Ndivyo wagombea urais Marekani walivyochuana

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:33 AM Sep 18 2024
DONALD Trump na Kamala Harris
Picha:Mtandao
DONALD Trump na Kamala Harris

DONALD Trump na Kamala Harris wametunishiana misuli kwa mara ya kwanza kwenye jukwaa la mdahalo wa urais huko jijini Philadelphia.

Wanaofuatilia mchuano huo wapo wanaoweza kumwita mgombea wa Democrat Kamala Harris ‘the sleeping giant.’ Wakati Mzee Trump akibaki na viulizo. 

Ikimaanisha kuwa ana nguvu lakini bado hajaonyesha kiwango kamili cha uwezo wake.

Katika dakika 90 za patashika, Harris mara kwa mara alimvaa rais mstaafu Donald Trump kwa mashambulizi binafsi ambayo yalimtoa Trump kwenye mstari ni kwa mujibu wa BBC.

Harris anazungumzia mwenendo wa Trump wakati wa ghasia za Capitol au jengo la bunge na maofisa waliohudumu katika utawala wake ambao wamekuwa wakosoaji wa wazi wa kampeni zake mara kwa mara, akimuacha Trump katika wakati mgumu. 

Sehemu kubwa ya mdahalo huu, Harris alimweka mpinzani wake wa Republican katika mazingira ya kutoa utetezi kuhusu mwenendo na maoni yake ya zamani.

 Wakati mwingine Trump akalazimika, kupaza sauti yake mara kwa mara na kutikisa kichwa, inaeleza BBC.

“Wamarekani wanapaswa kwenda kwenye mkutano wa Trump,” Harris anasema wakati wa swali la mapema kuhusu uhamiaji. "Watu huanza kuondoka kwenye mikutano mapema kutokana na uchovu na kuchoka," anasema.

Shambulizi hilo ni wazi lilimkera rais huyo wa zamani, akatumia sehemu kubwa ya jibu lake - kwenye mada ya uhamiaji ambayo ni moja ya eneo kuu la nguvu, kutetea ukubwa wa mikutano yake na kudharau kampeni za Harris.

Trump anakwenda mbali zaidi hadi katika ripoti iliyokanushwa kwamba wahamiaji wa Haiti katika mji wa Springfield jimboni  Ohio, walikuwa wakiteka nyara na kula wanyama wanaofugwa sehemu hiyo.

 Iwapo midahalo ina kushinda na kupoteza, ni mgombea yupi anayetumia vyema masuala ambayo yanampa nguvu  na kutetea hoja au kukwepa maeneo yenye udhaifu kwake, kilichofanyika Jumanne iliyopita usiku utasema ulikuwa ni wakati wa Makamu wa Rais Kamala, inasema BBC.

Katika mada za uchumi na kutoa mimba zilipojadiliwa, uchunguzi wa maoni ya umma unaonyesha Wamarekani wengi hawajafurahishwa na jinsi utawala wa Biden ambao Harris ni mwanachama muhimu  ulivyoshughulikia mfumuko wa bei na uchumi.

Lakini Harris anageuza mada hiyo na kuzungumzia ushuru uliopendekezwa na Trump, na kuuita ni “kodi ya mauzo ya Trump” na kisha akaleta mradi wa 2025, mpango huru wenye utata wa utawala wa baadaye wa Republican.

Kama ilivyokuwa huko nyuma, Trump anajitenga na mradi huo na kutetea mpango wake wa ushuru, akibainisha kuwa utawala wa Biden ulikuwa umeweka ushuru mwingi katika muhula wake wa kwanza wa urais. 

Zilikuwa hoja halali, lakini zilimzuia kumkosoa Makamu wa Rais kuhusu  mfumuko wa bei na ugali wa bidhaa, inaeleza BBC.

Kuhusu mimba, Trump anatetea jinsi alivyoshughulikia suala hilo, akisema Wamarekani katika nyanja mbalimbali wanataka sheria ya kutoa mimba ya Roe  Wade ibatilishwe na Mahakama ya Juu. Kauli ambayo kura za maoni haziiungi mkono. Anahangaika kueleza msimamo wake na jibu lake wakati fulani lililokuwa la kukurupuka.

Kamala, wakati huo huo, anachukua fursa hiyo kutoa kauli ya hisia kwa familia ambazo zimekabiliwa na matatizo ya ujauzito na hazijaweza kupata huduma ya kutoa mimba katika majimbo ambayo yamepiga marufuku utaratibu huo, yenye "marufuku ya Trump ya kutoa mimba".

Kama alivyoyaita Kamala: "Ni matusi kwa wanawake wa Marekani," anahitimisha.

Ni ujumbe uliopangwa kwa uangalifu katika eneo ambalo ana faida kuliko Trump, BBC inachambua.

Wakati mdahalo ukiendelea, Harris anamweka Trump kwenye mashambulizi na kejeli, ambazo angeweza kupuuza lakini inalazimika kuzijibu.

Wakati mmoja, Harris anaulizwa maoni yake ya uchumi aliyo achana nayo zamani, wakati wa kampeni yake ya urais iliyoshindwa 2019.

Rais wa zamani badala ya kumkosoa Makamu wa Rais juu ya maoni yake yanayobadilika, kuonyesha udhaifu wake wa wazi, alifungua majibu yake kwa kuzungumza "sehemu ndogo" ya pesa aliyochukua Kamala kutoka kwa baba yake.

Kuhusu kujiondoa Afghanistan, eneo jingine dhaifu kwa Harris, Makamu wa Rais, anahamisha mazungumzo na kuyapeleka kwenye maelezo ya Trump na maofisa wa Taliban na kuwaalika Camp David, eneo maarufu kwa shughuli za marais wa nchi hiyo. 

Ilikuwa ni mbinu ambayo ilijirudia na ilionekana kufanya kazi vizuri.

Wanachama wa Republican tayari wanalalamika kuhusu kile wanachosema ni upendeleo ambao wasimamizi wa ABC, David Muir na Linsey Davis, waliuonyesha kwa Harris. Wote wawili walimrudisha nyuma Trump na kukagua madai ya uongo aliyoyatoa mara kadhaa.

Mwishowe, hata hivyo, yalikuwa ni majibu ya Trump na shauku ya kuchukua na kula chambo chochote ambacho Harris alikiweka katika mdahalo wa jioni.

Wakati wowote mpinzani wa Harris alipokuwa akizungumza, Harris aliweka sura ya mshangao au kutokuamini. Trump, kwa upande wake, sura ya kukasirika zaidi.

Timu ya kampeni ya Harris ilikuwa haijaamua hapo awali ikiwa itakubali mjadala mwingine. Mara tu baada ya huu kumalizika, wataitisha mjadala wa pili wa urais kabla ya Novemba.

Hiyo pekee inaonyesha jinsi wanachama wa Democratic walivyoona namna Jumanne usiku ilivyokwenda kwa Harris, kwa mujibu wa BBC.