AFYA ya akili ni jambo muhimu kwa ustawi wa binadamu kwa kila hali ila, hupuuzwa mara nyingi au ni tatizo lisilopewa kipaumbele na familia hata jamii kubwa.
Mpaka sasa inatokea kusiwe na msaada wala tiba, kuendeleza unyanyapaa dhidi ya wenye shida ya afya ya akili na wapo watu wanaoamini kuwa wenye shida hizo wamerogwa, ni mkosi au wameadhibiwa kutokana na matendo yao ya kihalifu.
Sababu mojawapo ya changamoto ya afya ya akili ni msongo wakati mwingine huitwa msongo wa mawazo.
Wataalamu wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA), wanasema msongo ni hali inayojitokeza pale unapoona uwezo, maarifa au ujuzi hauendani na jambo lililo mbele yako.
Wanasema katika mazungumzo na machapisho waliyotoa wakati walipotembelea vyombo vya habari vya IPP Mikocheni Dar es Salaam na kuzungumza na wafanyakazi na kuwapima kisukari.
Wanaohudumiwa ni pamoja na wafanyakazi wa ITV, Radio One, East Televisheni, magazeti ya Nipashe na The Guardian na kuwapima uzito, sukari na kuwapa ushauri wa kiafya.
Wataalamu hao wanasema msongo unaweza kujitokeza pale malengo uliyojiwekea yasipotimia, au kufikiri hayatafanikiwa.
Kitabu cha Mtindo wa Maisha na Magonjwa yasiyoambukiza: Dalili, Athari na Kinga, kinachoandaliwa na TANCDA, kinaeleza kuwa msongo kwa kiwango fulani hufanikisha kuboresha utendaji kazi ila unapozidi unaathiri afya.
Wanakumbusha kuwa msongo husaidia mwili kupambana na hatari kwa kukimbia au kupambana, lakini ukiendelea kwa muda mrefu huongeza uwezekano wa kupata kisukari, shinikizo la damu, maradhi ya moyo, mishipa ya fahamu na fahamu, saratani na kuathiri mfumo wa kinga mwili.
Vyanzo vikuu vya msongo vinatajwa kuwa ni pamoja na mabadiliko ya kimaisha mfano kufiwa, kuugua, kuuguliwa, wasiwasi au mfadhaiko wa mambo ambayo yanaleta hofu licha ya kwamba hayajulikani.
Kingine ni muda unaobakia kutimiza lengo au kufanya kitu, kukosa mpangilio na uchovu wa mwili.
DALILI ZA MSONGO
Unadhihirika kwenye kuumwa kichwa, kukosa usingizi, hamu ya kula, kutokuwa na morali ya kufanya chochote au kutokufurahia kazi.
Nyingine kwa mujibu wa TANCDA ni uchovu wa mwili na akili, mabadiliko ya kihisia kama kukasirika kwa kitu kidogo, kupungua umakini au usahaulifu mara zote, kufanya makosa madogo madogo na kuwa na mawazo hasi zaidi wakati wote.
Dalili kama ulevi kupindukia, kutumia dawa za kulevya na tumbaku ni mojawapo ya mambo yanayoashiria kuwapo msongo wa mawazo.
Ni vizuri kuwa na malengo lakini malengo yasiwe hayaendani na uwezo na iposhindikana kuyatimiza inakuwa vigumu kukubali ukweli.
Ikumbukwe kila binadamu ni tofauti. Watu hawakuumbwa sawa kila mmoja ana uwezo na vipaji vyake na kila wakati hawawezi kulingana.
KUKABILI MSONGO
Unapopitia msongo wataalamu hao wanakushauri kuwa uwe na matumaini kwa kila tatizo, shida au changamoto unayopitia.
Fanya mambo yaliyo kwenye uwezo wako malengo au madhumuni yako kimwili, kiafya na kiroho kulingana vipaji ulivyo navyo ukizingatia jukumu lako, wanaongeza.
Kadhalika wanasisitiza kuwa na matumaini kuwa utafanikiwa kwa kila unachoamua, tena usipange kushindwa wala kukwama, kadhalika jijengee tabia ya kujitegemea kwa kujimudu mwenyewe na kujiendeleza kwa maeneo mbalimbali.
Wanasema ni vyema kujenga umahiri wa kusimamia na kutumia muda ipasavyo na kupanga vipaumbele ili uwe na imani na uwezo wako wa kudhibiti mazingira yako.
Wanashauri pia kuwa makini na jambo moja kwa wakati mmoja. Pia kujifunza kukubali kuwa huwezi kushindwa kila kitu na uwe tayari kusema ‘hapana’, zinapokuja fikira mbovu.
Wanasema ni vyema kugawa majukumu na kuomba msaada unapokwama au unapouhitaji.
Kuwa na tabia chanya na epuka kupima thamani yako mwenyewe kwa kujilinganisha na watu wengine, ni jambo jingine linalotajwa.
Wanashauri kushikamana na kuwa na mawasiliano na wengine, kuwa rahisi na tayari kukubaliana na wengine, pia shirikisha wengine maisha kwani kuna changamoto hasi na chanya ambazo lazima kupitia.
Kushirikisha mtu unayemwamini changamoto na shida au kuzungumza na mtaalamu wa afya ya akili yanayokusibu kunapunguza athari na kutoa fursa ya kukabili tatizo au kuwa na uhimilivu wa kuendana nalo, wanasema wataalamu hao.
Aidha, TANCDA inashauri kuwa na muda wa kufurahia muziki, kucheka na kushiriki michezo, sherehe, tamasha, burudani na mambo ya kiroho.
Shirikisho hilo linashauri pia kutumia muda kutembelea mazingira ya asili mfano misitu, wanyama, bahari, mito na kuangalia nyota angani kwa muda mfupi kama huna wa kutosha ili kuipa nguvu akili.
Ni vyema pia kusoma vitabu, vya elimu na maarifa na vitakatifu au kufanya mambo tofauti badala ya kukaa sehemu moja muda wote.
Shiriko hilo linahimiza kufanya mazoezi kila siku ili kupunguza kusononeka na kujiongezea furaha.
Ni vyema pia kutafakari mafanikio yako na kujipatia nafasi ya kuishi bila kufikiria yajayo wala yaliyopita. Tena jisamehe nafsi yako.
Unaweza kukabiliana na msongo kwa kujipa muda wa kutosha wa kupumzika na kulala usingizi wa kutosha, wanasema wataalamu.
Kushirikiana na wengine na kuwasaidia ili nawe usaidiwe ni moja ya mbinu wanazozitaja za kukabiliana na msongo.
Pia wataalamu wanashauri kujenga tabia ya kushukuru kwa kila jambo, ulichonacho na kuweka orodha ya mambo unayoshukuru.
Wanashauri kufanyakazi unazozipenda ili ziwe kama mchezo na kila siku uzifurahie.
KUMBUKA MAZOEZI
TANCDA wanashauri kuishi maisha ya mazoezi na kutaja baadhi ambayo unaweza kuyafanya nyumbani.
Mfano, wanasema ukiwa nyumbani kimbia mahali pamoja mfano kuzunguka sebuleni mara kadhaa, mengine ni kushuka na kupanda kwenye kiti.
Aidha, unaweza kunyoosha na kuinua mgongo na kiuno. Piga goti kwa kubadilisha miguu, anza na kulia, maliza piga wa kushoto mara kadhaa.
Mengine ni kunyoosha mikono na kuizungusha mabegani kwenda mbele na kurudisha nyuma mara kadhaa pia.
Mazoezi mengine wanayopendekeza na wataalamu wa TANCDA ni kuchuchumaa na kunyanyuka, pia kupiga pushapu, jingine ni kulala chali kisha kutumia vidole vya miguu na mikono kujinyanyua juu.
Zoezi jingine ni kuruka juu mara kadhaa, kucheza kamba na vyote vifanyike kila mara.
Wanashauri kuwa kwa kuzingatia mazoezi na ushauri wa kitaalamu watu wengi watapunguza msongo na pia magonjwa yasiyoambukizwa kadhalika kubakia na afya njema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED