Kongamano Ekaristi Takatifu liwe somo kulinda haki, amani na demokrasia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:30 AM Sep 18 2024
Katibu Mkuu CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi,  akimsadia Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara Tundu Lissu kupanda jukwaani, katikati ni John Mnyika  Katibu Mkuu CHADEMA , wakishiriki  Kongamano la Ekaristi Takatifu.
PICHA: MTANDAO
Katibu Mkuu CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi, akimsadia Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara Tundu Lissu kupanda jukwaani, katikati ni John Mnyika Katibu Mkuu CHADEMA , wakishiriki Kongamano la Ekaristi Takatifu.

KENGELE ya wito wa kudumisha amani, umoja, maelewano na mapatano imepigwa na Kanisa Katoliki, ikihimiza na kukumbusha taifa kuthamini zawadi kuu ya uhai na kuendeleza mshikamano wa udugu wa Watanzania.

Jukumu kubwa   ni la viongozi wa vyama vya siasa kutimiza wajibu ili kuliweka taifa pamoja ndani ya ramani ya kisiwa cha amani na utulivu na mhifadhi wa  kila raia bila kujali kabila, dini itikadi wala mtizamo. 

Kanisa kuwakutanisha wanasiasa na viongozi mbalimbali   kutoka  serikalini na  upinzani , kuwe njia ya kufungua pazia na kuingia kwenye barabara itakayoiweka pamoja  Tanzania Bara na Visiwani kabla na baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa na ule mkuu wa 2025. 

Wito wa Kongamano la Ekaristi ni ‘udugu wa kuponya ulimwengu’  lakini uwe udugu kuiponya Tanzania , ukiwakumbusha pia viongozi  wa kijamii, dini,wasomi wanataaluma wa kila aina na mashirika ya kiraia  kuwa   wadau wa kuhubiri umoja na  amani ya taifa . 

Makamu Mwenyekiti  wa CHADEMA, Tundu Lissu, Katibu  Mkuu wa chama hicho John Mnyika na  Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi  wanakutana na kutazamana ana kwa ana  wakiwa kwenye  kongamano hilo  la tano la Ekaristi Takatifu katika Uwanja wa Taifa,  jijini Dar es Salaam, ushirikiano huo uendelezwe kwa manufaa ya kila mmoja.  

Wameitwa, wameitikia wito. Hawakupuuza bali  walisimama mbele  ya halaiki ya waamini wengine  wakiwa pamoja kwenye  ibada na  mbele  ya Mungu  kuonesha utayari wa kushirikiana. 

Uamuzi huo si mdogo wala si wa kupuuzwa tena si wa  kubahatisha .Badala yake  wamethibitisha kiapo chao katika  dhima ya kusimamia  ustawi wa maendeleo  ya amani  ,utulivu, kuthamini utu  na upendo. 

Hatua ya kukutanishwa kwao ni wito wa moja kwa moja katika kuonesha  kutii   mbele ya jamii inayowatazama wakiwa viongozi  na wanaotegemewa na wananchi kuwaongoza katika njia inayonyooka na inayojali haki za wote. 

Viongozi hao  kukutana  katika ibada moja,haitokani na nguvu au ujanja wao bali ni karama toka  kwa Mungu, inayoelekeza wito wa kuwataka  kuepusha aina zote na majanga yanayotishia hatma bora ya taifa. 

Kongamano hilo liwakumbushe wanasiasa na raia kuwa kauli mbiu kama tunahitaji  ‘ watu, ardhi, siasa safi, uongozi bora, maendeleo ya uchumi, ustawi wa  demokrasia ,utawala wa sheria au  kuenzi haki za binadamu  ili tuendelee havitafikiwa  ikiwa amani itapuuzwa , kuchezewa na kuachwa itoweke. 

Popote duniani amani, utulivu na umoja vilipokosekana kilichotawala ni shari, kuporomoka maadili, chuki , kukosa maelewano, vita, kumwaga damu, uasi na vifo vinavyoondoa zawadi kuu ya uhai ambayo ni haki ya msingi ya binadamu. 

Watanzania wakumbuke kuwa haipo nchi   yoyote  duniani iliyofuzu kama haikuenzi amani na umoja wa  kitaifa, kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria.  

Tanzania iliyojenga na kudumisha umoja wake, udugu wa watu wake bila kutumia  nguvu na ushawishi wa ukabila ,dini, rangi au ukanda, haipaswi ikubali ipoteze tunu ya mshikamano wake kwa sababu yoyote.

 Kengele  iliyopigwa kwenye kongamano  la tano la Ekaristi Takatifu imewajumuisha wanasiasa kwa niaba ya vyama na wafuasi wao.Viongozi wa vyama  vikuu CCM na CHADEMA  wakisimama bega  kwa bega mbele ya viongozi  wa dini yote hiyo ikionesha njia ya muafaka.

 Kusimama  kwao kuwe mwanzo wa kuelekea katika maelewano thabiti na kutuma ujumbe utakaodumisha   amani badala ya kutokea vurugu, chuki na hamaki  na wakati mwingine habari za mauti.

Siku  zote jazba, chuki, husuda na hamaki hazijajenga  badala yake vitu hivyo vinadhoofisha hupoteza uhai na  maisha ya watu, kuvuruga amani ,maelewano , maendeleo ya kisekta na kuwarudisha nyuma watu na taifa wakibakia masikini tena wanaosongwa na migawanyiko.

 Historia siku zote  ni mwalimu, Tanzania  bila amani isingefanya  lolote katika  harakati za kujenga nchi, kupigania  uhuru  wake na kufanikisha  ukombozi Kusini mwa Afrika na kuhifadhi wapigania  uhuru wa kila pembe ya dunia .

 Vyama kadhaa vya wapigania  uhuru viliendeleza harakati zake katika  ardhi ya Tanzania  ili viweze kupigania  uhuru, kutafuta haki ,usawa na umoja katika nchi zao na leo Msumbiji, Angola, Zimbabwe, Afrika Kusini ni huru.

 Katika  vipindi  hivyo  vyote Tanzania ilikabiliana na  mitikisiko,  misukosuko  ya ndani na nje, shida,vita na Uganda, furaha na misiba lakini imeendelea kuwa kisiwa cha amani na utulivu kutokana na taifa  kuwa na umoja , amani,  utulivu na mshikamano wa kindugu.

 Licha ya kuwepo taabu , dhiki na hata upungufu wa baadhi ya bidhaa  na huduma muhimu za kufanikisha maisha, Watanzania walibaki  wamoja  katika nyakati  zote  hatimaye  kupata ushindi wakishikamana hivyo hata sasa amani hiyo iendelezwe kwa juhudi zote.

 Sauti na   wito kutoka katika kongamano hilo  ni sauti muhimu  kusikilizwa . Ni ujumbe  wa amani wala si utani  au  mzaha bali ni wazi  viongozi wa vyama vya siasa wanatakiwa kukutanishwa pamoja mezani  kujadili hatma ya nchi hasa kudumisha amani ushirikiano na umoja pia kudumisha demokrasia na uhuru ambavyo ni haki ya kila mmoja. 

 Viongozi wa dini wameonesha njia ya kujenga demokrasia na misingi ya utawala bora kwa vyama vya siasa kushindana kwa hoja pamoja na dhamana ya kusimamia kwa vitendo usalama wa raia, uhai wao  na mali zao, kujenga uchumi   na kujiepusha na  sintofahamu zinazojitokeza na kutia doa historia ya taifa hilo linalotukuka kwa amani na kushikamana.