Bilioni 19 zatengwa kuukarabati Uhuru

By Saada Akida , Nipashe
Published at 07:17 AM Apr 26 2024
 Uwanja wa Uhuru.
Picha: Maktaba.
Uwanja wa Uhuru.

WIZARA ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imesaini mkataba na Kampuni ya Railway Construction Engineering Group (CRCEG) kutoka China wenye thamani ya Sh. bilioni 19.7 kwa ajili ya ukarabati wa ujenzi wa Uwanja wa Uhuru ulioko, Dar es Salaam.

Ukarabati wa uwanja huo maarufu Shamba la Bibi unatarajiwa kuchukua mwaka mmoja na utafanyika katika vyumba vya kubadilishia nguo, kuta za uwanja, ubao wa kuonyesha matokeo, mifumo ya sauti, sehemu ya kukimbia riadha, kuweka kamera za usalama na  eneo la kuchezea (pitch).

Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, alisema licha ya kumpa muda wa mwaka mmoja mkandarasi huyo, lakini wamemwomba ikiwezekana kukamilisha ukarabati huo ndani ya miezi sita.

Msigwa alisema anaamini ukarabati huo unaweza kukamilika mapema kwa sababu ya uhaba wa viwanja haoa nchini hasa Dar es Salaam ambayo itapata upungufu kutokana na Uwanja wa Azam Complex nao utafungwa kwa muda ili kufanyiwa maboresho.

"Sawa tumempa miezi 12, lakini tumemwomba ndani ya miezi sita uwe umakamilika kwa sababu ya uchache  wa viwanja hapa Tanzania, tumezungumza na mkandarasi tunahitaji uwanja kukamilka mapema, Azam Complex ukija kufungwa itakuwa tabu kwa ligi kuchezwa, hivyo tunauhitaji Uwanja wa Uhuru mapema,” alisema Msigwa.

Aliongeza uwanja huo ukitumika ipasavyo utasaidia kupunguza matumizi ya Uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini pia utatoa fursa kwa Tanzania mwenyeji wa kuandaa mashindano mbalimbali ya kimataifa.

“Tunauhakika na wakandarasi tuliowapa, kwa sababu tunawafahamu na tunaimani watafanya kitu kizuri, Uwanja wa Uhuru unaingiza watu 23,000, lakini tunahitaji kupandisha hadi 30,000.

Tutajadiliana na mkandarasi wa Uwanja wa Uhuru kuondoa sehemu ya kukimbilia riadha na kuongeza vitu ili kupanda daraja (kutoka daraja la tatu hadi daraja la pili) katika viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA),” alisema Msigwa.

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, alisema tukio la kusaini mkataba huo ni jambo kubwa kwa sababu Uwanja wa Uhuru, una historia na anaahidi kushirikana na serikali katika kupata viwanja vizuri kwa ajili ya kutumika katika mazoezi.

"Ukarabati wa Uhuru utakuwa na faida kubwa sana kwetu, kwa sababu baada ya AFCON, utatumika kwa ajili ya timu  kucheza michezo ya mbalimbali ikiwamo Ligi Kuu Tanzania Bara,” alisema Karia.

Ukarabati wa uwanja huo ni mwendelezo wa ujenzi wa viwanja kama sehemu ya maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), ambayo Tanzania, Kenya na Uganda watakuwa wenyeji.