Gamondi alalamikia uwanja, JKT kicheko

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 06:47 PM Apr 25 2024
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi.
Picha: Mtandao.
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi.

BAADA ya kulazimishwa suluhu na JKT Tanzania katika mechi ya Ligi Kuu Bara, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema sababu iliyowanyima ushindi katika mchezo huo ni hali mbaya ya Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo iliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha Dar es Salaam.

Mechi hiyo ilichezwa kwenye uwanja uliojaa maji na matope hasa katika eneo la katikati na kusababisha mpira kushindwa kudunda, awali mchezo huo ulipangwa kufanyika Jumanne.

Akizungumza na gazeti hili jijini jana, Gamondi ambaye timu yake ilipunguzwa kasi katika mbio za ubingwa alisema hali ya uwanja  haikuwa rafiki na haukupaswa kutumika kwa mechi hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Gamondi alisema timu yake haiwezi kucheza vyema katika uwanja wa aina ile na hawezi kutoa tathmini ya mechi namna ilivyokuwa.

"Huwezi kucheza vyema kwenye uwanja wa aina hii, huwezi kucheza mpira wa mfumo na kiufundi namna hii, nataka kujua kwa nini tulihitajika katika uwanja huu?" alihoji Gamondi.

Kocha huyo, ambaye ni raia wa Argentina, alisema alivyoona wachezaji wa JKT Tanzania walikuwa wazuri zaidi kucheza kwenye matope kuliko wachezaji wake ambao ndio vinara wa ligi hiyo.

"Siwezi kuzungumza tumechezaje na madhaifu yaliyoonekana wakati wachezaji wangu walikuwa ndani ya uwanja wenye hali kama hii, wao JKT Tanzania nimeona ni wazuri kucheza katika hali hii, nadhani ndiyo maana wametulazimisha kucheza hapa. Siwezi kutoa tathmini, si unaona wanafuraha sana, naona watu wengi wamefurahi kwa sababu tumetoa sare kutokana na hali mbaya ya uwanja," alilalamika kocha huyo.

Hata hivyo, baadaye Gamondi alisema wapinzani wao walitengeneza nafasi mbalimbali katika kipindi cha kwanza ambazo hawakuzitumia vyema, lakini kipindi cha pili wachezaji wake wakalazimika kuzoea changamoto ya uwanja.

"Na mimi pia nashukuru kwa kupata pointi moja kwa sababu tumecheza katika mazingira magumu ya uwanja na hali ya hewa pia," kocha huyo wa zamani wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, alisema.

Naye Kocha Msaidizi wa JKT Tanzania, George Mketo, alisema waliwasoma vyema Yanga katika michezo yao mitatu iliyopita na kuandaa mpango mkakati, ikiwamo kumfanya kiungo mshambuliaji, Stephane Azi Ki, asiwe huru na mpira kutokana na kupenda kupiga mashuti ya mbali.

"Tuliwasoma Yanga zaidi ya michezo mitatu nyuma, tulijua ina wachezaji wenye nguvu, na wanategemea sana kupitisha pembeni mashambulizi yao, na mtu mwingine ambaye ni hatari tuliyemwekea mikakati ni Aziz Ki, anashuka chini kuchukua mpira ili kutengeneza nafasi za kupiga mashuti, tukaweka mabeki watatu kati ili yeye na wenzake wasiweze kupata nafasi ya kupiga, na hilo tumefanikiwa," alisema Mketo.

Kocha huyo aliwapongeza wachezaji wake akisema walicheza ndani ya mpango waliupanga katika uwanja wa mazoezi yaliyochukua wiki mbili.

Matokeo ya mchezo huo yameifanya Yanga imeendelea kujiimarisha kileleni ikifikisha pointi 59, ikihitaji pointi 15 ili kutetea taji la ubingwa wanaloloshikilia.

Endapo Simba itashinda mechi zake tisa zilizosalia itafikisha pointi 73 huku Azam iliyoko nafasi ya pili kwenye msimamo, imebakisha michezo sita, ikifanikiwa kushinda, itafikisha pointi 72.