Hatima ya biashara na uwekezaji Afrika anaporejea Rais Trump

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:31 AM Nov 08 2024
Rais Donald Trump.
PICHA: MAKTABA
Rais Donald Trump.

UTAWALA unaoondoka wa Rais Joe Biden unatajwa ulijaribu kujenga hisia kwamba, Afrika ilikuwa mshirika wa thamani na muhimu," anavyotamka W Gyude Moore, mshirika katika Kituo cha Maendeleo ya Dunia na waziri wa zamani wa Liberia.

Inaelezwa, msatafu Rais Biden, alijitahidi kupatanisha shauku hiyo na mikataba na ushirikiano mkubwa, lakini hiyo haimaanishi kuwa mkakati wake wa Afrika haukuwa na matunda.

Marekani ilisifiwa kwa kuwekeza katika Ukanda wa Lobito - njia ya reli inayopitia Angola, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Zambia, ambayo itatumika kusafirisha malighafi muhimu.

Mnamo mwaka 2023, Marekani ikasema imewekeza zaidi ya Dola za Marekani bilioni 22 tangu Biden aingie madarakani.

Lakini kuna wasiwasi kwamba ujio wa Rais Trump, anaweza kuondoa uwekezaji na biashara hii. Rais wa hivi karibuni ana mtazamo wa kulinda zaidi maslahi ya nchi yake, usio wa kawaida kuliko Biden.

Mkataba wa Ukuaji na Fursa ya Afŕika (AGOA), ambao umewezesha nchi zinazostahiki za Afŕika kuuza nje baadhi ya mazao yao kwenda Maŕekani bila kulipa kodi tangu mwaka 2000, unatajwa chanzo kikuu cha wasiwasi huo.

Wakati wa utawala wake uliopita, Trump alisema mpango huo hautaongezwa muda wakati utakapoisha mnamo 2025.

Na wakati wa kampeni yake ya 2024 aliahidi kutekeleza ushuru wa mapato wa asilimia 10 kwa bidhaa zote zinazotengenezwa na nchi za kigeni. 

Hiyo inaelezwa kwamba itafanya bidhaa zinazoagizwa kuwa ghali zaidi na hivyo wauzaji nje ya Afrika watakuwa na uwezekano wa kuuza mazao yao kidogo katika soko kubwa la Marekani.

Wachambuzi wengi nchini Afrika Kusini - mmoja wa wauzaji bidhaa nje wakubwa chini ya mkataba wa AGOA - wametabiri kuwa kukata mkataba wa AGOA kunaweza kuwa na athari kubwa katika uchumi.

Hata hivyo, taasisi ya ushauri ya Marekani ya Brookings inatabiri kuwa Pato la Taifa la Afrika Kusini litapungua kwa "asilimia 0.06 pekee". Hiyo kwa kiasi fulani ni kutokana na kwamba bidhaa nyingi ambazo Afŕika Kusini inauza nje kwenda Maŕekani kama vile madini na chuma hazifaidiki na Agoa, ilisema.

Ingawa Rais Donald Trump hakutaka AGOA, alitambua kwamba ikiwa Marekani itakabiliana na ongezeko la ushawishi wa kiuchumi wa China barani Afrika, ilihitaji kudumisha kiwango fulani cha ushirikiano.

Mwaka 2018 utawala wa Trump ulizindua Prosper Africa - mpango ambao unasaidia kampuni za Marekani zinazotaka kuwekeza Afrika na Shirika la Fedha la Maendeleo (DFC).

Ni shirika linalofadhili miradi ya maendeleo barani Afrika na duniani kote. Biden ameendelea kuuendesha baada ya kuchukua wadhifa wake na DFC inasema hadi sasa imewekeza zaidi ya Dola za Marekani bilioni 10 barani Afrika.

Ikizingatiwa kuwa China bado ina nguvu kubwa barani Afrika na kwamba Trump alianzisha sera hizo mwenyewe, kuna uwezekano mkubwa wa kufikiria mara mbili kabla ya kuzipunguza.

·    Kwa mujibu wa BBC