EWURA yashusha bei za mafuta

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 02:23 PM Oct 02 2024
EWURA yashusha bei za mafuta
Picha:Mtandao
EWURA yashusha bei za mafuta

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), kutoa bei kikomo za rejareja na jumla za mafuta ambazo zimeanza kutumika rasmi usiku wa kuamkia jana katika Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dk, James Mwainyekule, bei kikomo ya rejareja katika bandari ya Dar es Salaam kwa lita ya Petroli itakuwa 3,011, Dizeli 2,846, Mafuta ya taa 2,943, Tanga Petroli 3,016 Dizeli 2,859 Mafuta ya taa 2,989 na Mtwara Petroli 3,016 Dizeli 2,862 Mafuta ya taa 3,016. 

Amesema bei kikomo za jumla kwa lita katika bandari ya Dar es Salaam kwa Petroli 2,880.15 Dizeli 2,714.83 Mafuta ya taa 2,812.20, Tanga Petroli 2,884.77 Dizeli 2,728.21, Mtwara Petroli 2,884.93 na Dizeli 2,730.38.

“EWURA inapenda kuwakumbusha wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kwa jumla na rejareja pamoja na jamii kuzingatia bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli kwa eneo husika zinazopatikana kupitia simu za mkononi kwa kupiga namba *152*00# na kisha kufuata maelekezo. Huduma hii ni bure na inapatikana kupitia mitandao yote ya simu za mkononi hapa nchini, amesema.

Ameongeza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, kifungu namba 166, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko. Na kwamba EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta.

Pia amesema kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani isipokuwa bei hizo zisizidi bei kikomo au kuwa chini ya bei iliyoruhusiwa kama zilivyokokotolewa kwa mujibu wa kanuni za EWURA za kupanga bei za mafuta za mwaka 2022 zilizotangazwa Januari 28, 2022.

Aidha, Dk. Mwainyekule amesema vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.

“Wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani. Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja. Adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika,” amesema.

Hata hivyo amesisitiza kuwa wauzaji wa bidhaa za mafuta ya petroli wanatakiwa kutoa stakabadhi za mauzo kutoka kwenye mashine za (EFPP) na wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.

Amehimiza kuwa stakabadhi hizo zitatumika kama kidhibiti kwa wanunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au kuuziwa mafuta yasiyo na kiwango cha ubora unaotakiwa.

Vile vile, amesema stakabadhi hizo pia zitasaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi za serikali zitokanazo na mauzo ya bidhaa za mafuta ya petroli.