Raha ya barabara nzuri Dar inapogeuka karaha ya usafiri

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:33 AM Dec 24 2024
Vyombo vya usafirir
Picha: Mtandao
Vyombo vya usafirir

DAR ES SALAAM imejaa barabara nzuri karibu kila upande pia kuna mtandao mkubwa wa njia za mabasi ya mwendo wa haraka. Hakika inapendeza kutiririka na ‘motokaa’ ndani ya barabara za lami lakini kwenye uzuri hapakosi kasoro.

Uzuri huo wa barabara unakuwa kero kwa watumiaji kutokana na kila saa kukoswa koswa na ajali za kila mara hasa za bodaboda, bajaji kadhalika msongamano uliokithiri hasa jioni kwenye vituo vya mabasi.

Mojawapo ni Mbezi Magufuli kunakomfanya msafiri au mtumia barabara akereke na foleni zinazomsonga karibu kila wakati asubuhi, mchana na pia nyakati za sikukuu na hata mwisho wa juma.

Lakini pia upo utitiri wa vyombo vya moto kwa vile kila upande kipo chombo kinachomghasi kulia na kushoto, nyuma na mbele anasongwa na pikipiki, guta, baiskeli, lori, magari madogo, daladala, mabasi yaendayokasi ya masafa na malori.

Unafika kipindi kituo hasa Mbezi Lousi au kwa Magufuli nyakati za asubuhi huwezi kuingia wala kutokea.

Hali hii inamfanya mtumiaji asione uzuri wa maelezo kuwa Dar es Salaam ina mtandao kabambe wa barabara na pia inamkera asipende usafiri wake ambao ni kama gereza ndani ya barabara.

Mwaka jana 2023 Rais Samia Suluhu Hassan akiwahutubia maofisa wa Jeshi la Polisi anaahidi kuweka kamera za usalama kwenye barabara kuu kudhibiti na kupunguza uhalifu na ajali.

Ukweli unabaki kuwa ajali nyingi zinapatikana Dar es Salaam kwenye mtandao wa barabara bora na nyingi. Takwimu za Jeshi la Polisi za mwaka 2023 zinathibitisha hilo. 

Takwimu hizo za hali ya uhalifu na matukio ya usalama barabarani ya Januari hadi Desemba 2023 zilitokea ajali 1,733 zilizoua Watanzania 1,645 na kujeruhi 2689.

Kadhalika zinaonyesha kuwa mwaka 2022 kipindi kama hicho ziliripotiwa ajali 1,545 na kwamba lipo ongezeko. Kwenye bodaboda zilikuwa 431 na wakati 2023 zikiongezeka hadi 448.

Polisi wanasema kitaifa Ilala ni mkoa unaoongoza kiajali zikifikia 514,951, Kinondoni 259,707 na Temeke ajali 229,532 ziliripotiwa. Jeshi hilo linataja ubovu wa barabara na vyombo pamoja na makosa ya kibinadamu kuwa ni chombo.

Mwezi Septemba kila mwaka mambo ya usalama barabarani hupewa kipaumbele Jeshi la Polisi na wadau, wakikumbusha usalama wa maisha na mali za watumia barabara lengo ni kupunguza ajali, kuuelimisha umma juu ya matumizi salama ya barabara, vyombo madhubuti, kutumia leseni na kuwa na madereva wataaluma wanaoendesha kwa kujihami na kwa usalama.

Lakini mwaka huu unapoelekea ukingoni kero ya usafiri barabarani ya kuwa na makondakta, madereva na daladala chafu iko pale pale.

Ni kwa nadra kuwakuta madereva na makondakta wa daladala wakiwa nadhifu. Ni kero kwa abiria kukutana na kondakta mchafu kuanzia mavazi, viatu kinywa na hata mikono anayomkaribisha nayo mteja kwenye daladala ni michafu.

