KONGAMANO la 10 la Jotoardhi Afrika linatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 21-27, Mwaka huu lenye lengo la kuchangiza azma ya serikali ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Mathew Mwangomba akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, amesema Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na TGDC pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira (UNEP) wameandaa kongamano hilo.
Amesema kongamano hilo linatarajiwa kufunguliwa na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango na kufungwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na lina kauli mbiu isemayo "Kuharakisha Maendeleo ya Rasilimali za Jotoardhi katika Afrika, Masoko ya Gesi ya Ukaa na Upunguzaji wa Gesi ya Ukaa".
Amesema kaulimbiu hiyo inasadifu azma ya Serikali kupitia Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia.
Mwangomba kongamano hilo linatarajiwa kuwa na washiriki takriban 1000 kutoka nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Msumbiji, Djibouti, Newzealand, Japan, Iceland, Marekani, Canada na Saudi Arabia.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED