Fadlu aiona Simba tofauti kwa Mkapa

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:12 AM Sep 17 2024
KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids
Picha;Simba SC
KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema anaamini mashabiki wa timu hiyo watakuwa sehemu kubwa ya ushindi katika mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza, Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya utakaochezwa Jumapili ijayo, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam huku akiamini itakuwa mechi tofauti kabisa na hiyo waliyocheza nchini Libya.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo wa mkondo wa kwanza juzi, Uwanja wa Juni 11, jijini Tripoli, Libya, Fadlu alisema umati wa mashabiki 45,000 uliokuwa ukihanikiza uwanjani hapo kwa kiasi fulani uliwaathiri wachezaji wake, lakini anaamini kuwa hata wao watapata faida hiyo watakaposhangiliwa na mashabiki kiasi cha 60,000, Uwanja wa Benjamin Mkapa, akisema hali inaweza kuwa zaidi na tofauti kabisa ya hicho walichokipata wao.

"Tunakwenda kuifanyia kazi mechi ya marudiano kwa kuendelea kuwasoma, leo wameweka baadhi ya wachezaji wapya ambao hatujawahi kuwaona na kuwafanyia kazi, lakini pia mashabiki wao na jinsi wanavyoshangilia ilitupa shida kidogo, ila najua nyumbani mashabiki wa Simba wanaweza kufanya zaidi yao katika mchezo ujao.

"Nawafahamu mashabiki wa Simba, wanaipenda timu yao na mara nyingi wapo nyuma ya wachezaji wao, najua watakuja wengi zaidi ya hawa, watawashangilia wachezaji wao, watawatoa mchezoni wapinzani zaidi ya walivyokuwa wanafanya hawa wa Al Ahli Tripoli, na matokeo yake tutapata matokeo mazuri," alisema kocha huyo raia wa Afrika Kusini.

Simba ililazimisha suluhu ugenini, matokeo ambayo yanaiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kama itapata ushindi wa aina yoyote.

Akizungumzia mchezo huo, aliwapongeza wachezaji wake, akisema wameonesha uwezo mkubwa wa kucheza wakiwa hawana mpira.

"Tulikuwa na kiwango kizuri, hasa kwa mabeki wetu na hata viungo, tumeonesha kuwa tunaweza kupambana kwa pamoja, tumeonesha jinsi gani tunaweza kucheza tukiwa hatuna mpira.

"Tulikosa nafasi moja kipindi cha kwanza, unajua mechi hizi nafasi zinapatikana kwa nadra sana, hivyo ilibidi zitumiwe," alisema.

Baada ya mchezo huo kumalizika vurugu kubwa zilitokea, ambapo mashabiki wa timu hiyo ambao walionekana kutoamini timu yao kama imeshindwa kupata ushindi nyumbani, hali iliyowalazimu watu wa usalama kuwaondoa haraka wachezaji wa Simba uwanjani, huku kipa Aishi Manula akivamiwa na mmoja wa polisi aliyekuwa akiwalinda.

Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, alisema hali haikuwa shwari baada ya mchezo kumalizika kwani timu yao pamoja na waamuzi walifanyiwa vurugu.

"Baada ya mchezo kumalizika tulishauriwa na watu wa usalama kuwa tusitoke kule jukwaani tusubiri vurugu zipungue, wakati huo wachezaji wakaondoshwa uwanjani kwa pamoja kutoka katikati ya uwanja kwenda vyumbani huku wakirusha chupa.

Tulikaa vyumbani kama dakika 15 hivi, vurugu zikapungua, katika hali ya kushangaza, mtu ambaye alikuwa anatulinda ndiye aliyemvamia Manula tuliyekuwa tumekaa naye kule jukwaani na kumfanyia vurugu, lakini hajapata madhara yoyote.

"Tulikaa vyumbani na wachezaji kama dakika 40 kusubiri vurugu mitaani zipungue ndipo tulipoondoka," alisema Ahmed.

Alisema kufanya kwao fujo ni dalili za kukata tamaa kwani wanajua watapata shinda, Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mchezo wa marudiano.

"Aina ya usajili walioufanya na walichokipata uwanjani hawakukitarajia, ni sare ambayo tuliitolea machozi, jasho na damu. Hili limekwisha akili yetu ni mechi ya marudiano," alisema.