Mtaji mpya wa maendeleo; uwekezaji darasani, vyuo ufundi, mavuno mara tu baada kuhitimu

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 09:21 AM Sep 13 2024

Shughuli za ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam, ilipoendelea katika tawi lake la Mwanza, ikiwa ni sehemu ya mradi huo wa Benki ya Dunia na serikali.
PICHA: MTANDAO
Shughuli za ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam, ilipoendelea katika tawi lake la Mwanza, ikiwa ni sehemu ya mradi huo wa Benki ya Dunia na serikali.

MARA zote hatua za kimaendeleo ambazo daima huakisiwa katika mustakabali wa uchumi, suala la uwekezaji katika taaluma hupewa msingi mkubwa na kadri unavyokuwa mkubwa, matokeo yanashuhudiwa katika maendeleo ya nchi.

Hiyo inashuhudiwa hata nchini, tangu siku ya kwanza kupatikana uhuru mwaka 1961, hadi sasa, uwezekaji katika elimu kwa ngazi zote, umekuwa na nafasi ya kipekee na endelevu.

Ni hatua inayochukua nafasi kuanzia chini hadi kileleni, kwa maana ngazi ya kujua kusoma na kuandika hadi elimu ya shahada ya falsafa. Hiyo inaendana na shughuli mbalimbali za kitafiti.

Matokeo yake kwa jumla, yamekuwa yakirejewa katika maisha ya kijamii ya kila siku, iwe tiba, biashara, mawasiliano na kila nyanja inayotumiwa na wakazi hao, ikijumuishwa na kinachoendelea duniani.

Katika karne ya 21, Maendeleo ya Teknolojia, Utafiti na Elimu ni nguzo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa mataifa. 

KINACHOJIRI NCHINI

Inaelezwa, kabla ya uwekezaji wa vituo vya umahiri nchini, sekta ya elimu ilikabiliwa na changamoto kubwa, kama inavyooneshwa katika Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Elimu ya Mwaka 2018, asilimia 40 ya shule nchini zilikuwa na miundombinu duni.

Hiyo ikaendana na kutokuwapo vifaa vya kisasa, ulioathiri zaidi ya asilimia 60 ya shule na kusababisha kuwapo elimu duni nchini, huku asilimia 25 ya wanafunzi wana matatizo ya kuelewa kwa undani masomo yao kutokana na ukosefu wa vifaa vya kisasa.

Kwenye sekta ya ajira hali ilikuwa mbaya, Ripoti ya Benki ya Dunia (2017), ikibainisha asilimia 70 ya vijana walikabiliwa na changamoto ya ajira za kitaaluma zinazohitaji ujuzi maalum.

Utafiti uliofanywa na Tume ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTEVET) (2020) ulibainisha kwamba asilimia 50 ya wahitimu walikuwa na ujuzi mdogo wa vitendo, ikasababisha ugumu wa kupata ajira. Upungufu huo ulitokana na ukosefu wa mafunzo ya vitendo na uwekezaji mdogo katika sekta za viwanda na teknolojia.

Baada ya muda inatwa hata hivyo, uwekezaji katika vituo vya umahiri nchini, umepata hatua mpya ya maendeleo, kuibuliwa nguzo kama vile Kituo cha Mafunzo ya TEHAMA (RAFIC) cha Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT).

Kwingine kunahusu Kituo cha Mafunzo ya Taaluma za Anga na Operesheni za Usafirishaji (CoEATO) cha Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Kituo cha Mafunzo na Utafiti wa Nishati Jadidifu (KIKULETWA) cha Chuo cha Ufundi Arusha.

Aidha, kunatajwa Kituo cha Umahiri cha Uchakataji Ngozi (CELPAT) cha Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Mwanza.

Ripoti ya Benki ya Dunia ya Mwaka 2022  na utafiti uliofanywa na Tume ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTEVET), uwekezaji katika vituo vya umahiri unatarajiwa kuboresha ujuzi wa wahitimu kwa kiasi kikubwa.

Kuna Mradi wa Kujenga Ujuzi na Ushirikiano Afrika Mashariki (EASTRIP) kwa nchi za Tanzania, Ethiopia na Kenya ulioanza mwaka 2019, na ukileta mabadiliko makubwa kupitia uanzishwaji wa vituo vinne vya umahiri nchini.

EASTRIP inatekelezwa na serikali za Kenya, Ethiopia na Tanzania katika vituo 16 vya umahiri kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kuanzia mwaka 2019 na unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.

Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, ambaye ni Mratibu wa Mradi huo, Fredrick Salukele, anasema vituo hivyo vya umahiri vimejengwa kupitia Mradi wa Kujenga Ujuzi kwa Maendeleo na Uingiliano wa Kikanda, Afrika Mashariki (EASTRIP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia. Ulianza mwaka 2019 na hadi  2024, ilishagharimu, zaidi ya shilingi  bilioni 172.

Akizungumza katika mjadala wa utekelezaji wa mradi huo katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dar es Salaam, Salukele anasema, malengo ya mradi yanajumuisha kuongeza upatikanaji na uboreshaji programu katika Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi vya Kikanda (TVET).

Anasema, mradi huo umesaidia kutoa elimu bora  na ujuzi wa kitaaluma katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), walikojenga Kituo cha Mafunzo na Utafiti wa Nishati Jadidifu, eneo la Kikuletwa wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro.

Anasema ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 90, kukitarajiwa kukuza matumizi ya nishati jadidifu, ikiwamo safi ya kupikia, ambayo kwa sasa inapiganiwa kutumika nchini, kukabili mabadiliko ya tabianchi yanayochangiwa na shughuli za kibinadamu kama kutumia mkaa na kuni.

Salukele anasema, kituo hicho kutapunguza utegemezi wa vyanzo vya nishati nyinginezo, ambazo sio rafiki kwa mazingira na mbadala wake ukitumika.

Anataja nafasi ya Kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya TEHAMA (RAFIC) chuoni DIT, Dar es Salaam, kitasaidia kuboresha viwango vya mafunzo katika sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano, kwa  kutumia mbinu za kisasa, darasani na nje ya darasa.

Anataja maeneo, yanajumuisha wahitimu wenye ujuzi wa wanaoweza kukabiliana na changamoto za kidigitali, pia wakiimarisha uwezo wa vijana nchini, ambao kwa sasa una umuhimu mkubwa katika uchumi wa kidijitali.

“Kupitia mafunzo hayo, vijana watakuwa na ujuzi wa kubuni na kuendeleza teknolojia mpya ambazo zitawasaidia kuanzisha biashara za kiteknolojia, kuzalisha ajira na kuongeza ushindani katika soko la ajira, pia itachangia kuimarisha uchumi wa nchi kwa kuongeza tija na ufanisi katika sekta za teknolojia na mawasiliano,” anasema Salukele.

 

Anaendelea: “Kituo hiki kitachangia kuboresha miundombinu ya teknolojia nchini kwa kutoa wataalamu  wenye ujuzi wa kisasa ambao wataweza kuchangia katika miradi mikubwa ya kitaifa na kimataifa, kuimarisha matumizi ya teknolojia na kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi na kijamii,” anasema.

Kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya Taaluma za Anga na Operesheni za Usafirishaji (CoEATO), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Salukele anasema, kitasaidia kuimarisha sekta ya usafiri wa anga na ardhi kwa kutoa mafunzo ya kina kwa wahandisi wa ndege, wataalamu wa usafiri wa anga, na maofisa wa usalama wa usafiri.

Anasema kituo hicho kitakuwa msaada wa kuboresha usalama wa anga na ufanisi wa huduma za usafiri, hivyo kuongeza usalama na uaminifu wa miundombinu ya usafiri nchini, vijana watakuwa na ujuzi wa 

kupitia mafunzo haya, anaeleza vijana watakuwa na ujuzi wa kitaaluma wa hali ya juu katika sekta ya anga na usafiri, itasaidia kupunguza tatizo la ajira na kuongeza tija katika sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.

 KUTOKA MWANZA

Akizungumzia Kituo cha Umahiri cha Uchakataji Ngozi (CELPAT) kwa DIT, Kampasi ya Mwanza, Augustine Mbitila, anasema wameanzisha programu zinazoendana na mahitaji ya soko, akidokeza kuwa kati ya mitaala 15 waliokubaliana kuanzisha, kwa sasa wanatumia nane, zote zikionyesha matokeo mazuri, baada ya wanafunzi kumaliza na kupata ajira.

Anasema, kwa hatua zaidi, chuo chake kinafuatilia maendeleo ya kila mwanafunzi mhitimu kujua ujuzi wake na namna ya kumsaidia, apate ajira au kuajiriwa, jukumu ambalo ni la miezi tangu kumaliza masomo.

Salukele anasema, mwaka jana waliwatembelea  wahitimu 52 katika maeneo mbalimbali nchini kukagua wanachokifanya, kutokana na ujuzi wa masomoni.

Mwongozo wa mradi huo, ni kila mwaka wanawafikiwa wahitimu 25, lakini anasema wao walivuka lengo ikiwamo namna ya kuwasaidia kukabiliana na soko la ajira.

KIWANDA CHA CHUO

“Chuo chetu kina viwanda viwili vyenye miundombinu na teknolojia ya kisasa, ambayo hutumika kuchakata ngozi na kuzalisha bidhaa kama vile, mabegi, mipira, majaketi, viatu na  mikoba,” anasema Mbitila.

Anasema mwanafunzi anashiriki mafunzo kwa vitendo na chuo kimeingia makubaliano na viwanda vinavyotengeneza bidhaa za ngozi, wakivitembelea kujifunza zaidi teknolojia mpya na wanatembelea vingine nje ya nchi, ikiwamo Kenya na Ethiopia.

Anafafanua mikakati hiyo inawasaidia wahitimu kubobea na kuwa wajuzi kwenye sekta za uchakataji ngozi, usindikaji na utengenezaji bidhaa zinazotokana na ngozi kama vile mipira, viatu, mabegi na mikanda.

Mbitila anasema, kuna tija inayoonekana, kwa sababu wanapokea wanafunzi wa kigeni, wanaofika kujifunza teknolojia mpya za kuchataka ngozi  na kuongeza tija na ubora wa bidhaa.

“Tunatoa mafunzo kuhusu mbinu za kisasa za uchakataji na utengenezaji wa bidhaa. Hatua hii imeongeza ushindani kwenye soko la kimataifa ukilinganisha na ilivyokuwa awali ambapo kiwanda cha ngozi mkoani Mwanza kilikufa,” anasema Agustine.

Mkuu wa Kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya Taaluma za Anga na Operesheni za Usafirishaji (CoEATO) cha NIT, Dk. Chacha Ryoba, anasema mradi huo umeleta vifaa na mitambo mipya ya kisasa ya kufundishia na kujifunzia, inayochangia kuboresha miundombinu ya usafiri nchini.

 Anataja, hatua hiyo inafanikishwa kwa kupatikana wataalamu wenye ujuzi na watakaosaidia katika miradi mikubwa ya miundombinu ya usafiri, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanja vya ndege, miundombinu ya usafiri wa ardhini, majini na reli.

Dk. Ryoba pia anasema, vijana wahitimu wa chuo hicho wameajiriwa katika maeneo tofauti, ikiwamo Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), mashirika binafsi ya ndege na Treni ya Kisasa ya Mwendokasi (SGR).

Anaongeza kuwa kupitia utafiti na mafunzo, NIT inasaidia kuendeleza teknolojia mpya katika sekta ya nishati, ambayo inaweza kubadilisha sekta hiyo nchini, kutoa fursa za uwekezaji, na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na ubora wa maisha kwa wananchi.

Dk. Ryoba anasisitiza kwamba, kuanzishwa vituo hivyo vya umahiri, kutachochea ukuaji uchumi, kwa sababu kila  kituo kinachangia kutatua changamoto za jamii na kuchochea maendeleo ya taifa.

Anaeleza, uboreshaji miundombinu, ikiwamo ujenzi wa madarasa na hosteli kwa ajili ya malazi ya wanafunzi, utaongeza uwezo wa vyuo vya umahiri kupokea wanafunzi zaidi. Anabainisha kwamba mradi ukikamilika, wanatarajia kupokea wanafunzi takriban 2,500, kati yao 2,100 watasoma kozi ndefu na 400 kozi fupi.

Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Sylivia Lupembe, anasema miradi hiyo nchini na mataifa ya Ethiopia na Kenya, imeboresha elimu na kuwaongezea ujuzi wanafunzi, kuzalishwa ajira, ongezeko la matumizi ya teknolojia, pia uvumbuzi.

“Tanzania mradi huu umefanikiwa kwa asilimia 100, tumekuwa kinara kuwa na  Mfumo wa Uhakiki wa Vigezo vya Elimu  unaozingatia  muundo  ambao unawezesha kutambua na kulinganisha viwango vya elimu, mafunzo na ujuzi kwa kuhakikisha wahitimu wanatimiza viwango vya kitaaluma vinavyotakiwa.