DIRA 2050: Ujenzi miji, vijiji ni holela kupindukia, iwekwe mikakati na viwango endelevu

By Gaudensia Mngumi , Nipashe
Published at 07:04 AM Sep 04 2024
Sehemu ya ujenzi holela kwenye Barabara ya Morogoro, Dar es Salaam.
PICHA: SABATO KASIKA
Sehemu ya ujenzi holela kwenye Barabara ya Morogoro, Dar es Salaam.

KWA mgeni anayetembelea Tanzania kwa mara ya kwanza, akishuka kwenye ndege, meli, au basi, anachokiona ni makazi duni, holela na yasiyopangika kila upande atakaotupa jicho.

Ujenzi huo duni na holela wa makazi unaopatikana kuanzia  mijini hadi  vijijini, ni dosari inayotajwa na mbobezi wa kusanifu majengo  Profesa mstaafu wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), Victor Chissanga.

Anasema:‘Tanzania is growing too informaly in,” akimaanisha ujenzi wa makazi ni holela kupindukia.

Anasema miji yote kuanzia Dar es Salaam ambalo ni jiji kuu hadi vijijini hakuna mipango na hilo ni janga kwa sababu hivyo kuwa nchi isiyozingatia mipango ya miji wala vijiji. 

“Tukumbuke miaka 50 ijayo vijiji vyetu vitakuwa miji mikubwa au midogo. Miji nayo itakuwa majiji. Mbona hatujali kanuni za mipango mijini na vijijini. Tunakwenda wapi?” Anahoji. 

 Anaeleza kuwa miji kukosa mpangilio inasababisha kwanza kuwa na sura mbaya na kuongeza shinikizo la ziada au ‘presha’  kufikisha huduma muhimu na za kimsingi kama maji, umeme, barabara na mawasiliano.

 Anasema majiji, miji mikuu, midogo na vijiji vinakuwa kiholela kiasi cha kushangaza wakati kuna wasomi wa mipango mijini na vijiji, wabunifu na wasanifu majengo wengi, wasio na kazi wakiachwa kuendesha bodaboda na kuuza mafuta ya magari vituoni au kufuga kuku.

“Jiji kuu la Dar es Salaam, majiji ya Arusha  Mwanza, Mbeya  na Tanga hayana mpangilio wa makazi, ujenzi holela unafanyika kwa kasi.  Ni vyema kuchukua hatua. Kupanga sehemu za makazi,  nyumba za aina tofauti, ghorofa fupi, ndefu, makazi ya viongozi, huduma za biashara, maduka, suparmaket, nyumba za ibada, shule na hospitali. Miji na vijiji visiachwe kukua kama uyoga au vinavyotaka vyenyewe.”

Anasema sehemu ambazo hazijapangwa zipangwe serikali isitegemee kufanya ‘upgrading ‘ au kuboresha, kunakohusisha kuvunja,  kubomoa na pia kufidia hatua ambayo ni gharama zaidi. 

 Anatoa mfano makanisa kuibuka  popote mijini yakijengwa kwa  viroba, maturubai na mabati machakavu  katikati ya miji  na majijini bila kuona Idara ya Mipango Miji na Vijiji ikichukua hatua.

Profesa Chisanga anatoa mfano wa kujenga kiholela mabanda ya biashara popote mchuuzi anapotaka, lakini pia kuna vibanda vya kuuza simu, nguo, vinywaji na pombe juu ya mitaro ya barabara.

Anasema ndani ya hifadhi ya barabara kumewekwa vibanda vya mama na babalishe popote pembeni ya barabara kuu za majiji na miji na vibanda na nyumba zisizopangika na za kienyeji mno.

Anataja gereji, makontena ya kuuza pombe na bidhaa  nyingine  mtu  anapoamua yanabandikwa popote na kuongeza: “Tunajiuliza hivi maofisa mipango miji na vijiji pamoja na  idara ya upimaji wa ardhi na ramani wanachukuliaje hali hiyo?”

Profesa Chisanga aliyefanyakazi Chuo Kikuu cha Ardhi na vyuo vikuu vingine anakumbusha kuwa  miji na vijiji visiyopangwa  leo 2024 ndiyo majiji, miji mikuu na midogo ya kesho hivyo Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, iwajibike.

UPIMAJI ARDHI

Mtaalamu huyo anasema wananchi wanataka kujenga lakini hakuna ardhi iliyopimwa na hiyo ndiyo sababu ya kujenga kiholela, kuanzia Dar es Salaam hadi vijijini.

Anakumbusha kuwa  Tanzania ni ya kwanza kuwa na chuo kikuu cha ardhi katika ukanda wa  Mashariki na Kusini mwa Afrika  lakini inashangaza kuwa ni nchi inayoongoza  kwa makazi holela, duni  na ukosefu mkubwa wa mipango miji na vijiji. 

Makazi ya binadamu yana ngazi saba kwa Tanzania  ikianza na majiji, miji mikuu ya mikoa miji mikuu ya wilaya, makazi ya tarafa, kata vijiji na vitongoji, anaeleza. 

“Inashangaza ngazi zote ni ujenzi holela ambao hauzingatii mipangilio  kuanzia barabara,  usafirishaji, huduma za kijamii, miundombinu ya kibiashara na matumizi bora ya ardhi.” Anasema msomi huyo.

“Inasikitisha kuanzia jiji kuu ‘mega city’ Dar es Salaam hadi kitongoji kilichoko mpakani Tunduma havijapangwa. Kuna wasomi wa mipango miji, wachora ramani, wasimamizi wa makazi  na wasanifu majengo  hawaajiriwi. Wapate kazi watimize jukumu hilo.”  anaongeza.

ELIMU ITOLEWE

Violate Mafuwe ni mbunifu wa majengo, anayefanyakazi Dar es Salaam, anasema kukosekana mipango miji na vijiji ni tatizo la kitaifa akishauri kupanga kuanze sasa.

Hata hivyo, anasema kabla ya yote elimu ya mipango miji na vijiji elimu itolewe ili watu wafahamu umuhimu, kisha washirikiane na mamlaka  na Wizara ya Ardhi na Makazi kupanga maeneo yao. 

“Watu wanatakiwa kuelimishwa athari za makazi holela, duni na namna ya kuyaepuka. Iwafikie wote walioko mijini na vijiji na waelezwe kuhusu sheria na kanuni zake.”

Msanifu huyo anasema licha ya kwamba upangaji miji ulikosewa  au kukosa kipaumbele miaka mingi iliyopita ni vyema kuanza sasa kutumia wataalamu kupanga na kuboresha makazi mijini na vijijini.

Viollet anashauri kuwa na vijijini vyenye mpangilio wa makazi, serikali ibainishe ardhi au inunue kabla haijapanda thamani ianze kuweka alama za miundombinu ya mabomba ya maji, nguzo za umeme, gesi, mkongo wa taifa na hifadhi ya barabara.

Kadhalika ipange makazi kwa kuzitambulisha sehemu za kujenga nyumba za viongozi, nyumba za kisasa zaidi, za gharama nafuu,  hospitali na vituo vya afya, shule, masoko, majosho ya vijiji, matangi ya maji, dampo za taka, viwanda, maeneo ya wazi  na nyumba za ibada.

“Ni vyema kuwa na maofisa mipango miji na vijiji wasimamie kufikia ujenzi wenye viwango  kwani maendeleo ya vijiji na miji yasiposimamiwa yana athari kimazingira.” 

Anakumbusha kuwa Tanzania ina ardhi ambayo haijaguswa bado akitaka ipangwe kabla ya kuchukuliwa na kupanda zaidi thamani.

DIRA IWEKE VIWANGO

Erasmus Kiwango ni msanifu na mbunifu wa majengo, anayezungumzia umuhimu wa taifa kuandaa  mpango endelevu wa ukuaji na upangaji miji na vijiji.

Anashauri dira ya taifa 2050 ianishe suala hilo na lifanyiwe kazi kama juhudi zinavyofanyika kujenga barabara, madaraja na reli na kufikisha maji na umeme kwenye makazi. “Dira iweke viwango maalumu vya ujenzi na ukuaji wa miji  na kuwe na utashi wa kisiasa kutimiza hatma hiyo,” anasema Kiwango.

Anazungumzia kujenga miji mipya nje ya  majiji iliyopangika yenye huduma zote ili kuondoa msangamano unaotokana na ujenzi holela wa majiji na miji mikuu.

Anasema miji hiyo inaweza kujengwa  mikoa jirani kama Tanga na Pwani kupunguza msongamano Dar es Salaam.

Akiita ‘setilite cites’  kiwango anashauri katika maeneo hayo yawekwe masoko makubwa kama Kariakoo, hospitali za kitaifa na za rufani za kikanda, benki na chochote muhimu ili kuepusha kukifuata kwenye jiji.

Aidha, anasema kuwe na huduma za usafiri kuanzia miundombinu ya barabara na reli ili kuwapo na  treni na mabasi ya mwendokasi, kielimu viwepo vyuo vikuu na shule za aina mbalimbali na  makazi ya kila aina ya nafuu au juu zaidi.

Kiwango anasema makazi hayo ni kwa ajili ya wafanyakazi wa majiji ili waishi nje ya jiji lakini waweze kuwahi kazini na kurudi makwao muda wote.

Anashauri suala hilo lianze kufanyiwa kazi kupunguza msongamano Mwanza,  ECOSKY Builders  

Kiwango cha Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya ECOSKY Builders ya Dar es Salaam, anasema pia ni bora kujenga miji kama  Kibaha, Bagamoyo, Kigamboni na Chalinze na kuipa huduma muhimu ni suluhisho kupunguza msongamano na makazi holela.

“Ili kuwa na miji na vijiji vilivyopangwa ni lazima kushirikisha wananchi kwa sababu ardhi inamilikiwa na watu  au mtu mmoja mmoja hivyo wanahitaji elimu kuelewa umuhimu wa kuruhusu ardhi hiyo kupangwa na kuwa na makazi bora,” anashauri.

Hata hivyo anasema Dira ya Maendeleo 2050 iweke kipaumbele kuwa na mipango endelevu ya mipango na ukuaji miji na vijiji.

 Anasema idadi ya watu inapoongezeka huduma nazo zitahitajika hivyo ni lazima kuzipanga na kuziwekea maeneo ya kuziweka.