RIPOTI YA UCHUNGUZI -4: Mapendekezo ya TANAPA yakwama, mwekezaji arejesha mzigo kwa serikali

By Sanula Athanas , Nipashe
Published at 06:32 PM Nov 08 2024
Sehemu ya nyumba kwa ajili ya malazi ya wafanyakazi wa mashamba ya
miwa na kiwanda cha Kampuni ya BSL wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.
Picha:Mpigapicha Wetu
Sehemu ya nyumba kwa ajili ya malazi ya wafanyakazi wa mashamba ya miwa na kiwanda cha Kampuni ya BSL wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.

MWEKEZAJI aliyemegewa eneo katika Mbuga ya Wanyama Saadani, ameingia makubaliano mapya na serikali. Badala ya kusalimisha mita 500 kutoka ukingo wa Mto Wami, sasa atasalimisha mita 200.

Awali kulikuwa na pendekezo la kitaalamu toka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) likitaka mwekezaji kusalimisha eneo la mita 500 kutoka ukingo wa Mto Wami ili kulinda ikolojia ya mbuga hiyo.

Katika hatua ya sasa, mwekezaji ameshikilia kusalimisha mita 200 tu kutoka ukingo wa Mto Wami na kwamba serikali ndiyo isalimishe mita 300 ili kukamilisha mita 500 zilizopendekezwa.

Kwa upande wake, serikali ilijenga hoja ya usalama na uhai wa ikolojia; kwa upande wa mwekezaji – Bagamoyo Sugar Limited (BSL) – hoja ilikuwa miwa ambayo tayari imestawishwa.

Katika vutanikuvute hii, miwa ilishinda usalama na uhai wa ikolojia. Hivyo, upande wa serikali ndio utarudi nyuma mita 300 na mwekezaji atarudi nyuma mita 200. Hayo ndiyo makubaliano.

Mwekezaji anategemea Mto Wami kupata maji kwa ajili ya kilimo cha miwa. TANAPA inategemea mto huo kwa ustawi wa wanyamapori na usalama wa ikolojia.

Janeth Msema, Msomi wa Sayansi ya Usimamizi wa Mazingira, anaonya kwamba, kilimo cha miwa kinahusisha matumizi ya mbolea na dawa kwa ajili ya kuua wadudu wanaoshambulia miwa. 

Kwa hiyo, anasema mbolea na dawa hizo zinapoingia katika miili ya wanyamapori, zinakuwa na madhara kama vile kuharibu figo, ini, mfumo wa neva za fahamu, kubadili mfumo wa homoni kinga na hata kuwaua, hasa watoto wa wanyama hao ambao kinga zao hazijaimarika. 

Janeth – Mhitimu wa Shahada ya Sayansi ya Usimamizi wa Mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), ana hoja nyingine kwamba, uzalishaji sukari unahusisha mitambo inayotumia mafuta na oili; hivyo huzalisha taka hatarishi ambazo zisipodhibitiwa, husababisha madhara kwa mazingira na viumbe vilivyomo.

Katika hilo, mwanamazingira huyo anafafanua kuwa, mvua inaponyesha, kemikali hizo zinaingizwa katika vyanzo vya maji na kuathiri watumiaji wa maji hayo, wakiwamo wanyamapori. 

“Mnyama anapokula vitu vilivyo na, au vilivyoathirika kwa kemikali hizo; au kuzinywa katika maji, madhara yake ya moja kwa moja yanaanzia katika ini na figo. Hivi ni viungo vinavyochuja sumu mwilini. Baada ya hapo, madhara yanahamia katika mifumo ya neva za fahamu, kinga ya mwili na hata kupunguza uwezo wa wanyamapori kuzaliana.

“Kuishi kwa wanyama kunategemea kumbukumbu nzuri na hisia za kuzunguka katika mazingira yao. Uharibifu wowote katika neva zao za fahamu, kama matokeo ya uchafuzi wa mazingira kutokana na kemikali, unaweza kuwa hatari kwao. 
“Miwa ni mitamu. Tembo atatamani kula miwa kwa sababu ya utamu wake. Hapo unambadilisha tembo kifikra na hisia zake katika kula. Wanyamapori wanatakiwa wale majani au nyasi za asili; siyo miwa na vitu vingine vilivyo nje ya mfumo wao wa kiikolojia,” anasema. 

Janeth anaendelea kufafanua kuwa wanyama wakishakula mazao yaliyozalishwa kwa kemikali na mbolea, mfumo wao wa homoni kinga unabadilika.

“Wakiugua, hawatibiki kwa dawa za kutibu wanyamapori kwa sababu hizo kemikali zinaifanya miili yao kuwa sugu kwa dawa hizo,” anaonya.

Uwekezaji wa kilimo cha miwa na uzalishaji sukari, anafafanua Janeth, unasababisha kelele hifadhini toka kwa wafanyakazi na ngurumo za mitambo ya kiwanda. Anasema kelele hizo ni usumbufu kwa wanyamapori.

