Malasusa aungana na wadau vilio vya utekaji, mauaji

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:17 AM Sep 18 2024
Askofu Dk. Alex Malasusa
Picha:Mtandao
Askofu Dk. Alex Malasusa

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa, amesema matukio ya kutekwa au kutoweka kwa Watanzania ambayo hayakuzoeleka na yanayoendelea hivi sasa, yanapaswa yafike mwisho.

Pia, amemuomba Naibu Waziri Mkuu, Dk. Dotto Biteko, kufikisha salaam za kanisa hilo kwa viongozi wakuu wa nchi kuruhusu kuwapo na meza ya majadiliano ili kupatikane suluhisho la hayo mauaji.

Askofu Dk. Malalsusa, alitoa ujumbe huo wa KKKT jana katika Kanisa Kuu la Usharika wa Mwanga, wakati wa ibada ya maziko ya aliyekuwa Askofu wa Dayosisi ya Mwanga, Dk. Chediel Sendoro, aliyezikwa katika Kanisa Kuu la Usharika wa Mwanga.

Askofu Dk. Chediel Sendoro, alipoteza maisha Septemba 9, mwaka huu kwa ajali majira ya saa 1:30 usiku, baada ya gari alilokuwa akiendesha kugongana uso kwa uso na lori eneo la Kisangiro, wilayani Mwanga.

Dk. Chediel Sendoro, ni mtoto wa Askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Elinaza Sendoro. 

Akizungumzia matukio ya utekaji na kutoweka kwa Watanzania, Dk. Malasusa alisema, “Nimepata fursa ya kutamka masikitiko yetu, hasa kwa hali inayoendelea katika nchi yetu kwa kusikia habari ambazo sio nzuri. Vifo, utasikia habari nyingi sana katika kipindi hiki, hasa katika barabara zinazounganisha nchi yetu na hakika sisi sote tukichukua wajibu wetu, basi huenda tukavifuta au kuvipunguza.

“Lakini samabamba na hilo, masikio yetu na mengine yameshuhudia jinsi ambavyo tumekuwa na matukio ambayo hayakuzoeleka, hasa tukitumia maneno yanayotumika sasa ‘kutekwa’ au ‘kutoweka’ kwa Watanzania.

Nafikiri tuseme hivi ifike mwisho, kanisa liombe kwa ajili ya jambo hilo. Na mauaji ndugu zangu, Biblia iko wazi kabisa, nchi inalaaniwa damu inapomwagika. Hatutaki laana iingie katika nchi yetu, tuombe kila mwenye kujua maana ya maombi kuliombea jambo hili; najua wanasiasa wamekuwa wakilizungumza, lakini hebu tulisogeze pia kama haja yetu mbele za Mungu.

“Nachukua fursa hii kuomba Jumapili zijazo wachungaji, maaskofu katika kanisa letu tuanze kuomba kama kitu cha pekee kilichotokea katika nchi yetu.

Naibu Waziri Mkuu (Dk. Dotto Biteko), niwasihi kama raia, kama kiongozi wa imani, wanasiasa kuruhusu kuwapo na meza ya majadiliano, huenda likapatikana suluhisho la haya mauaji.”

Kadhalika, Askofu Dk. Malasusa, alisema hivi sasa imekuwa tabia na hata wengine wanauawa, kwa sababu watu wanaonekana wanaiba watoto, wengine wamekuwa wakipigwa na mambo kadhaa wa kadhaa, hivyo ni vyema kuweka muda wa kuzidi kusikilizana.  

Kutokana na yanayoendelea, Dk. Malasusa amewaelekeza maaskofu wa KKKT, kama wanajua wana kitu, mawazo wasiache kuyatoa. Tumefika katika kipindi ambacho Watanzania wamekuwa na hofu.

AJALI ILIVYOKUWA 

Kamanda Maigwa, alisema kabla ya kupoteza maisha, Askofu Sendoro na mwanawe ambaye anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufani ya Kanda ya KCMC, alikuwa akitokea katika mji mdogo wa Himo, Wilaya ya Moshi kwenda Mwanga.

Alisema gari lake lilikuwa likiyapita magari mengine mawili na kisha kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa likitokea Tanga kwenda mkoani Arusha.

MAISHA YAKE

 Askofu Sendoro, ambaye hadi anafariki dunia alikuwa mhitimu wa Shahada ya Uzamivu (PhD) na Shahada ya juu ya Uhasibu (CPA), alizaliwa Mei 1, 1970 akiwa mtoto wa nne wa Askofu Dk. Elinaza Sendoro.

*Imeandikwa na Godfrey Mushi na Mary Mosha (Mwanga).