Mashindano makubwa matano ya soka duniani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:37 PM Jul 22 2024
Mashindano makubwa matano ya soka duniani.
PICHA: MTANDAO
Mashindano makubwa matano ya soka duniani.

SOKA ndio mchezo maarufu zaidi ulimwenguni na moja ya sababu za hilo ni idadi kubwa ya mashindano ya kusisimua na yenye mashabiki wengi ambayo hufanyika kila mwaka.

Iwe ni ndani ya nchi, bara au kimataifa, karibu kila siku kuna mechi za mashindano ya kandanda kwa wachezaji na wapenda soka.

Kuanzia Ligi ya Mabingwa hadi Kombe la Dunia, kandanda ina mashindano ya kipekee na ya kuvutia katika ulimwengu wa michezo.

Katika makala haya mtandao wa habari za michezo kutoka Uingereza, talksport – inataja orodha ya mashindano matano makubwa ya mpira wa miguu. Tukianzia namba tano:

 Copa Libertadores

Kombe la Copa Libertadores ndiyo mashindano makubwa ya soka kwa ngazi ya Klabu kwa Bara la Amerika Kusini. Mashindano hayo huandaliwa kila mwaka na Shirikisho la Soka la bara hilo, CONMEBOL, na hushirikisha timu 47.

Michuano hiyo huanza Februari na fainali hufanyika katika uwanja tofauti Novemba ya kila mwaka.

Tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo mwaka 1960. Klabu ya Independiente ya Argentina ndiyo timu iliyofanikiwa kubeba ubingwa mara nyingi katika historia ya mashindano hayo, ikiwa imeshinda mara saba.

Copa America

Copa America pia ni mashindano ya mpira wa miguu kwa Mataifa ya Amerika Kusini. Yalianzishwa mwaka 1916, Copa America ndio mashindano kongwe zaidi ya mpira wa miguu duniani.

Kwa aina ya vipaji vinavyooneshwa katika mashindano hayo, Copa America ni mojawapo ya mashindano ya soka yaliyotazamwa zaidi duniani.

Jumla ya mataifa 19 hucheza michuano hiyo huku Mexico na Marekani zinazotokea sehemu ya Kaskazini ya Mataifa ya CONMEBOL, zikishiriki pia.

Baadhi ya wachezaji wakubwa wamecheza kwenye Copa America wakiwamo Lionel Messi, Neymar, Pele na Diego Maradonna. Argentina ndio wanashikilia taji la Copa America kwa sasa baada ya kulitwaa mwezi huu, kwa mwaka 2024.

Argentina ndilo taifa lililofanikiwa zaidi katika michuano hiyo kwa kushinda mara 16. Michuano ya Copa America pia inaalika mataifa kutoka CONCACAF (Asia) kushiriki michuano hiyo. Michuano hiyo imeshirikisha timu za Japan na Qatar. Vilevile Australia na China zimekuwa miongoni mwa waalikwa. 

Ligi ya Mabingwa Ulaya

Ligi ya Mabingwa Ulaya ni mashindano makubwa ya ngazi ya Klabu barani Ulaya. Ni michuano ya kila mwaka inayozikutanisha timu bora kutoka ligi za Ulaya. Idadi ya timu kutoka kila nchi inatofautiana kulingana na nafasi ya ligi kwa mujibu wa viwango vya UEFA.

Ligi Kuu ya England, ndio ambayo mara nyingi huingiza timu nyingi, timu nne zikiingia kila mwaka. Katika mashindano ya 2024/25, Klabu za Arsenal, Manchester City, Liverpool, na Aston Villa zitacheza.

Michezo ya mashindano hayo huchezwa katikati ya wiki. Hatua ya makundi huanza Septemba, na hatua ya mtoano huanza Februari na fainali hufanyika Mei.

Real Madrid ndio klabu iliyofanikiwa zaidi katika historia ya mashindano hayo, na kushinda mara 14. Liverpool ndio klabu iliyofanikiwa zaidi ya England kwa kushinda mara sita. 

Michuano ya Euro

Hii huchezwa kila baada ya miaka minne, mwaka huu mashindano hayo yanayozikutanisha timu za Mataifa ya Ulaya (Euro), yamefanyika nchini Ujerumani na Hispania imeibuka mshindi.

Euro hukusanya baadhi ya wachezaji bora kote Ulaya. Mashindano hayo huwa na watazamaji wengi. Mashindano ya kwanza ya kimataifa ya Ulaya yalifanyika mwaka 1960 huko Ufaransa.

Mashindano kumi na saba yamefanyika. Hispania imeshinda mataji manne, Ujerumani wameshinda mara tatu, Italia na Ufaransa wameshinda mara mbili, na Umoja wa Kisovieti, Czechoslovakia, Uholanzi, Denmark, Ugiriki na Ureno zote zimeshinda mara moja kila moja.

Mnamo 2014, mashindano yalipanuka kutoka timu 16 hadi 24, lakini kupanuka huko hakukupunguza kushuka kwa ubora wa mashindano hayo. 

Kombe La Dunia

Kombe la Dunia la FIFA linaendelea kuwa shindano namba moja na kubwa zaidi katika soka ulimwenguni kwa sasa. Hukutanisha wanasoka bora kutoka kote ulimwenguni.

Baadhi ya wanasoka bora duniani wamecheza, wakiwamo Zinedine Zidane, Cristiano Ronaldo, Rivaldo, Diego Maradonna na Pele. Kombe la Dunia la FIFA linaendelea kuwa mashindano ya soka yanayotazamwa zaidi na kufuatiliwa zaidi.

Yalifanyika kwa mara ya kwanza 1930, huko Uruguay na hufanyika kila baada ya miaka minne isipokuwa 1942 na 1946 kwa sababu ya vita ya pili ya dunia.

Argentina waliibuka kuwa mabingwa wa Kombe la Dunia 2022 kwa mara ya tatu baada ya kuishinda Ufaransa kwa mikwaju ya penalti katika fainali ya mwisho iliyofanyika Qatar.