Mbona wiki ya usalama haisaidii kuhimiza usafi wa wahudumu wa kwenye daladala? Magari ni machafu kupindukia mengine yana viti vya vyuma na mbao sponji zimetoka, yanaendeshwa na dereva asiyechana nywele, asiyevaa kwa unadhifu aliyevalia nguo kadhaa zote zikiwa zimechakaa, ana fulana chafu ndani, suti imeraruka na wakati mwingine kiunoni amevaa mkanda wa kufungia  raba, katani au kipande cha zipu.

Makamanda mnasimama barabarani kagueni sare sisitizeni kuweka mabasi katika hali ya usafi. Pia vioo na madirisha ya daladala nyingine ni vibovu na ikinyesha mvua maji yanavujia ndani abiria wanalowana kwa vile dari ni bovu.

VURUGU BARABARANI

Wakati mwingine barabara zinatumiwa kienyeji kwa mfano wanaobeba mkaa wanafunga magunia kadhaa kwenye pikipiki hawaoni nyuma tena wanajaa barabara nzima bila woga.

Makamanda lazima barabara ziwe na mpangilio wasaidieni watumiaji  wajisikie salama. Jitihada za kuweka maeneo maalumu ya teksi, bajaji na pikipiki zimezifanya barabara kuwa na kitisho zaidi maana boda na bajaji zinaegeshwa kila mahali.

Wapo wanaojibanza kwenye kona kwa mfano makutano ya njia nne zinazokwenda Goba, Madale, Kimara na Matosa, kadhalika kila eneo linakuwa na pikipiki na bajaji ambazo huingia barabarani wakati mwingine kuzuia mabasi hasa daladala kuegeshwa.

Haipendezi kuona boda ziko kila mahala, zikiwakera watembea kwa miguu na wapanda magari. Mathalani abiria akifika Mbezi anakutana na makundi ya vijana wenye misuli na nguvu wakiwafukuza abiria ili kuwapa usafiri wa kwenda mikoani.

Kikosi cha Usalama Barabarani, hili limekaaje? Mbona watu hawa wanazidi kujikusanya Mbezi? Hili nalo halina tiba kama kuna ufumbuzi kwanini vijana kama hao wamejazana kituoni hata kukwamisha magari na abiria?

Boda na bajaji zimekuwa kero zinaingia barabarani bila mpangilio na kusababisha watu kugongwa kutokana na kuchanganyikiwa kushindwa kulipisha gari kubwa ama boda ambazo huranda barabara muda wote bila kujali kuwa hata magari mengine yapo.

Mwaka mpya unavyokaribia kuna haja ya kufanya juhudi zaidi ili kuwa na maeneo maalumu ya boda boda na bajaji kuzizuia zisijirundike vituoni na kukwamisha watu kutumia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kusubiri na kupanda daladala.

Licha ya viongozi kuzungumzia mara kwa mara kuhusu malalamiko ya kuwapo trafiki barabarani na kuahidi kuwa wataweka kamera za kurekodi matukio bado walinzi wa usalama wanazidi kulalamikiwa kuwa wanafanya yanayowafaidisha zaidi na kuwaumiza wasafirishaji.

Kuna madai kuwa kinachotafutwa ni ‘chochote’ wasimamizi hao wanawatoa upepo madereva na kuna madai kuwa wanaelekezwa maeneo maalumu kuweka kitu kidogo vikiwamo vibanda vya mawakala simu. Mambo hayo yanawafanya kudharaulika kuwa lengo siku kuwa na usalama bali ni kuapata ‘kitu kidogo’.

Ikumbukwe usalama wa barabara ukiegemea zaidi eneo hilo ni kama taifa linaambiwa liendelee kuvumilia ajali zaidi, majeruhi watazidi kuongezeka, walemavu na vifo zaidi vya barabarani pamoja na uharibifu wa miundombinu.

Ni kwa sababu magari mabovu yanajaa barabarani, madereva wasiojali wanaendesha, pikipiki zinavunja sheria alimradi kila mtu anafanya apendavyo.