Azam yazitaka tatu za kwanza Simba

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 10:11 AM Sep 18 2024
Azam FC
Picha: Azam FC
Azam FC

KATIKA kuhakikisha inazipata pointi tatu za kwanza kwenye mchezo wa Ligi Kuu msimu huu Klabu ya Azam inaendelea kujifua vikali ikijiandaa na mechi yao ijayo dhidi ya Simba itakayopigwa Septemba 26, mwaka huu.

Tangu msimu wa Ligi Kuu 2024/25, uanze, Azam FC hajafanikiwa kuzoa alama zote tatu kwani katika michezo miwili iliyocheza yote imeambulia sare.

Akizungumza na Nipashe jana, Msemaji wa timu hiyo, Thabit Zakaria maarufu Zaka Zakazi, alisema malengo yao ni kutwaa ubingwa msimu huu kwa kufanya vizuri katika michezo yao yote ilisalia. 

"Kwa sasa tunajiandaa na mchezo wetu ujao dhidi ya Simba, ni mchezo ambao unatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa kutokana na aina ya timu tunayokutana nayo," alisema Zaka Zakazi. 

Alisema kwa sasa kila mchezaji ana morali ya juu kuhakikisha wanapata matokeo katika mchezo wao huo na kuomba mashabiki wao waendelee kuwaunga mkono. 

Zaka Zakazi alifafanua kuwa licha ya msimu huu kuwa mgumu na wenye ushindani mkubwa, watapambana ili waweze kuipa mafanikio timu yao hiyo. 

"Msimu huu una ushindani kutokana na maandalizi yaliyofanywa na kila timu, lakini tutapambana ili tupate nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa kwa mara nyingine msimu ujao," alisema Msemaji huyo. 

Alisema licha ya kutolewa kwenye mashindano ya kimataifa, bado hawajakata tamaa na badala yake wataendeleza ushindani ili msimu ujao waweze kushiriki tena. 

Azam FC ambayo msimu huu ilikuwa ikiiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ilitolewa raundi ya awali na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 2-1, baada ya kushinda bao 1-0 nyumbani na kwenda kukubali kulala kwa mabao 2-0 katika mechi ya marudiano ugenini.