Rais CAF atoa kauli Simba kufanyiwa fujo

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:44 AM Sep 18 2024
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe
Picha:Mtandao
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe

KABLA hata barua ya malalamiko ya Klabu ya Simba haijaanza kufanyiwa kazi, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe, ameagiza kufanyika uchunguzi dhidi ya vurugu walizofanyiwa wachezaji na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo nchini Libya Jumapili iliyopita, kabla, wakati wa mechi na baada ya kumalizika kwa mchezaji wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahli Tripoli nchini humo.

Akizungumza nchini Kenya juzi, Motsepe alisema akiwa kama rais kwenye kipindi chake cha kuwapo madarakani, hatoweza kuvumilia kuona timu kuna ambayo inaweza kukubaliwa kufanya vitendo vya vurugu ambavyo vinalishushia heshima soka la Afrika, hivyo kuamua kufanyika uchunguzi haraka.

Rais huyo alikuwa akijibu moja kati ya maswali ya waandishi waliokuwa kwenye Kikao cha Watendaji Wakuu wa CAF, kilichofanyika nchini Kenya, ambapo pamoja na mambo mengine, wanahabari walipata nafasi ya kumuuliza maswali rais huyo mwenye dhamana ya soka la Afrika.

Kwa mujibu wa mwandishi, Collins Okinyo, aliyehudhuria mkutano huo wa wanahabari na rais wa CAF, alisema awali Motsepe alikuwa haelewi nini kimetokea na baada ya kuambiwa hivyo, alionekana kushtuka.

"Kwanza alishtuka, inaonekana hakuwa anafahamu hilo, aliulizwa na mmoja wa waandishi hapa Kenya,  halafu akaamuru mmoja wa watu wa CAF, Samson Adam, afanye uchunguzi wa tukio hilo ambalo linalishushia heshima soka la Afrika, amesema akiwa kama rais hakuna timu ambayo inaweza kukubaliwa kufanya vitendo vya vurugu," alisema mwandishi huyo.

Ingawa klabu hiyo haikutaka kuliweka hadharani jambo hilo, lakini taarifa kutoka ndani zinasema tayari wameshatuma malalamiko CAF ili wachukue hatua, kutokana na mashabiki wa klabu hiyo kufanya fujo kubwa kwenye Uwanja wa Juni 11 jijini Tripoli, wakati mechi ikiendelea na baada ya hapo.

Baadhi ya vyombo vya habari nchini humo na waandishi mbalimbali wa Afrika waliokuwapo katika mchezo huo, wamethibitisha klabu hiyo kushtaki juu ya vurugu iliyofanywa na wenyeji wao.

"Simba imeamua kutuma mlalamiko CAF dhidi ya Al Ahli Tripoli na hili limethibitishwa.

"Chupa za maji, vitu vya plastiki walirushiwa wachezaji na viongozi, lakini pia lugha mbaya, matusi, maneno ya kibaguzi na kushambuliwa kwa wachezaji na baadhi ya viongozi wa timu hiyo ya Tanzania vilitolewa, kabla na baada ya mechi yao iliyoisha kwa sare ya bila ya kufungana usiku wa Jumapili iliyopita.

"Viongozi wa Simba wamekusanya ushahidi wote uliopo na  wameuwasilisha CAF ili kutafuta haki na adhabu dhidi ya upande wa klabu hiyo ya Libya," vyanzo mbalimbali vya habari viliandika.

Baada ya mchezo huo iliripotiwa viongozi na wachezaji walipigwa chupa za maji, ambapo hali ilikuwa mbaya uwanjani kiasi cha wachezaji kukimbizwa haraka vyumbani.

Meneja Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, alisema wakiwa jukwaani, golikipa Aishi Manula alishambuliwa, huku mashabiki wa timu hiyo wakiendelea kufanya fujo uwanjani kwa saa kadhaa ambapo ililazimika wakae vyumbani hadi fujo zilipopungua.

Tayari kikosi cha Simba kimewasili alfajiri ya leo na kwenda moja kwa moja kambini tayari kwa mchezo wa marudiano utakaochezwa Jumapili ijayo, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kikosi hicho kimewasili kwa makundi mawili, kimoja kikipitia nchini Uturuki na kingine Cairo nchini Misri.

Ahmed, alisema kuwa Kocha Mkuu, Fadlu Davids, amemwambia kuwa kwa sasa anaandaa mfumo na mbinu za kushambulia baada ya mfumo wa kwanza kufanikiwa.

"Kila kitu kinakwenda sawa, hatuna majeruhi na wote wako tayari kwa mchezo unaofuata. Mechi bado ni ngumu na haijaisha ndiyo maana tunaendelea kujiandaa ili kushinda na kwenda hatua ya makundi.

"Fadlu amejiandaa na mbinu na mfumo wa kucheza nyumbani, mechi iliyopita ilikiwa ni mbinu ya kucheza ugenini kuhakikisha hatupotezi na hilo limefanikiwa, kwa sasa anaandaa mpango madhubuti kuhakikisha tunapata ushindi, katika mechi ya marudiano linatakiwa jambo moja tu ni ushindi, sare haitusaidii, kitu pekee kitakachotuvusha ni ushindi," alisema.