Gamondi apania 'gharika' kwa CBE

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 10:18 AM Sep 18 2024
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi.
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi.

KUELEKEA mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema anaamini wachezaji wake watafanya vizuri Jumamosi kwa kufunga mabao mengi katika Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar dhidi ya CBE ya Ethiopia kutokana na kufanyia marekebisho kasoro zilizojitokeza kwenye mechi ya awali.

Gamondi aliyasema hayo jana wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari katika siku ya kukutana na vyombo vya habari, tukio ambalo lilifanyika makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam.

"Malengo yangu ni kuingia hatua ya makundi kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuhakikisha tunafanya vizuri katika mchezo wetu wa Jumamosi," alisema.

Yanga inapigania kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya pili mfululizo na mara ya tatu tangu kuanzwa kwa mfumo wa makundi.

Mara ya kwanza ilikuwa 1998, ambapo ilimaliza ikiwa ya mwisho kwenye kundi, msimu uliopita ilifanikiwa kufika hatua ya robo fainali ilipotolewa na Mamelodi Sundows ya Afrika Kusini kwa mikwaju ya penalti 3-2 baada ya timu hizo kutoka suluhu katika michezo yote miwili wa kwanza ukianzia Dar es Salaam na wa pili ukichezwa, Afrika Kusini.

Gamondi alisema mchezo uliopita dhidi ya CBE wachezaji wake walicheza chini ya kiwango kwani walipata nafasi nyingi na kushindwa kuzitumia. 

"Mchezo uliopita mengi yalisemwa, lakini tunashukuru tulipata pointi tatu katika mchezo huo kwa sasa tunajipanga kwa ajili ya mechi yetu ya marudiano ambayo naamini itakuwa na ushindani mkubwa," alisema kocha huyo raia wa Argentina. 

Aidha, alisema maandalizi ya mchezo uliopita yalikuwa na changamoto kutokana na wachezaji wake walikuwa kwenye timu za taifa, hivyo kukosa muda wa kutosha kuandaa mbinu za pamoja, lakini sasa amepata muda wa kuwa na kikosi chake chote. 

Kwa upande wa Meneja wa Klabu hiyo, Walter Harrison, alisema malengo yao ni kufanya vema kwenye mchezo wao wa marudiano ili waweze kuingia hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. 

"Kwa sasa tunaendelea kuwajenga kisaikolojia wachezaji wetu ili tuweze kupata pointi tatu katika mchezo wetu huo, uwanja ambao tutakwenda kuutumia tunaufahamu kwa kuwa tulishawahi kuutumia," alisema Harrison. 

Naye Nahodha wa timu hiyo, Bakari Mwamnyeto, alisema malengo yao ni kufanya vizuri katika mchezo wao wa marudiano na kuweka wazi mchezo uliopita ulikuwa mgumu na wenye ushindani. 

"Mchezo uliopita tatizo lilikuwa baadhi ya wachezaji wetu walikuwa wamechoka kutokana na majukumu ya timu ya taifa pamoja na hali ya hewa," alisema Mwamnyeto. 

Mwamnyeto pia alikiri mchezo uliopita walipata nafasi nyingi na kushindwa kuzitumia na kudai kocha wao anaendelea kufanya marekebisho ili yasijirudie katika mechi ya marudiano. 

Katika hatua nyingine, Ofisa Habari wa Klabu ya Yanga, Ali Kamwe, amesema kikosi cha Yanga kitanarajia kuondoka jijini Dar es Salaam kesho kuelekea Zanzibar, huku kile cha CBE nacho kikitarajiwa kutua siku hiyo na kuunganisha moja kwa moja kwa boti kuelekea Zenji, ambapo huenda wakakutana bandarini, Dar es Salaam.

Kwa maana hiyo huenda timu hizo zikasafiri pamoja kesho kuelekea kwenye mchezo huo ambao utapigwa saa 2:30 usiku kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar baada ya mchezo wa kwanza uliopigwa, Uwanja wa Abebe Bikila, Jumamosi iliyopita, Yanga kupata ushindi wa bao 1-0.

"Maandalizi yanakwenda vizuri sana, mwalimu Miguel Gamondi amekuwa na kibarua cha kuwaelekeza wachezaji nini cha kufanya kwenye mchezo huo hasa kwenye kutumia nafasi na tunaamini mchezo wa Jumamosi utakuwa mzuri kwetu na mashabiki tunawaomba wajitokeze kwa wingi waje kufurahia ushindi pamoja na soka safi la kushambulia," alisema.