NOVEMBA 19 kila mwaka hufanyika maadhimisho ya Siku ya Choo Duniani. Kaulimbiu yamwaka huu ilikuwa kuongeza kasi ya mabadiliko katika upatikanaji wa majisafi na usafi wa mazingira. Yote hiyo ni katika kutekeleza lengo la sita la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG).
Tanzania ikiwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa, iliungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku hiyo kwa lengo la kuhamasisha jamii kuwana vyoo bora pamoja na matumizi sahihi ya huduma ya choo. Siku hiyo huadhimishwa kwa ajili ya kuhamasisha na kutoa elimu ya afya hasa katika matumizi ya vyoo kwa usafi wa mazingira na afya kwa ujumla.
Matumizi sahihi ya vyoo ni jambo muhimu kwa ajili ya utunzaji wa mazingira ili kujikinga na maradhi mbalimbali yanayoweza kuzuilika. Wakati juzi siku hiyo ikiadhimishwa, inakadiriwa kuwa takriban watu bilioni 3.5 duniani wanaishi bila vyoo salama.
Kutokana na takwimu hizo, ni dhahiri kwamba nchi za Afrika ni miongoni mwa nchi zenye watu wanaoangukia katika kundi hilo, hivyo ni muhimu kuongeza kasi kuhakikisha matumizi sahihi ya vyoo bora yanahimizwa ili kuokoa jamii katika kukumbwa na maradhi ya mlipuko.
Katika kutambua umuhimu wa vyoo, miaka ya karibuni kumekuwa na kampeni mbalimbali ikiwamo ya ‘Nyumba ni Choo’ ambayo ilikuwa ikihamasisha kila kaya kuwa na choo bora. Kampeni hiyo ilienea mijini na vijijini na kufanikisha ujenzi wa vyoo vya kisasa na hatimaye kupunguza maradhi na vifo vitokanavyo na matumizi yasiyo sahihi ya vyoo hasa magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu, homa za matumbo, kuhara na kuhara damu.
Katika kampeni hiyo pia kulikuwa na amri kwamba mtu atakayekutwa akijisaidia ovyo ama njiani au vichakani, akamatwe na kutozwa faini au kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Wakati juzi Siku ya Choo Duniani ikiadhimishwa, nchini Tanzania ilielezwa kuwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii wamekuwa na mchango mkubwa wa utoaji wa elimu ya afya kuhusu umuhimu wa matumizi ya vyoo katika kuepuka na magonjwa ya mlipuko yanayosababisha kujisaidia ovyo vichakani.
Wahudumu hao wamekuwa wakitoa elimu ya afya katika ngazi ya jamii kuhusu matumizi ya vyoo wakishirikiana na maofisa afya, ikiwamo umuhimu wa kunawa mikono baada ya kutoka kujisaidia ili kuepukana na maradhi kama homa ya matumbo na kipindupindu. Elimu hiyo wanayoitoa imesaidia kwa kiasi kikubwa jamii kuwa na uelewa mpana kuhusu matumizi ya vyoo na kuimarisha afya zao. Kwa elimu hiyo, idadi ya wagonjwa na vifo vitokanavyo na magonjwa ya mlipuko vimepungua kwa kiwango kikubwa.
Katika kuonesha kuwa elimu hiyo imewafikia wengi na kuongeza uelewa, shuhuda zilitolewa na baadhi ya wananchi katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma kwamba ina umuhimu mkubwa kwa kila mmoja hasa kwa kuzingatia matumizi sahihi ya vyoo. Wananchi hao walisema kujisaidia vichakani kuna athari kubwa kwa binadamu ikiwamo kung'atwa na nyoka na wanyama wakali pamoja na athari ya kueneza magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.
Kuna msemo miongoni mwa jamii kwamba kupika chakula ni jambo moja lakini ili kiive mpishi anapaswa kuchochea mara kwa mara. Kwa mantiki hiyo, pamoja na elimu na uelewa wa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya vyoo, elimu zaidi haina budi kuendelea kutolewa.
Hiyo inatokana na ukweli kwamba katika baadhi ya maeneo, mijini na vijijini, bado kumekuwa na changamoto ya magonjwa ya mlipuko hasa nyakati za mvua jambo ambalo limekuwa likichangia matatizo ya afya na hata vifo. Kwa hiyo kasi ya elimu kuhusu matumizi ya vyoo inatakiwa kuongezwa ili kufanikisha lengo la usafi wa mazingira endelevu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED