LICHA ya kiwango cha kujua kusoma na kuandika kwa watu wazima kutajwa kuongezeka kutoka asilimia 78.1 mwaka 2012 hadi asilimia 83.0 mwaka 2022 kwa mujibu wa ripoti ya Takwimu za Msingi za Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi ya mwaka 2022 bado inaonesha kuwa asilimia 17 hawajuhi kusoma wala kuandika ‘mbumbumbu’.
Kadhalika idadi kubwa ya wanawake sawa na asilimia 20.5 wanatajwa kutokujua kusoma wala kuwandika tofauti na asilimia 13.2 upande wa wanaume nchi nzima hii ni kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022.
Hata hivyo tatizo hilo linatajwa kutokana na udumavu wa akili na afya kuanzia miaka sifuri hadi nane ambako kwa mujibu wa wataalamu wa malezi na makuzi ya watoto kipindi hicho mtoto anatakiwa kuwa chini ya uangalizi na kuchangamshwa akili pamoja na kupewa vyakula vinavyohitajika kwa umri huo ili kuchangamsha ubongo.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge na Uratibu), Dk.Jim Yonazi anasema zaidi ya watoto milioni tatu nchini wana tatizo la udumavu hali anayoitaja kuwa mbaya zaidi kwa watoto.
Kadhalika anasema kwa takwimu za mwaka 2022 za Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (TDHS) zinasema kiwango cha udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ilikuwa ni asilimia 30 huku zaidi ya watoto 600,000 wakitajwa kuwa na utapiamlo mkali na wakadili na kuwa ukondefu ukiwa ni asilimia 3.5 mwaka 2015 hali inayotajwa kuathiri mfumo mzima wa kiafya kwa mtoto pamoja akili kwa ujumla.
Taarifa ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa ya mwaka 2021 inaeleza kuwa hadi kufiki mwaka 2019 asilimia 14 ya watu dunia walikuwa hawajuhi kusoma wala kuandika huku zaidi ya Wanafunzi milioni 500 wakiachwa nyuma kwa kushindwa kuendelea kujifunza kusoma na kuandika.
Kadhalika ripoti ya mwaka 2023 inasema zaidi ya watu milioni 763, ulimwenguni hawajuhi kusoma wala kuandika tatizo ambalo linatajwa kuwa mzigo kwao katika shughuli zao za muhimu.
Septemba 4, 2024 Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga alikiri kuwepo kwa tatizo la wanafunzi wanaomaliza darasa la saba bila kujua kusoma wala kuandia na kueleza kuwa serikali inatarajia kuanzisha madarasa ya watu wasiojua kusoma wala kuandika.
“Takwimu za sensa zinaonesha asilimia 17 hawajuhi kusoma wala kuandika na hii idadi siyo ndogo kwa karne ya sasa ya kidigitali, hivyo katika maboresho yetu ya sera ya elimu pamoja na mitaala tuliyoyafanya mwaka jana jambo hili tumelizingatia.
Kipanga anasema madarasa hayo yataanzishwa katika kata na vijiji vyote na watawekwa maofisa elimu watakaokuwa na jukumu la kusimamia elimu hiyo.
MZIZI WAFUNULIWA
Mtaalam wa utengenezaji wa zana za kujifunzia na uchangamshi wa mtoto ambaye pia ni Mratibu wa Mradi wa Tuwaandae pamoja kutoka Shirika la Tanzania Early Childhood Education and Care (TECEC), Ester Macha anasema tatizo la akili na utambuzi kwa mtoto linaanzia pale akiwa bado tumboni.
Anasema muda huo kutaalam unatambulika kama miaka sifuri hadi minane na kuwa maandalizi yake yanatakiwa kuanzia hapo ili kupata mtoto anayeweza kutambua na kuelewa haraka kila kitu hatua inayoenda mpaka umri wa miaka nane.
Ester anaseama udumavu wa akili unasababishwa pia na malezi ambacho ndicho chanzo mama na kuwa eneo hilo linahusisha vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchangamshi wa awali wa mtoto kuanzia miaka 0-8 na kutokufanya hivyo kunasababisha mtoto kutokufikia vitu hivyo katika umri husika.
“Nini cha kufanya sasa kama tumeshaona tatizo hili ni kubwa ni vema tukaendelea kutoa elimu ya malezi na makuzi ya awali ya mtoto elimu itakayotoa vitu muhimu anavyotakiwa kuvipata mtoto katika umri mdogo ili kumtengeneza mtoto mwenye akili zaidi,”anasema Ester.
