Ado Shaibu ataja sababu nne za kuipinga CCM Kagera

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:32 PM Oct 02 2024
Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Ado shaibu
Picha: Mtandao
Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Ado shaibu

Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Ado shaibu ametaja sababu nne za kukipinga Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kagera.

Amesema Mosi ni umasikini, ambapo amedai kuwa serikali ya CCM imewaangusha wananachi wa Kagera kwa kueleza kuwa kila mwaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inatoa ordha ya mikoa masikini ambapo mkoa huo unashika namba moja.

"Umaskini, serikali ya CCM imewaungusha sana wananchi wa Kagera, Benki kuu ya Tanzania kila mwaka huwa inatoa orodha ya mikoa ambayo ndio masikini zaidi Tanzania, na ajabu ya Mwenyezi Mungu Kagera hii yenye ardhi ya rutuba, ina mito, ina mabwawa, ina maziwa, ina madini, ina mbuga ina utajiri wa kila namna lakini mikoa maskini ikitajwa Kagera lazima iwe namba moja au namba mbili" amesema 
 
Ado, ametaja sababu ya pili kuwa ni;  "Serikali ya CCM imeweka mpango wa kusaidia kaya masikini lakini kila nilipokwenda Kagera nimekuta ubabaishaji mkubwa kwenye TASAF kwanza wanaostahili kupata wanaondolewa na wasiostahili wengi wanawekwa."

Sababu ya tatu ameitaja kuwa ni; "Michango mashuleni, CCM inasema kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha sita elimu ni bure. Ni maneno matupu. Wameondosha ada tu lakini michango kila siku inaongezeka na hii ni kwa sababu Serikali haitengi fedha za kutosha za uendeshaji wa mashule zinaitwa capitation. Walimu kama hawapati fedha za kutosha wanakimbilia kwenye michango."

Ado ameitaja sababu ya nne kuwa ni; "Afya, CCM walisema wanawake wajawazito matibabu ni bure, watoto chini ya miaka mitano matibabu ni bure, wazee wa miaka sitini matibabu ni bure. Nenda hospitali ukajionee mambo bila maokoto hawakuelewi"