Makonda awaomba wananchi kujitokeza Mei Mosi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:32 AM Apr 28 2024
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki kilele cha siku ya wafanyakazi itakayofanyika Mei Mosi mwaka huu kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Makonda ameyasema hayo jana alipokuwa anazungumza kwenye kikao kazi cha maandalizi kuelekea siku ya wafanyakazi duniani kilichofanyika  ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Arusha.

Amesema uwepo wa shughuli hiyo ya kitaifa mkoani humo ni fursa kubwa kwa wakazi wake katika kuchangamkia fursa, hivyo uongozi wa mkoa huo umeandaa eneo maalumu kando ya uwanja wa Sheikh Amri Abeid kwa ajili ya kutumiwa na wajasiriamali kufanya biashara zao.

Amesema uwepo wa siku ya wafanyakazi   unaashiria uhuru na haki za wafanyakazi mahala pa kazi .

"Ni vyema wananchi wakatambua kuwa ushiriki wao utawaongezea morali watumishi katika kuhudumia jamii tunawomba wajitokeze kwa wingi kuhudhuria siku hii maalum ya wafanyakazi," amesema Makonda.

Naye Rais wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, amemshukuru Makonda kwa kuitisha kikao kazi hicho ambacho kimesaidia kuongeza msukumo na kasi kwa watumishi na wananchi kushiriki kikamilifu kwenye shughuli mbalimbali zinazofanyika mkoani humo kama sehemu ya shamrashamra za kuelekea siku ya wafanyakazi duniani.

Ametaja baadhi ya shughuli zinazofanyika kuwa ni mashindano ya michezo ya aina mbalimbali yanayoendelea kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, maandalizi ya riadha, maonyesho yanayoendelea kwenye viwanja vya General Tyre yaliyoandaliwa na Wakala wa usalama na afya mahala pa kazi (OSHA) ambayo yanatarajiwa kufungwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Doto Biteko, Aprili 28 mwaka huu.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Justine Masejo, amesema jeshi la polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalamakuimarisha usalama kwenye kila kona ya mkoa huo.

Amesema wananchi hawapaswi kuwa na mashaka yoyote ya kiusalama wakati huu ambao idadi ya watu imeongezeka maradufu kwenye jiji la Arusha.