JUMAPILI Desemba mosi, ndiyo Siku ya UKIMWI Duniani, zimesikika ripoti na kazi mbalimbali zikizungumzia hali ya maambukizi, mafanikio, changamoto bila kusahau ukweli kuwa mambo ni mabayá zaidi kwa waathirika wanawake na watoto.
Mkoani Mara Shirika la Haki Sawa kwa Wote, linalotetea ustawi wa wafanyakazi wa nyumbani, linasema wasichana watumishi wa ndani walioathirika na VVU wanapogundulika na waajiri wao baadhi wananyanyapaliwa na kuumizwa zaidi.
Mkurugenzi wa Haki Sawa, Angelina Nyamusika, akizungumzia harakati za siku 16 za kupinga ukatili, anasema wamejikita kwenye VVU, kuwasaidia mabinti wanaoishi na maradhi hayo.
Kwa kushirikiana na viongozi wa serikali, waajiri na asasi za kiraia wanawahamasisha wafanyakazi hao kupima VVU kujua hali zao, kujitibu na kuchukua tahadhari.
Anasema wanalenga kuwapunguzia kunyanyapaliwa endapo watagunduliwa kuwa wanaishi na VVU na pia kuwasaidia kufikia huduma za tiba kinga zinazogharamiwa na serikali.
“Tunataka watumishi wa ndani wenye VVU wajitambue, pia waajiri na wazazi au walezi wafahamu na kuwasaidia kupata huduma. Tunalenga kuongeza ustawi wa maisha yao na pia kupunguza maambukizi mapya.” Anasema Angelina.
“Kwa kuanza tulilenga kuwafikia wasichana watumishi wa majumbani 25 hapa wilayani Musoma, baada ya kuomba kibali cha halmashauri tukishirikiana na viongozi wa serikali za mitaa tukawatembelea na kuanza utekelezaji.
Aidha, tukawaelimisha waajiri na kuwashawishi wasichana hao kukubali kuchunguzwa afya na kati yao 10 walikubali na wengine 15 hawakuwa tayari.
Anaeleza kuwa wamewashirikisha wazazi, walezi pamoja na waajiri wa wasichana hao kabla ya kuwapima na kwamba sheria inaelekeza kuwa endapo binti hajafikia miaka 18 ni lazima mzazi au mlezi atoe ridhaa ya kumpima mtoto VVU.
Anasema kazi ya kupinga ukatili dhidi ya watumishi wa ndani wanaoishi na VVU imefanyika maeneo ya Mlimani, Mshikamano na Nyakato katika Halmashauri ya Musoma.
“Kuwapima na kuwatambua na kuhamasisha mitandao mingine kufanya hivyo kunalenga iwe chachu ya kupunguza unyanyapaa mitaani na nyumbani kwa hiyo tunachotaka ni heshima na kuwathamini wenzetu.
Umma utambue kuwa kuishi na VVU hakuondoi haki ya kulipwa mshahara kisheria, kufanyakazi na kupata riziki yako na kwamba hata kama ni MVIU bado ni binadamu na unastahili haki sawa,” anasema Angelina.
Anaongeza kuwa wapo baadhi ya waajiri au jamaa zao wanaowabaka watumishi wa ndani na kuwaambukiza VVU, lakini wakigundulika wana maambukizo wasichana hao hunyanyapaliwa, kadhalika wanafukuzwa na pengine hata bila kuwalipa mishahara.
Pia, kuna wale wanaokataa kuwalipa watumishi wa ndani Shilingi 60,000 kwa mwezi ambacho ni kiwango cha mishahara yao kisheria. Tena kuna wengine waolimbikiza mishahara hiyo na kesi kama hizo zinakuja kwenye ofisi za Haki Sawa kwa Wote.
Anasema wamewajengea uwezo wa kukabiliana na unyanyapaa. Wanataka kuweka tabasamu kwenye nyuso za wasichana hao hata kama wanaoishi na VVU wajue kuwa wana haki, wanawajali na wasijinyanyapae.
Godwin Charles ni Mratibu wa Haki Sawa kwa Wote mkoani Mara, akizungumzia jitihada hizo, anasema shirika hilo lenye wanachama zaidi ya 61, wanatetea haki za watumishi hao kupunguza unyanyapaa na ukatili dhidi ya Wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI (WAVIU).
Anaeleza kuwa walipokuwa wanafanya kampeni za kuwachunguza afya, waliwashirikisha wazazi na walezi wa mabinti, waajiri na wao wenyewe, lakini idadi kubwa haikuonyesha ushirikiano.
Anasema baadhi ya walezi na wazazi walikataa wasichana kuchunguzwa wakisema waachwe na hivyo hawakuwapima.
Anaeleza kuwa lengo ni pale wanapowagundua kuwa ni WAVIU wataalamu wawape ushauri, kisha waajiri, wazazi au walezi wafahamu kuhusu hali zao na kuwashauri wasiwanyanyapae na hata WAVIU wasijinyanyapae.
“Tunawafundisha njia za kuwa salama zaidi, hasa kwenda hospitalini, kujiandikisha na kuanza kutumia tiba kinga au ARV mara moja,” anasema Charles.
Wanalolenga ni kuwaelimisha ili wajifahamu na kujikubali watumie tiba kinga na kujiepusha na kuwaambukiza wengine na kuongezewe virusi zaidi.
Charles anasema wakifahamu kuhusu hali zao kuwa wanaishi na maambukizi ya VVU watatumia tiba na pia waajiri watatengeneza utaratibu bora zaidi wa kuwahudumia na kuwawezesha kufanya majukumu yao au maamuzi mengine lakini yanayoheshimu na kuzingatia haki za binadamu.
Anakumbusha kuwa dunia ya leo mtu anaweza kupata chochote anachotaka bila kujali hali yoyote aliyo nayo hata kama anaishi na VVU.
Aidha, nawahimiza wanaoishi bila VVU kuwaheshimu na kuwathamini WAVIU kwa kuwa kila binadamu anastahili kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wake na kupata haki sawa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED