Mkuu wa Polisi ahukumiwa kifo kwa kumuua mwandamanaji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:31 PM Mar 28 2024
Maandamano ya Iran mwaka 2022.
PICHA: MAKTABA
Maandamano ya Iran mwaka 2022.

MAHAKAMA ya Iran imemuhukumu kifo Mkuu wa Polisi kaskazini mwa Iran baada ya kushtakiwa kwa kumua mtu wakati wa maandamano makubwa mwaka 2022.

Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuwa, Mkuu wa Polisi, Jafar Javan mardi, alikamatwa mwezi Desemba mwaka 2022 kutokana na mauaji ya mwandamanaji wakati wa maandamano makubwa yaliyochochewa na kifo cha Mahsa Amini akiwa chini ya ulinzi wa polisi.

Amini mwenye umri wa miaka 22, alifariki mwezi Septemba 2022 akiwa chini ya ulinzi wa polisi kufuatia kukamatwa kwake kwa madai ya kukiuka sheria kali ya nchi kuhusu mavazi kwa wanawake.

Javanmardi amehukumiwa kifo “kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu ya kulipiza kisasi, inayojulikana kama ‘qisas sharia’, kwa shtaka la mauaji ya kukusudia,” wakili wa familia ya mwathirika, Majid Ahmadi, aliliambia gazeti linalotetea mageuzi la Shargh.

Mwandamanaji, Mehran Samak, mwenye umri wa miaka 27, alifariki kutokana na majereha aliyoyapata baada ya kupigwa risasi wakati wa maandamano katika mji wa kaskazini wa Bandar Anzali tarehe 30 Novemba, mwaka 2022.