Samia avunja ukimya utekaji, mauaji

By Elizabeth Zaya ,, Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 11:08 AM Sep 18 2024
Gwaride la heshima lililoandaliwa na Jeshi la Polisi likipita mbele ya Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Dk. Samia Suluhu Hassan wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya jeshi hilo, katika Shule ya Polisi Tanzania (TPS), Moshi, mkoani Kilimanjaro jana.
PICHA: IKULU
Gwaride la heshima lililoandaliwa na Jeshi la Polisi likipita mbele ya Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Dk. Samia Suluhu Hassan wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya jeshi hilo, katika Shule ya Polisi Tanzania (TPS), Moshi, mkoani Kilimanjaro jana.

RAIS Samia Suluhu Hassan rasmi amevunja ukimya, akiwa na ufafanuzi wake kuhusiana na madai dhidi ya serikali juu ya matukio ya utekaji na mauaji ya watu.

Sambamba na hilo, Rais amelielekeza Jeshi la Polisi katika maeneo manne yanayogusa ufanisi wa utendaji wake, akioanisha na madai yanayoendeleza kuelekezwa kwalo. 

Mkuu wa Nchi aliyasema hayo jana kwenye Shule ya Polisi Tanzania (TPS) iliyoko Moshi, mkoani Kilimanjaro, ambako alishiriki Maadhimisho ya Miaka 60 ya jeshi hilo, akifunga mkutano mkuu wa mwaka wa maofisa waandamizi, makamanda wa mikoa na vikosi. 

Rais aliagiza wizara na jeshi hilo kuendelea kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai kwa ukamilifu na kuendelea kutekeleza mapendekezo yote yasiyohitaji mabadiliko ya sheria au ongezeko kubwa la bajeti. 

Aliagiza Jeshi la Polisi kama walinzi wa raia na mali zao ambalo lina haki ya usimamizi wa haki na sheria, halipaswi kuhusishwa au kuhisiwa kwa namna yoyote katika tuhuma za ukiukwaji wa sheria na haki linazosimamia.

 Rais alielekeza jeshi hilo liongeze kasi ya matumizi ya Tehama ili lidhibiti uhalifu na wahalifu kwa ufanisi zaidi. 

Vilevile, alielekeza wizara kutekeleza maelekezo ya serikali kuhakikisha mifumo inasomana na taasisi nyingine. 

Mkuu wa Nchi alionesha kukerwa na matukio ya mauaji na utekaji watu yanayoendelea kuripotiwa nchini, akitaka jamii kutofumbia macho vitendo hivyo kwa kushindwa kutoa taarifa na kusubiri kulaumu jeshi kutoa matamko na kulaani.

 Alisema serikali inazo taarifa kuhusu njama zinazopangwa na baadhi ya watu wanaoendesha mipango ya uvunjifu wa amani, akionya kuwa serikali haitawavumilia. 

"Tumeshuhudia mauaji ya watu wazima na watoto kwa imani za kishirikina kama ilivyoibuliwa na Jeshi la Polisi hivi karibuni, kumekuwa na matukio ya wapenzi kuuana, wazazi kuua watoto na watoto kuua wazazi wao kikatili na kisha maiti kuchomwa moto na wengine kukatwa vipande na kufukiwa, na mambo ya aina hiyo ambayo kwa vyovyote vile hayaridhishi.

 "Huku ni kuondokwa na utu na ni uhalifu mkubwa sana, wananchi wanakata tamaa kuona matukio haya yanahusishwa si tu na waganga wa kienyeji, bali hata watu mashuhuri kama viongozi wa dini na hata wazazi na watoto," alisema.

 Akizungumzia tukio la kuuawa kwa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Ali Kibao lililotokea hivi karibu, Rais Samia alisema serikali ilisikitishwa na jambo hilo na kutoa maelekezo kwa vyombo vya dola.

 "Kifo hicho kimeleta hisia kali pia kwa wawakilishi wa baadhi ya mataifa ya nje na wawakilishi wa nchi zao hapa kwetu. Ninataka niungane nao na niseme kwamba kwa sababu yoyote ile, mauaji haya hayakubaliki na ndio maana serikali tuliyalaani na kutaka uchunguzi wa haraka ufanyike na ndivyo inavyofanyika duniani kote.

 "Baada ya mambo haya kutokea, serikali husimama kulaani na kutaka vyombo vyake vya usalama kwenda na uchunguzi na tujue kilichotokea na kazi hii nimeambiwa inaendelea vizuri," alisema.

 Aliendelea: "Niseme tu kwamba baada ya tukio lile, nimekuwa nikiangalia maoni ya viongozi mbalimbali wa kisiasa, viongozi wa dini na baadhi wakiniomba nikemee mambo hayo.

 "Maoni ya wazee mashuhuri, nimemsikia Mzee Butiku naye kasema, wawakilishi wa mataifa ya nje hapa nchini nao wametoa matamko, jumuiya za kiraia na wananchi kwa ujumla nao wamesema waliyoyasema.

 "Hisia za makundi yote niliyoyataja, zikiibuliwa na kifo cha mtu mmoja tu niliyemtaja, ndugu yetu Ali Kibao, lakini kuna vifo vinasemwa muda baada ya muda, watoto albino wanakatwa mikono, wanauliwa, watoto wadogo wanachukuliwa, wanakatwa sehemu nyeti wanatupwa, sijui nani wanauliwa.

 "Mpaka leo (jana) asubuhi nimepewa ripoti huko Dodoma watu watatu wamekutwa chumbani wameuliwa, lakini yanapotokea haya kwenye maeneo yetu lakini kuko kimya mpaka polisi iibuke iseme, wengine hawasemi.

 "Hii inashangaza kwamba kifo cha ndugu yetu Kibao, kimeibua wimbi kubwa kulaani, kusikitika, kulaumu, kuita serikali ya wauaji, hii si sawa," Rais Samia alitamka kwa hisia kali.

Mkuu wa Nchi alisema, "Nilikuwa nasikiliza kwa makini, maelezo yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, nimerushiwa na nimeisikiliza vizuri sana clip ya Dk. Slaa wa CHADEMA, vilevile clip ya Joseph Yona wa Chalinze, wote wakitoa mipango ya taswira ya uvunjifu wa amani inayopangwa na baadhi ya vyama vya siasa.

 "Nayaunganisha haya na uamuzi wa kikao cha Septemba 11 mwaka huu kilichofanywa na chama kimoja cha siasa kule Ngurelo, mkoani Arusha, ambacho kimeazimia kuwatumia na kuwachochea vijana kwa kuzusha tuhuma dhidi ya Jeshi la Polisi, kufanya siasa chonganishi kwenye misiba na kushusha morali kwa jeshi hilo ili washindwe kufanya kazi yao ya kulinda usalama wa raia na mali zao."

 Rais Samia pia alitunuku vyeti vya pongezi kwa askari polisi wastaafu 10 wa kwanza kabla na baada ya uhuru, waliotumikia jeshi hilo kwa uzalendo, uhodari na ujasiri hadi walipostaafu kwa heshima.

 Kati ya askari hao wastaafu, wamo ambao walikuwa miongoni mwa askari wanane wa kwanza wa kike waliojiunga na kuajiriwa katika Jeshi la Polisi Tanganyika mwaka 1958.

 Pia yumo askari wa kike ambaye ni miongoni mwa askari wa kike 12 wa kwanza kuajiriwa na Jeshi la Polisi Zanzibar baada ya Mapinduzi Matukufu.