“Ukweli mpevu ni kwamba, makosa yamefanyika kwa kutoa rukhsa ya kiwanda na kilimo cha miwa hifadhini. Kila bidhaa inayozalishwa kiwandani hapo inaweza kuathiri mazingira jirani na wanyamapori,” anahitimisha Janeth, ambaye sasa anafanya kazi katika hoteli ya kitalii ya Monica kisiwani Unguja.

Hoja ya kelele inaungwa mkono na Sadick Omary, Mhitimu wa Shahada ya Sayansi ya Wanyamapori toka SUA na mtetezi wa dhati wa ikolojia ya mbuga za wanyama, anayesema:

“Kuna wanyama, mfano chui, hawapendi kukaa maeneo yenye kelele. Kukishakuwa na kelele hifadhini, ni usumbufu mkubwa kwao. Kama hawatohama kutoka hifadhi hiyo yenye kelele, basi kuzaliana kwao kutapungua.” 
Profesa wa Mifumo na Ikolojia, Idara ya Mifumo Ikolojia na Uhifadhi ya SUA, Pantaleo Munishi, anashauri serikali izuie kilimo cha miwa na uzalishaji huo wa sukari hifadhini.

“Huo uwekezaji uondolewe kabisa katika hifadhi… Tutasababisha uhabirifu. Tungeacha kabisa kufanya kilimo na shughuli nyingine za kibinadamu ndani ya maeneo ambayo ni hifadhi za taifa.

“Sheria ya Misitu ipo. Sheria ya Wanyamapori ipo. Sheria zinazohusiana na masuala ya hifadhi za taifa na uhifadhi zipo; na zote zinazuia shughuli za aina hii kufanyika hifadhini,” anasema.

Kinachoendelea Saadani kwa sasa, anasema Profesa Munishi, ni matokeo ya “watendaji wa serikali kutozingatia sheria za nchi katika utendaji wao wa kazi.

“Hawafuati sheria. Wanangoja mpaka imetokea watu wameingia hifadhini na kufanya shughuli za uharibifu, ndipo wanaanza kuja kusema aah hawa watu, eeeh...!

Anasema sheria zikifuatwa, zikazingatiwa, na kuhakikisha kuwa shughuli zote zinafanywa kwa kufuata sheria, ”…hicho kinachoshuhudiwa Saadani kwa sasa (kiwanda na kilimo hifadhini) kingezuiwa, tena mapema tu!”

Profesa Munishi anakumbusha kile anachoita   ‘precautionary principle’ (msingi wa tahadhari) – yaani kama hujui madhara ya jambo unalokusudia kulifanya, basi liache. Usilifanye!

“Kama kuna eneo tengefu ambalo limeshaingiliwa na shughuli za binadamu; hizo shughuli ziondolewe kwa sababu sheria ipo. Tufuate sheria tu. Huo ndio ushauri wangu.

“Kama hakuna uwezekano wa kuondoa shughuli hizo hifadhini, basi tutafute mbinu ambazo zinaweza kupunguza madhara, ili yasiwe tishio kubwa sana,” anashauri Profesa Munishi.

Kabla ya kuzungumza na wataalamu hao, mwandishi wa habari hizi alikwenda kujionea mradi wa kilimo cha miwa na uzalishaji sukari wa kampuni ya BSL.

Alitumia dakika 28 kwa gari aina ya Toyota Coaster kutoka mjini Bagamoyo hadi Makurunge Mkwajuni, njiapanda ya Saadani, kwa nauli ya Sh. 1,500.

Kutoka hapo, kulikuwa na safari nyingine kwa pikipiki, umbali wa Km 25 iliyochukua dakika 40 hadi kiwandani kwa nauli ya Sh. 8,000. Barabara yake ni ya vumbi.

Karibu na kiwanda kuna makazi yanayoitwa, Kijiji cha Kibuyu-Mimba. Hapa pamechangamka na kuna kijiwe (kituo) cha waendesha pikipiki (bodaboda). Baadhi ya wakazi wake ni wafanyakazi wa mashamba ya miwa na kiwanda cha sukari. 

Kabla ya kulifikia geti la ofisi za kiwanda hicho kutoka barabarani, kuna nyumba nane zilizojengwa kwa matofali ya saruji na kuezekwa kwa bati.

Kuna vibanda vingine vitano vilivyojengwa kwa bati kuanzia chini hadi juu. Wenyeji walisema hayo ni ”malazi” ya wafanyakazi wa mradi. Karibu na nyumba hizo, kuna vibanda vitatu ambavyo mwandishi alielezwa kuwa ni vya mamalishe.

Kimsingi, mazingira ya sasa ya hifadhini Saadani, hasa katika eneo hili, yanakinzana na sheria na kanuni za nchi; na Programu ya Utalii ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ya 2020-2030 inayohimiza nchi wanachama kuhakikisha kunakuwa na utalii endelevu na kuondosha vikwazo vya utalii na uhifadhi katika ukanda huo.

Tanzania ni mwanachama mwasisi wa SADC.