Aidha anasema miongoni mwa mambo yanayotakiwa kutolewa elimu ni pamoja na malezi yenye muitikio na ujifunzaji wa mapema kwa kuwafanyia watoto uchangamshi kupitia zana mbalimbali zinazopatikana nyumbani ili kumsaidia mtoto kutambua kusoma, kuandika na kuhesabu kupitia vitu vilivyopo nyumbani kabla hajaanza shule.
“Kama shirika tumekukitoa elimu hii katika jamii, shuleni hata kwa wazazi juu ya namna ya kukaa na watoto kuwaelekeza pamoja kuwafundisha kupitia kituo chetu cha malezi na makuzi ya mtoto kilichopo jijini Mwanza,” anasema
Pia anasema wamekuwa wakitengeneza zana pamoja na wazazi na kuwafuata wazazi wengine wajawazito katika vituo vya afya na kuwaelimisha juu ya kuzungumza na watoto tumboni pamoja na kutembelea familia na kuboresha mazingira ya ujifunzaji kwenye madarasa ya awali katika baadhi ya shule mkoani Mwanza,Mara na Arusha.
Kuhusu udumavu Mtaalam wa lishe kwa watoto ambaye pia ni Ofisa lishe kutoka TECEC, Jackson Yawi anasema udumavu wa akili unaweza kusababishwa na mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na lishe duni, mazingira yasiyo rafiki, na ukosefu wa elimu ya kutosha kwa wazazi.
Yawi anasisitiza umuhimu wa lishe bora katika kipindi cha ukuaji wa watoto na kuwa lishe bora inachangia katika maendeleo ya ubongo na uwezo wa kujifunza wa watoto na kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha watoto wanapata virutubisho vyote vinavyohitajika ili kuzuia udumavu wa akili.
Anasema katika makuzi ya mtoto afya ya akili na mwili ni vitu muhimu katika kumfanya mtoto awe na uwezo kiakili pamoja na utambuzi wa mambo.
Anasema jinsi Mtoto anavyopungukiwa baadhi virutubisho muhimu mwilini husababisha mtoto kuwa na uelewa mdogo hasa darasani hivyo anapaswa kupata vyakula ambavyo vinagusa makundi tofauti ili kumsaidia katika ukuaji wake hasa vyakula vyenye Vitamini ‘A’ mfano viazi lishe.
“Kadri mtoto anavyozidi kukua anapaswa kula walau milo minne kwa siku , ambapo mikuu ni milo mitatu ukijumuhisha na matunda na juice asili pamoja na maji, pia utumiaji wa aina moja chakula ni tatizo kwa sababu haukidhi mahitajia ya mtoto kilishe ambaye anapaswa kupata virutubisho vingine,” anasema Yawi.
Anasema kuna madhara mbalimbali ambayo anaweza kuyapata mtoto anayetumia aina moja ya chakula ni pamoja na utapiamulo ambao unaweza kusababishwa na lishe hafifu na lishe duni ambayo inachangia mtoto kuingia katika hali ya ukondefu, udumavu, upungufu wa madini chuma.
Alisema upatikanaji wa vyakula hivyo haviitaji uwezo wa mzazi bali ni kujali afya ya mtoto na kutafuta vyakula hivyo kulingana na mazingira wanayoishi.
“Unaweza ukawa na unga wa mhogo na mahindi,ukapika uji wako wa mahindi tu wakati wa kupika ukatupia yai moja uji ukiivya unampa mtoto au ukapika bokoboko unatumia mboga za majani unampa mtoto inasaidia " anasema Yawi.
Kadhalika anasema upo utamaduni wa wazazi kuandaa aina tofauti za nafaka na kutengeneza unga wanauita wa lishe ili hali wametumia aina moja au mbili pekee za vyakula ambako wangeweza kutengeneza uji wenye virutubisho vya aina tofauti kwa kutumia gharama hizo hizo.
“Tunahitaji kupata watoto wenye afya njema lakini siyo kwa uji wa mchanganyiko unaoitwa lishe ilihali umewekewa mahindi, mhogo, ulezi,soya pamoja na karanga ambavyo vyote kwa pamoja ni protini na wanga,” anasema Yawi.
