ule wa mabao 4-0 dhidi ya Pamba Jiji, lakini timu hiyo imeweka rekodi ya kucheza michezo nane bila kupoteza.

Mabingwa hao watetezi waliruhusu rekodi yao kutibuliwa Jumamosi iliyopita walipofungwa bao 1-0 dhidi ya Azam FC.

Msimu uliopita ambao Yanga ilikuwa ikifunga mabao mengi, ilipoteza mchezo katika mechi ya nne tu baada ya kuanza kwa ligi ambapo Oktoba 4, mwaka jana ikiwa Mbarali, Mbeya nyumbani kwa Ihefu FC ililala mabao 2-1.