Chad kufanya uchaguzi kuhitimisha utawala wa kijeshi leo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:19 AM May 06 2024
Wanajeshi wakiwa katika eneo la kupigia kura.
PICHA: MAKTABA
Wanajeshi wakiwa katika eneo la kupigia kura.

CHAD inafanya uchaguzi wa rais leo Jumatatu baada ya miaka mitatu ya utawala wa kijeshi. Uchaguzi huo ni wa kwanza kwenye kanda ya Sahel tangu eneo hilo liliposhuhudia wimbi kubwa la mapinduzi ya kijeshi.

Nchi hiyo inafanya uchaguzi kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitatu ya utawala wa kijeshi, ikitazamiwa kuwa nchi ya kwanza barani Afrika inayoongozwa na jeshi kuhamia kwenye utawala wa kidemokrasia kwa kura za wananchi.

Chad itamaliza kipindi cha mpito cha miaka mitatu kilichowekwa, baada ya kifo cha ghafla cha kiongozi wa muda mrefu, Idriss Deby Itno alipokuwa akipambana na waasi.

Jenerali Mahamat Déby ambaye ni mtoto wa kiongozi huyo, ni mmoja mwa watu wanaopendekezwa kushinda kiti hicho cha urais katika uchaguzi unaofanyika leo Mei 6, 2024.

Waziri Mkuu Succès Masra ni miongoni mwa wapinzani wake tisa, na anaonekana kuwa mpinzani wake mkubwa katika kinyang’anyiro hicho.

Wanasiasa wengine kumi ambao walikuwa na matumaini ya kugombea, wakiwemo watu wawili mashuhuri, Nassour Ibrahim Neguy Koursami na Rakhis Ahmat Saleh, walitengwa na baraza la katiba kwa sababu ya "ukiukaji taratibu".

Koursami aliyeshtakiwa kwa ulaghai, lakini wengine wamedai kuwa uamuzi wa kuwazuia watu fulani ulichochewa kisiasa.

Wanaharakati wametoa wito wa kususia uchaguzi huo, ambao waliutaja kuwa njama ya kutoa mwanga wa uhalali wa kidemokrasia kwa familia ya Deby.

Watu wengi bado wako uhamishoni wakisakwa vikali baada ya kufanya maandamano ya upinzani Oktoba 2022.

DW