Anasema mfano wa vitu muhimu vya kuweka katika uji wa mtoto ni pamoja na unga wa mahindi au mhogo (wanga), karanga au mayai mabichi (protini), ukwaju (vitamini C) pamoja na maziwa ambacho ni chanzo kizuri cha kalsiamu.
Meneja wa Mradi, Programu ya Uimarishaji Chakula kutoka Shirika la GAIN Tanzania, Archard Ngemela alisema ili kukabiliana udumavu nchini kuna uhitaji mkubwa wa jamii kupata unga uliorutubishwa.
Alisema katika kuisaidia jamii kupata unga wenye virutubisho shirika hilo limekuja na mradi wa mashine yenye uwezo kusindika unga kwa kuchanganya virutubisho muhimu ikiwa na lengo pia la kuzisaidia shule kupata huduma hiyo muhimu.
“Wazazi wamekuwa wakichanga mahindi shuleni kwaajili ya chakula cha watoto lakini wamekuwa hawapati unga uliorubtubishwa hivyo kufanya hali ya udumavu kwa watoto kuendelea kuwa kubwa nchini,”anasema Ngemela.
Anasema mashine hiyo imetengenezwa nchini na wadau wa PEC ikiwa na uwezo wa kutumia umeme wa nishati jua ili kumudu hali ya mazingira ya watu wasiyo kuwa na umeme.
Naye Meneja Mradi wa Afya na Lishe kwa kuzingatia usawa wa kijinsia kutoka shirika la World Vision Tanzania, Shukrani Dickson anasema bado jamii imeshika mila na desturi potofu zinazodidimiza mwanamke na kumfanya mwanaume kuwa na uamuzi wa kipi kitaliwa nyumbani na kwanini.
Shukrani anasema kukabiliana na hali hiyo iliyobainika katika mikoa ya Simiyu na Shinyanga, shirika hilo limeanza kumshirikisha kwa karibu mwanaume katika afua za lishe ili kuondoa ule utamaduni wa kuuza mazao na vitu muhimu vyenye lishe kisha kuiacha familia na chakula cha aina moja.
“Kupitia modo yetu ya ‘men care’ tunahakikisha tunatoa elimu kwa jamii hasa kwa wanaume kujua umuhimu wa vyakula vy asili kama vile mayai, kuku, choroko na vingine ambavyo mara nyingi wamekuwa wakiviuza na kuiachia familia mahindi pekee,”alisema Shukrani.
Mkurugenzi wa Shirika la TECEC, Joel Elphas anasema mpango wa kudumu walioanzisha kama shirika ni pamoja na kujenga kituo cha kudumu cha malezi na makuzi ya mtoto ambacho kinawaandaa watoto, wazizi pamoja na walezi katika kuhakikisha katika kipindi cha siku 1000 za ukuaji wa mtoto anajengwa kuwa na akili, uelewa, afya njema na kujiamini.
Aidha anataja matumizi ya vifaa janja kwa kwatoto ikiwemo simu, vishikwambi pamoja na televisheni kuwa miongoni vitu hatari kwa ukuaji wa ubongo wa mtoto na kuwa hatua hiyo inasababisha ubongo kudumaa na kutokuwa na mawazo na uwezo wa utambuzi.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dk.Jesca Lebba, anasema kwa sasa hali ya udumavu mkoani hapa ni asilimia 28, na kuwa miongoni mwa Halmashauri zinazokabiliwa na tatizo hilo zaidi kuwa ni Ukerewe, Buchosa, na Kwimba na kuwa jitihada zinafanyika kuboresha hali hiyo.
Anasema miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii katika mikusanyiko mbalimbali na vituo vya afya, kwa ushirikiano na serikali na wadau. Halmashauri zimeweza kutoa asilimia 92 ya fedha za lishe, na waandishi wa habari wanachangia kwa kutoa taarifa muhimu kuhusu lishe.
WAZIRI MKUU ANENA
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifunga Mkutano wa kumi wa wadau wa lishe nchini uliofanyikahivi karibuni jijini Mwanzaalisema hali ya lishe kwa watoto nchini hairidhishi kwani theluthi ya watoto nchini wana udumavu hivyo kutaka mikakati mahususi kutoka kwa wadau pamoja taasisi za serikali kukabili tatitizo hilo.
Majaliwa anasema takwimu hizo ni kwa mujibu wa Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (TDHS) wa mwaka 2022 na kuwa hali hiyo siyo ya kufumbia macho bali inatakiwa mikakati kulikabili.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED