Burkina Faso yaishutumu Ivory Coast kwa kukaribisha wahujumu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:07 AM Apr 28 2024
Mkuu wa Utawala wa Kijeshi wa Burkina Faso, Ibrahim Traore.
PICHA: MAKTABA
Mkuu wa Utawala wa Kijeshi wa Burkina Faso, Ibrahim Traore.

MKUU wa Utawala wa Kijeshi wa Burkina Faso, Ibrahim Traore, ameishutumu Ivory Coast kwa kuwakaribisha wahujumu wote wa nchi yake, ambapo amesema kuwa kulikuwa na tatizo na mamlaka mjini Abidjan.

Hivi karibuni uhusiano kati ya nchi hizo mbili umekuwa ukiyumba, na Aprili 19 mawaziri wa ulinzi kutoka nchi hizo mbili, walifanya mkutano katika mpaka huo kwa lengo la kuleta “mwanzo mpya” katika mahusiano.

Akiizungumzia Ivory Coast katika mahojiano na kituo cha televisheni cha taifa RTB, Traore amesema “wahalifu wote wapo na hawajifichi”. Ameongezea kuwa kuna wakati lazima tuache unafiki na kusema ukweli, kuna tatizo na mamlaka ya nchi hii.

Serikali ya Traore ilichukua madaraka katika mapinduzi ya mwaka 2022 na tangu wakati huo imejitenga na mtawala wa zamani wa kikoloni Ufaransa, ikipendelea mahusiano ya karibu na tawala nyingine za kijeshi katika eneo hilo, pamoja na Russia. Akizungumza kuhusu Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara, Traore amesema hana mawasiliano maalum na yeye.