Awamu ya Sita ilivyopokea ‘hodi’ Korona 19, hadi hatua ya ushindi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:59 AM Jun 20 2024
Rais Dk. Samia Suluhu hassan, alipozindua kampeni ya kitaifa kukabili maradhi ya Korona 19, 21.
PICHA: MTANDAO.
Rais Dk. Samia Suluhu hassan, alipozindua kampeni ya kitaifa kukabili maradhi ya Korona 19, 21.

WAKATI kilio cha kuzuka maradhi ya Uviko 19 duniani mwaka mmoja kabla ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani, utata ulizingira wa ama kuwapo au kutokuwapo maradhi hayo nchini. Baadaye ikawa rasmi kwamba upo.

Lakini, kupita mwaka mmoja akiwa madarakani, Rais Dk. Samia, ambaye alishatumikia miezi kadhaa kupokea nafasi ya mtangulizi wake, marehemu, Dk. John Magufuli, akatoa ufafanuzi wa kuukabili. 

Akaanza na wito kwa wananchi wote “kila mmoja kwa nafasi yake kulinda afya, kwani ulinzi huo unaanza na mtu mwenyewe.”

Ni kauli yake akiwa Bungeni jijini Dodoma, katika hotuba yake wakati akielezea hali ya afya na hatua ambazoTanzania imezichukua kukabiliana na ugonjwa wa Korona 19. 

Rais Dk. Samia akafafanua: “Ugonjwa huu umeathiri dunia nzima na mbaya zaidi ni kwamba janga hili linapungua na kurudi katika mifumo tofauti tofauti.

‘Mpaka sasa bado hakujawa na dalili za kupatikana kwa tiba ya maradhi haya. Njia pekee iliyopo ni kujikinga na kuchukua hatua mbalimbali za tahadhari.”

Akaendelea: “Hapa nchini tumekuwa tukifuata miongozo kadhaa ya kinga inayotolewa na wataalamu na kwa kutumia njia zetu za tiba asilia tumeweza kwa kiasi kikubwa kushusha kiwango cha maambukizi.

“Hapa nchini tumeamua kuunda Kamati ya Wataalamu ambao kwa kushirikiana na taasisi za Afya Duniani na zile za kikanda za EAC (Jumuiya ya Afrika Mashariki) na SADC, wataliangalia suala hili kwa undani, kufanya uchambuzi wa kina na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua na jinsi ya kuendelea kupambana na maradhi hayo.”

Hadi sasa hatua zilizochukuliwa ni mbinu za kimataifa zikiwamo watu kuchanjwa mara ya kwanza na sasa iko awamu ya pili, watu kuwa na uhakika wa kinga za miili yao. 

Ufafanuzi wa kitaalamu wa mwanzo, ulijumuisha mhusika mkuu, Wizara ya Afya kupitia kwa Dk Leonard Subi, Mkurugenzi wa Kinga, aliyewataka wananchi kuvaa barakoa, kutumia vitakasa mikono na kunawa mikono kwa kutumia sabuni, ikiwa ni kanuni ya kinga, akidokeza kugundulika virusi vyake kutoka nchi jirani.

"Maambukizi yanaongezeka maradufu kuliko ilivyokuwa wimbi la pili," akafafanua.

HATUA KUBWA 2022

Mnamo Machi mwaka, 2022 Rais Dk. Samia kwa mara nyingine akazungumzia hali ya maradhi Uviko 19, akisema serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za dini na wanataaluma wa afya, imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Hatua zake akazitaja zimezingatia mazingira na hali ya jamii, ikiwamo kuruhusu wananchi kuendelea kujitafutia kipato chao, yaani kutokuwapo vikwazo kama nchi nyinginezo.

Hiyo inatajwa hadi kufika Machi 2022, jumla ya watu 33,789 walishathibitika kuwa na maambukizi ya UVIKO - 19 na kati yao 803 walipoteza maisha nchini.

Hatua zilizochukuliliwa na serikali ni pamoja na kuwaondoa hofu wananchi mlipuko wa ugonjwa huu, kufunga shule, vyuo na taasisi za elimu ya juu.

Hiyo akaitaja inaendana na kutoa elimu kwa jamii namna ya kujikinga na kuhimiza jamii kusitisha mikusanyiko isiyokuwa ya lazima.

Vilevile akasema, kuimarishwa ukaguzi na uchunguzi wa afya kwa wasafiri katika viwanja vya ndege, bandarini na mipaka ya nchi kavu, kuzuia kuingizwa maambukizi mapya, huku kukiimarishwa mchango wa tiba asili. 

Hayo yalikuwa yanafanyika katika Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii na Maabara katika Hospitali za Kanda za Bugando, Mbeya na Hospitali za Rufani za mikoa ya Dodoma, Arusha, Kigoma, na katika Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.

Hiyo ikaendana na kusimikwa mitambo 15 ya hewa tiba ya Oksijeni katika hospitali mbalimbali nchini. Pia, serikali imeendelea kuikinga jamii kuwezesha upatikanaji wa chanjo.

Waziri akafafanua miaka mwili iliyopita; “Wananchi, narudia kusisitiza kuwa UVIKO-19 bado upo na hutokea kwa mtindo wa mawimbi yanayoambatana na mabadiliko mbalimbali. Kila mmoja wetu anao wajibu wa kushiriki katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu.

“Nitumie fursa hii kuwashukuru sekta mbalimbali ndani ya serikali, wadau wa maendeleo, viongozi wa dini, viongozi wa kijamii na makundi mbalimbali ya kijamii kwa kutuunga mkono katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu. 

“Afya (Wizara) itaendelea kushirikiana na wote katika kuhakikisha tunaudhibiti ugonjwa huu. Hata hivyo, badala ya kupambana na ugonjwa huu peke yake, mwelekeo wetu sasa ni kuendelea kutoa huduma za kudhibiti Uviko -19 kupitia huduma nyingine jumuishi,” anasema.

Hapo Waziri Ummy, anazifafanua kwa mifano ya tiba Kifua Kikuu, Huduma za Mama na Mtoto, huduma za VVU/UKIMWI, Malaria magonjwa yasiyoambukiza

Lakini hatua iliyofikiwa sasa ni kwamba, huduma hizo zinapatikana kila mahali, ikiwamo katika ngazi ya vituo vya afya takriban vyote, binafsi na vya serikali msingi wa hoja kama alivyotambulisha Rais Dk. Samia, ni ushiriki wa pamoja na uwezeshaji kufikisha huduma tajwa.

Hiyo katika sura ya pili inaundwa katika Sera ya Afya nchini, inayotokelezwa kwa karibu sana na Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM), iliyobuniwa mwaka 2007 na kuanza kazi mwaka uliofuata.

MPANGO& PESA UVIKO

Kimsingi, dalili zake maradhi Uviko 19: -Homa kali; mgonjwa anajihisi kuchoka; anakohoa; anapata shida ya kupumua; vilevile kujihisi misuli imechoka.

Tanzania ilishawajibika na kunufaika na mradi wa miezi tisa, ilipotekeleza Mpango wa Serikali wa Kuinua Uchumi na Kukabiliana na Janga la Korona, uliopangiwa bajeti shilingitrilioni 3.62. Ulizinduliwa na Rais Dk. Samia, jijini Dodoma Oktoba, 2021.

Hapo Rais akaitaka Wizara ya Fedha na Mipango, pamoja na taasisi nyinginezo zitakazonufaika na fedha za mkopo wa shilingi trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF), kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Aidha, akaitaka sekta binafsi kutumia fursa hiyo, kwa kuzalisha bidhaa zitakazotumika katika utekelezaji wa miradi hiyo, mfano uzalishaji wa saruji, mabati na nondo, kusiwapo sababu ya kuchelewa kutumia fedha hizo.

Akaagiza miradi hiyo itekelezwe na makandarasi wazawa, ili fedha hizo ziendelee kubaki na kuzunguka katika uchumi wa nchi, huku akiwaelekeza makandarasi wazawa kuwajibika kwa tija.

Katika mpango huo, akataka kupunguzwa urasimu katika ununuzi wa vifaa vya miradi hiyo, agizo ililomfikia pia, Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu Nchemba kusimamia na kuondoa urasimu wa misamaha ya kodi katika vifaa na bidhaa zitakazotoka nje.

Vilevile, akamuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Mkaguzi wa Hesabu za ndani, kufuatilia kwa karibu matumizi ya fedha hizo ili malengo na thamani halisi iweze kuonekana.

Pia, Dk. Samia akazitaka Kamati za Bunge, kuisimamia kikamilifu miradi hiyo wakati wa kuitembelea, agizo linalowashukia nao wakurugenzi wa halmashauri zote nchini, pamoja na timu zao za kazi, kuhakikisha wanasimamia vizuri fedha hizo zilete tija katika miradi hiyo.

Zao la yote hayo, ndio sasa linaibua ufafanuzi wa kuwapo matokeo na huduma zinazobeba jina ‘Miradi ya fedha za korona.’