Biteko atangaza neema kushuka bei gesi ya kupikia

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 07:58 AM Sep 14 2024
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko
Picha:Mpigapicha Wetu
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amesema serikali inafanya kila linalowezekana kushusha bei ya gesi ya kupikia, ili ipatikane kwa gharama nafuu kwenye maeneo yote nchini.

Amesisitiza kuwa wananchi wanataka huduma bora, vyeo na mamlaka walizonazo havina maana kama watanzania watapata huduma hafifu.

Dk. Biteko aliyasema hayo jana jijini hapa katika hafla ya uzinduzi wa jengo la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na utiaji saini mikataba sita ya utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi za kupikia.

 Miongoni mwa mikataba hiyo ni wa kusambaza mitungi 450,000 ya gesi ya kilo sita katika maeneo ya vijiji na pembezoni mwa miji utakaotekelezwa na kampuni za Manjis, Oryx, Lake Gas na Taifa Gas ambapo serikali kupitia REA, itatoa ruzuku ya hadi asilimia 50 kwa wananchi ili kununua mitungi hiyo.

 Naibu Waziri Mkuu alisema Rais Samia Suluhu Hassan amewapa maelekezo mahsusi, kwamba waangalie kila aina ya fursa iliyoko ya kufanya nishati safi ya kupikia ipatikane kila mahali na watanzania waipate.

“Kuna wakati mtu anaonesha ugumu, anasema ajenda hamuiwezi kwa sababu bei ni kubwa, ni kweli ni kubwa lakini serikali inafanya kila linalowezekana kuishusha ili nishati hii ipatikane kwa unafuu katika maeneo yote.

“Tumeanza na hii mitungi zaidi ya 400,000 itakayopatikana kwa bei ndogo na ziko nishati nyingine ambazo zinapatikana kwa bei nafuu,” alisema.

Kuhusu mikataba iliyotiwa saini, Dk. Biteko alitaka ikawe kichocheo kwa kuhakikisha kwamba, malengo ya serikali ya kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

“Itakuwa aibu sana leo kutia saini hapa halafu baada ya muda watanzania wasione matokeo, watanzania wanatarajia kuona matokeo ya haraka nishati safi ya kupikia ni ajenda ya kuokoa maisha ya watu,”alisema.

Kadhalika, alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, kuhakikisha majengo yote ya wizara yanatumia nishati ya umeme jua na kuwa mfano kwa taasisi zingine za serikali, ili kupunguza gharama za uendeshaji.

 “Sisi wizara ambao tunawaambia watu kila wakati tutumie nishati safi, hivi ni kwa kiasi gani sisi katika ofisi zetu tunatumia nishati safi, ninataka nione majengo yote ya wizara tuwe mfano wa kutengeneza ‘provision ya solar’ ili mchana tutumie solar, usiku tena mara nyingine hata usiku hatupo matumizi yawe kidogo tuwe mfano kwa taasisi nyingine za serikali tuanza sisi,” alisema.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, alisema magereza yameanza kutekeleza matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuondokana na matumizi ya kuni kama chanzo kikuu kwa asilimia 98.

Alisema jeshi hilo lilianza kuhama katika matumizi hayo kuni na mkaa baada ya kubaini madhara na ilianzisha mradi wa matumizi majiko banifu ambayo yalipunguza matumizi ya kuni kwa asilimia 40 kati ya mwaka 2016 hadi 2019.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, alisema mikataba hiyo sita yenye thamani ya Sh. bilioni 72.8, pia inahusisha kujenga na kusambaza mifumo ya nishati safi katika Jeshi la Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Kuhusu jengo la REA, alisema limejengwa kwa miezi 18 kwa gharama ya Sh. bilioni 9.8 badala ya Sh. bilioni 13 iliyopangwa awali na hivyo kuokoa kiasi cha Sh. bilioni 3.2.